Thursday, April 26, 2007

TUFANYEJE?

Kama kuna faraja yoyote ambayo nimeipata tangu nilipoiweka hadharani picha ya watoto-wanafunzi waliokalia mawe hivi majuzi (kama hujui nazungumzia nini bonyeza hapa) ni jinsi gani sote tumekerwa na kudhamiria kufanya kitu ili kubadili hali hii.Maoni yaliyomiminika, simu mlizonipigia baadhi yenu, barua pepe mlizonitumia zilitosha kunihakikishia kwamba vita hii inawezekana kupiganwa.Tunachohitaji sasa ni kuazimia kuianza rasmi.

Serikali zetu, tawala na zote zilizopita haziwezi kukwepa lawama kwa kushindwa kwake vibaya katika kuleta mabadiliko ya kijamii yanayostahili,yaliyo ya haki na yanayotarajiwa.Tunapoongelea serikali tunaongelea suala zima la uongozi.Tunakuwa na viongozi ili sio tu kuheshimu dhana nzima ya demokrasia bali pia kupata watu wa kutusaidia katika kuijenga dira, kuleta mabadiliko ya kijamii, na kuzivusha jamii zetu kutoka upande mmoja mpaka mwingine.

Picha ya watoto-wanafunzi waliokalia juu ya mawe, ndani ya jengo chakavu kabisa huku wakionekana na kuwa na kila dalili ya njaa, ukosefu wa matumaini na ambao inaonekana jamii imewasahau imetukera, imetuhuzunisha na kutukumbusha wajibu mzito tulionao kama watanzania.

Ukiwauliza jamaa wa serikalini,viongozi,wabunge,mawaziri nk hawatokosa majibu. Hiyo ndiyo sheria ya kwanza ya taaluma ya siasa. Usishangae pia ukisikia lawama zikienda kwa wafadhili, IMF na Benki ya dunia na mara nyingine kwa kufoka kabisa,wakiwatupia wananchi lawama.Imeshatokea hata mwananchi kukabiliwa na kifungo kwa sababu alimuuliza mbunge wake swali gumu!

Japokuwa naafiki kuna mantiki fulani katika kuzitupia lawama jabali hizo za masuala ya fedha duniani kuhusiana na mustakabali mzima wa maendeleo, zaidi naamini kwamba wanasiasa na viongozi wetu siku hizi wanazitumia zaidi kama ngao ya kukwepa lawama na majukumu tu.Yapo mambo chungu mbovu ambayo yanawezekana bila kutegemea ufadhili wa mtu au nchi yeyote.Mbona hata hayo hayafanyiki? Tuna viongozi kweli? Kama serikali yetu inatoza kodi, inapiga tambo za kukua kwa uchumi na wakati huo huo inaweza kuwapatia viongozi wake vitendea kazi vyenye thamani kubwa mara dufu kushinda sio tu kipato chao bali pia kipato cha taifa, inashindwa vipi kuhudumia sekta muhimu kama ya elimu?Tunapata wapi fedha za kutupa kwenye kashfa nzito kama Richmond na ununuzi wa rada lakini tukashindwa hata kuwachongea wanetu madawati achilia mbali kuwapatia walimu na vitendea kazi vingine?

Tufanye nini? Hili ndilo swali ambalo hatuna budi kusaidiana kulijibu kwa pamoja. Jambo la kwanza ambalo naamini tunaweza kulifanya ni kutochoka kuhoji,kukemea na kusaidia kwa kutoa mchango wetu wa hali na mali. Tusiishie kuandika tu huku kwenye mitandao na wakati mwingine kutupiana lawama hata miongoni mwetu sisi wenyewe.Jambo moja ambalo ni muhimu sana ni kumuuliza mbunge kwa mfano wa jimbo hilo la Morogoro Kusini Hamza Abdallah Mwenegoha kwanini hali katika jimbo lake ni ya kukatisha tamaa na kutia aibu kwa kiwango kile? Binafsi nimeshafanya hivyo kwa kumuandikia barua pepe nikiambatanisha picha ile na kuhoji kwa kina,kulikoni? Ingawa bado sijapata majibu na pengine sitopata majibu kamwe nina uhakika kwamba ujumbe umemfikia na hivyo atatambua kwamba dunia inamtizama. Ukipenda kumtumia barua pepe pia unaweza kwa kutumia anuani ya hmwenegoha@parliament.go.tz
Usiishie kwa Mwenegoha peke yake bali pia mbunge wa jimbo
lako, kule utokako au kule ilipo familia yako,asili yako nk. Kwa bahati nzuri anuani za barua-pepe,simu za nyumbani, za ofisini, za kiganjani za wabunge wetu zimeorodheshwa katika tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Utaratibu mwingine wa kusaidia ni ule wa hali na mali. Ingawa ni vigumu kujua taasisi gani tunaweza kuiamini na kupeleka mchango wetu huko, naamini tukiulizana miongoni mwetu tutapata majibu tunayoyahitaji.Tupeane habari, tubadilishane uzoefu.

Mwishoni baadhi yenu mliomba kuona kama ninazo picha zingine za shule hiyo ya Kibogwa.Picha inayoambatana na ujumbe huu ni Shule ya Msingi Kibogwa kwa nje.Double click kwenye picha uione vizuri.Picha na Mathew Membe na nimeipata kupitia kwa Yahya Charahani, mwanablog, mwandishi wa habari aliyeko Tanzania.

Tuesday, April 24, 2007

UNAONA NINI KATIKA PICHA HII?


Pichani ni watoto-wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibogwa iliyopo katika tarafa ya Matombo mkoani Morogoro.Itazame kwa makini picha hii, double click juu kwenye picha yenyewe ili uione vizuri zaidi. Huu ni mfano mmoja kati ya mingi sana nchini mwetu. Hivi ndivyo tunavyoiandaa Tanzania ya leo. Ewe raisi wa nchi,ewe waziri, ewe kiongozi,ewe mwananchi mwenzangu,unajisikiaje kuona hali kama hii? Nini thamani ya uongozi wako?Nini thamani ya ubinadamu wako?

Picha imepigwa na Mathew Kwembe na nimeipata kupitia kwa Yahya Charahani.

Monday, April 23, 2007

UMESHAWAHI KUUMWA NJAA?:MSAIDIE ANAYEKUFA NA NJAA!


Jaribu kukumbuka siku ambayo ulishikwa na njaa isiyo ya kawaida na hukuwa na hata maji ya kunywa kupoza kiu. Jaribu pia kufikiria ni mateso ya kiasi gani kukosa chakula mpaka ukakata roho kwa njaa.Kila mwaka mamilioni ya watu duniani wanafariki kwa njaa pamoja na kwamba juhudi mbalimbali za kimataifa zinafanyika ili kunusuru hali hii.

Zaidi ya watu 24,000 duniani wanafariki kila siku kwa njaa. Robo tatu ya watu hao ni watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.Nchi kama yetu ya Tanzania kwa mfano, ni mojawapo ya nchi ambazo raia wake, hususani wanawake na watoto, wanafariki kwa magonjwa mbalimbali yanayotokana na ukosefu wa chakula na njaa kwa ujumla.

Sasa kwa kuzingatia nguvu ya mtandao, mwaka 1999 tovuti iliyopewa jina la “Tovuti ya Njaa” ilianzishwa ambapo kila unapoitembelea tovuti hiyo na kubonyeza kitufe kinachoonyesha “bonyeza hapa” sahani au kikombe cha chakula huchangiwa na mashirika wadhamini ili kumlisha mtu mwenye njaa mahali fulani duniani (sio lazima iwe Tanzania) Kwa hiyo unachotakiwa kufanya ni kujitahidi kuitembelea tovuti hiyo kila siku na kubonyeza mahali palipoandikwa Help Feed The Hungry .Inawezekanaje?

Ni hivi, mashirika ambayo ndio wadhamini wakubwa wa kuwepo kwa tovuti kama hii wanaweka matangazo ya biashara zao (naamini unajua kwamba matangazo ya kwenye mtandao ni biashara ya mabilioni ya dola) na kubakia na imani (sio imani bure hii) kwamba umeyaona matangazo yao na huenda ukanunua au kutumia bidhaa au huduma wanazozitoa. Ni rahisi namna hiyo kumsaidia mwenzako mwenye nja!Kwanini wasitoe basi fedha au chakula hicho bure kama wanajali? Swali zuri lakini kumbuka ubepari haujali utu wa mwanadamu bali faida.

Katika miaka mitano ya mwanzo tangu kuanzishwa kwa tovuti ya njaa, watembeleaji (surfers) wanaokadiriwa kufikia milioni 200 waliweza kuchangia zaidi ya sahani milioni 300 za chakula. Jamaa wengine wajulikanao kama Mercy Corps nao ni wazuri kuwatembelea na kuona jinsi gani wanapambana katika kuitokomeza njaa.Usisahau kumwambia pia rafiki,ndugu na jamaa yako afanye hivyo hivyo pia.

Picha na Cedric Kalonji.

Friday, April 20, 2007

923 MILIONI WANAISHI KWENYE SLUMS,NINI MCHANGO WAKO?


Zaidi ya watu milioni 923 duniani wanaishi katika maeneo ambayo kwa kiingereza yanajulikana kama “slums”.Tafsiri rahisi ya neno slum ni makazi ya binadamu yasiyo na huduma muhimu za kijamii kama maji, vyoo, ulinzi na huduma nyingi nyinginezo za kiserikali na kijamii.Unaweza kujiuliza, kwa tafsiri kama hiyo hapo juu ni maeneo mangapi basi, kwa mfano nchini kwetu Tanzania ni slums?

Eneo liitwalo Kibera nchini Kenya, nje kidogo tu ya jiji la Nairobi ndilo linasemekana kuwa ni slum kubwa kushinda zote duniani.Karibuni watu robo tatu ya milioni wanaishi Kibera. Kule India eneo lijulikanalo kama Dhavari, pembezoni mwa jiji la Mumbai (zamani Bombay) na eneo liitwalo Orangi, pembezoni mwa jiji la Karachi nchini Pakistani yanafuatia kwa ukubwa wa slums kubwa zaidi duniani.Magharibi mwa Afrika,nchini Ghana, katika jiji liitwalo Tema kuna slums zijulikanazo kama Ashaiman.Ukubwa wa slums hizi inasemekana ni ukubwa wa jiji kabisa- slum city.Jijini Dar-es-salaam maeneo mengi ya nje ya jiji yanazidi kugeuka kuwa slums hususani tukizingatia ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kama hizo nilizozitaja hapo juu.

Sababu kubwa ya kuwepo na kuongezeka kwa slums duniani ni umasikini jambo ambalo linachangiwa moja kwa moja na sera mbovu za kiserikali katika masuala ya uchumi, utandawazi ambao nchi zetu kwa mfano zinazidi kuukumbatia bila kufanya utafiti wa kina, sera za ubepari mamboleo zinazotungwa na mashirika kama IMF na wenzake nk. Ubinafsishaji wa mashirika ya umma kwa mfano ni sababu kubwa ya kuongezeka kwa ukosefu wa ajira= umasikini= kuishi kwenye slums. Kwa ufupi watu wengi wanavutwa kukimbilia mijini kwa sababu ya ukosefu wa huduma za jamii vijijini, ukosefu wa ajira nk jambo ambalo wanakutana nalo tena wanapofika mijini.Wakifika huko mijini wanakutana na mipango hovyo na sera mbovu zinazohusu makazi ya binadamu.

Yapo mambo kadha wa kadha ambayo sisi kama wananchi tunaweza kufanya ili kuhakikisha kwamba makadirio ya kwamba kama hatua za dhati zisipochukuliwa,ndani ya miaka 30 ijayo, takribani watu bilioni mbili watakuwa wanaishi katika slums, yanapunguzwa kama sio kusahaulika.Inawezekana kabisa nikawa mimi au wewe, ndugu na jamaa zetu,watoto wetu na hata wajukuu wetu. La kwanza ni kumuuliza mbunge wako juu ya mipango halisi ya serikali katika kutokomeza umasikini na kama wanayo mipango endelevu ya kuhakikisha kwamba idadi ya watu inaendana na huduma za jamii.Usingoje mpaka wakati wa uchaguzi kuhoji mambo haya.Pili ni kuunga mkono shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali kama lile la Shack/Slum Dwellers International (SDI). Tawi lao nchini Tanzania ni hili hapa.Mashirika kama UN Habitat ambalo linaongozwa na mtanzania mwenzetu, Prof.Anna Tibaijuka, nayo yanamipango fulani fulani mizuri ya makazi ya binadamu.

Pichani juu ni makazi ya binadamu jijini Dar-es-salaam, eneo lijulikanalo kama Magomeni Kota.Picha kwa hisani ya Maggid Mjengwa.



Sunday, April 15, 2007

USHINDANI NI MKUBWA,TUJIZATITI



Wiki kadhaa zilizopita rafiki yangu Metty wa Metty'z Reflections-Tanzania in Focus (Metty yeye hublog kwa kiingereza zaidi) aliandika waraka mfupi lakini mzito na akaupa kichwa cha habari Brand Tanzania:Please Do More. Alichokuwa akikiongelea Metty ni ulazima wa wizara na idara zetu zinazohusika na masuala ya utalii kufanya zaidi katika kuhakikisha kwamba utalii unazidi kustawi ili kuliongezea taifa pato la kigeni,ajira kwa wananchi wake nk.Niliupenda waraka wa Metty kwa sababu kimsingi ulijaa ukweli.

S
iku chache zilizopita nilipotembelea miji ya kusini mwa Marekani,hususani Tampa Bay,Florida nilikumbuka sana alichokiandika Metty.Miji mingi ya kusini mwa Marekani inalelewa na biashara ya utalii.Serikali za miji ile inajua thamani ya utalii na hivyo huhakikisha kwamba ukitembelea mara moja utatamani kurudi tena na tena. Nilipotembelea Busch
Gardens-Africa
(tafadhali tembelea hii tovuti yao ili uelewe zaidi ninachokiongelea), na kwa kuzingatia kwamba sijapata fursa ya kuziona mbuga halisi za wanyama kwa miaka kadhaa sasa,nilijihisi nimerudi nyumbani. Kuanzia vibanda vya wamasai, landrover za mbugani kama hiyo hapo pichani,(zilikuwepo landrover zenye plate number TZ NYANI,FISI,TEMBO nk) treni linalokatiza mbugani, mito,mabonde,majani kibichi nk ni vitu ambavyo vitakukumbusha mbali.Ukiingia humo ndani utaona karibuni kila aina ya mnyama unayemjua.Kwa ufupi zile mbuga zetu maarufu za Afrika Mashariki zote zimewekwa pale.Ukiona mto Congo waliotengeneza hawa jamaa utashikwa na butwaa.

I
ngawa kuna tofauti kubwa kati ya kuona kundi kubwa la twiga au wanyama wengine kule Manyara au Tsavo nk, kwa wenzetu wengi wa magharibi hii ni tosha kabisa.Pasipokuwa na kampeni imara za kutangaza utalii wetu ni wazi kabisa kwamba wengi wa watu hawa ambao tulitegemea ndio wawe watalii wa kesho na keshokutwa tutakuwa tumewakosa.Atakuwa na sababu gani ya kutembelea mbuga zetu endapo anaweza kuwaona wanyama hao nchini kwake au nchi jirani na kwake? Hapo hatujaangalia adha zingine kama malaria, ukosefu wa umeme, na sasa tishio la rift valley nk.Ni lazima wizara zetu zitambue kwamba zinakabiliwa na ushindani wa aina yake na wa hali ya juu sana.Ni muhimu tukajifunza kuzinadi nchi zetu,utalii wetu kuendana na karne hii mpya ya utandawazi. Kazi ipo mbele yetu.

Friday, April 13, 2007

IJUMAA YA TAREHE 13!


Leo kuna watu hawatoki majumbani kwao,hawayagusi magari yao,hawatizami luninga zao,hawali samaki wenye mifupa,hawatoki hata kitandani.Kisa? Leo ni Ijumaa yenye kubebwa na tarehe 13,tarehe ambayo imani za (sijui niziite za kishirikina?) zinatabiri kwamba leo ni siku mbaya kabisa.Ukitoka utapata ajali,jambo baya sana litakutokea aidha wewe au wanajamii wako.

Imani hii imesambaa zaidi kwa jamii za waingereza,wajerumani na wareno.Wagiriki na wahispania wao wanaiogopa zaidi Jumanne yenye tarehe 13.Siku hii ya ijumaa 13 inabebeshwa lawama kutokana na mambo kadha wa kadha ya kihistoria.Wanaoigopa siku hii wanasema mgeni wa kumi na tatu,Yuda Iskariote, ndiye alipelekea kufa kwa Yesu, siku ya ijumaa. Wanasema yule mama yetu wa kwanza yaani Eva alimpa Adam "tunda" siku ya ijumaa.Wanasema Abel(mtoto wa kwanza wa Adam na Eva) aliuawa na kama yake Kain siku ya Ijumaa(hivi ushawahi kujiuliza kama watoto wa binadamu wa kwanza wote walikuwa wa kiume,dunia iliongezekaje baada ya hapo?)

Wachumi wanatabiri kwamba takribani dola za kimarekani milioni 900 huota mbawa kwenye ulimwengu wa biashara siku ya leo kwa sababu ya hofu ya siku hii kwa sababu watumiaji,wanunuzi wa bidhaa na huduma leo hawatoki majumbani mwao nk.

Sasa hizi ni imani za kizungu.Sisi waafrika tunazo zetu,unazikumbuka zipi?Mimi nazikumbuka kadhaa, ukikojoa vichakani unaambiwa titi la mama yako litakatika, ukiona mvua inanyesha huku jua linawaka unaambiwa ujue simba anazaa.Ukimruka mtu lazima umruke tena ama la atakuwa mfupi.Ukimcheka mkweo utaota kisenene kwenye jicho.Hapo sijataja zile imani kwamba fulani akioa kutoka ukoo fulani au kabila fulani basi mambo yatakuwa vinginevyo.Unazikumbuka zipi?Unadhani imani hizi zina ukweli ndani yake au ni ushirikina na hofu zetu kama wanadamu tu?Ijumaa 13 njema!

Wednesday, April 04, 2007

KUMBUKUMBU YA VITA



M
wanadamu amefanikiwa katika mengi.Ameweza hata kumpeleka mtu mwezini.Ameweza kuifanya dunia kuzidi kuonekana kama kijiji.Lakini mwanadamu ameshindwa vibaya katika kuipata amani.Vita vimetuzunguka kila kona.Mwanadamu haoni haya kushindwa kuipata amani.Ni kwanini?

Pichani ni mnara wa kumbukumbu ya vita ya kwanza ya dunia uliopo jijini Ottawa,makao makuu ya serikali ya Canada.Kwa bahati mbaya minara hii haijatukumbusha uchungu wa vita ili kuamsha ari ya kupatikana kwa amani bali imetufanya tuwe wapenzi wa vita na mauti zaidi.

Angalau leo hii raisi wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad ametoa msamaha kwa waingereza waliokuwa wamekamatwa katika maji ya Iran.Hivi ingekuwa wa-Iran ndio wamekamatwa huko Uingereza au Marekani unadhani ingekuwaje?