VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Friday, August 12, 2005
Tusipojipenda sisi, nani atatupenda?
Waraka Julai 24

Mtanzania mwenzangu,

Najua heka heka za uchaguzi zimerudi - safari hii kwa kishindo zaidi, kwani kinachofuata ni kampeni za nguvu, huku kila mmoja akijaribu bahati yake ya kupaita ikulu nyumbani kwake kwa miaka mitano ijayo.

Bahati mbaya, leo sitaki kuandika habari za siasa. Unajua, wakati mwingine siasa zinakera. Si ndiyo jamani? Siasa si zimejaa uongo? Kwani siri? Basi, leo tuachane nazo kidogo.

Mojawapo ya matukio ya kufurahisha sana, hususani wakati huu wa majira ya joto hapa Toronto, katika jamii ya Waafrika, ni tamasha linaloitwa AfroFest. Tamasha hili hufanyika kila mwaka. Wiki iliyopita lilifanyika kwa mwaka katika bustani za Malikia Jijini Toronto (Queens).

Nia ya tamasha hilo ni kutukuza na kukuza muziki wa kutoka Afrika. Hivyo, kila mwaka, wanamuziki mbalimbali wenye majina na mafanikio ya kimuziki barani Afrika hualikwa ili waje kutumbuiza katika shamrashamra hizo ambazo hudumu kwa siku mbili. Nasikia Remmy Ongara aliwahi kualikwa na kutumbuiza.

Mwaka huu, aliyealikwa ni Oliver Mutukudzi kutoka Zimbabwe. Alitoa
burudani iliyokonga nyoyo za kila mtu aliyehudhuria. Wazimbabwe waliokuwapo walijawa na furaha isiyo kifani.

Tamasha hili haliishii kwenye muziki tu. Linakuwa na vibanda mbalimbali vya wauzaji wa nguo, vinyago, mapambo na vitu kadha wa kadha kutoka Afrika. Wakenya wametokea kuchangamkia sana biashara hii. Na niliona vitu vingi wanavyoviuza pale, vinatoka Tanzania. Lakini kwa ujanja wao, wanasema vinatoka Kenya. Sisi tumezubaa, tunapigwa bao.

Vyakula mbalimbali vya Kiafrika vinakuwapo tele. Nakumbuka yupo rafiki yangu aliyewahi kuniuliza: “Hivi huko Kanada mnakula vyakula gani?”

Wapo wanaodhani kwamba huku ni mwendo wa kuku na burger tu. Hapana! Ukweli ni kwamba hapa Kanada kuna kila aina ya vyakula. Ushahidi unaupata unapotembelea viwanja kama hivi.

Kuna bamia, mlenda, maharage, mishikaki, nyanya chungu, ugali, wali wa nazi, matembele na kila aina ya chakula. Mishikaki na nyama choma pia vipo kwa wingi. Hata mimi bado nashangaa kwa sababu sijajua vyakula hivi vinapatikana wapi. Lakini ukweli ni kwamba ladha ya vyakula vya hapa si kama vya hapo nyumbani.

Nyumbani kuzuri bwana. Ninachojua ni kwamba Wachina ndio wanaongoza kwa kuuza vyakula vyenye kupendwa sana na Waafrika.

Tofauti ya wazi inaonekana katika matumizi ya pombe. Huku, pombe haiuzwi kiholela. Zipo sehemu maalumu zilizotengwa kwa ajili ya biashara hiyo. an ili uingie humo sharti uwe na umri wa miaka 18 na kuendelea.

Walinzi wakihisi kwamba wewe bado mdogo, watakulazimisha utoe kitambulisho kuthibitisha vinginevyo.

Jambo moja ambalo lilinisikitisha na kunifurahisha. Ni jinsi ambavyo lugha ya Kiswahili inazidi kupanda thamani duniani. Nilifurahishwa kuona maandishi mengi yaliyokuwapo katika bustani hizo yameandikwa kwa Kiswahili. Kilichonisikitisha ni kuona kwamba Kiswahili kinapewa kipaumbele na Wakenya, Wanyarwanda, Warundi na Wakongo.

Watanzania hawamo. Kila sehemu nilipoona maandishi ya Kiswahili nilitabasamu nikidhani nimeona Mtanzania mwenzangu. Wapi! Kila mara nilijikuta mtu-baki. Kichwa kiliniuma pale nilipokwenda kununua bendera ya Tanzania. Nikaambiwa zimeisha. Nani aliziuza?

Ajabu, nikawa kila nikiangalia uwanja mzima naona bendera za mataifa mengine zinapepea - ya Tanzania haipo. Nikauliza, ‘nani ananunua bendera za Tanzania wakati sizioni zikipepea?’ Nikaenda kwa muuza bendera mwingine. Akaniambia ameuza ya mwisho kama dakika mbili tu zilizopita. Basi nikahisi kwamba wapo Watanzania wengi hapa uwanjani lakini hawajivunii nchi yao.

Kwa sababu kama tunajivunia nchi yetu, inakuwaje ununue bendera na kuitia mfukoni wakati wenzetu wote wanapeperusha bendera zao? Ilinibidi nitoke uwanjani na kuingia mjini kidogo ili kupata bendera ya Tanzania. Nikaipata na kurudi nayo pale uwanjani.

Nikawa naipeperusha kila kona ninayokwenda. Nikikutana na Watanzania, wanatabasamu na kunisalimia “Mambo vipi?” Lafudhi yao inanijulisha kwamba ni Watanzania wenzangu; maana Kiswahili cha Tanzania ni tofauti na cha sehemu nyingine. Ajabu ni kwamba watu wenyewe wanasalimia huku wakipita kwa kasi kabisa. Huwaoni tena!

Matukio kama haya yanaibua maswali mengi sana kichwani kwangu.Je ni kweli kwamba sisi Watanzania hatuipendi nchi yetu kwa kiasi hiki? Ni kweli kwamba kuna Watanzania wengi tu ambao wanatamani wasingekuwa raia wa Tanzania? Kama sivyo basi tatizo letu ni nini basi?

Hatuipendi nchi yetu kwa sababu ni masikini sana au vipi? Tunajivunia kweli lugha ya Kiswahili kama ambavyo wengi wanadhani? Au tunatamani kwamba hata tusingekuwa tunaizungumza? Au ndiyo maana wengi tukikaa huku ughaibuni tukirudi nyumbani tunajifanya hatukumbuki tena lugha yetu?

Zamani nilidhani kwamba sisi Watanzania ni masikini jeuri. Nilidhani Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alifanikiwa kutupa kitu cha kujivunia. Ninaloliona sasa ni tofauti. Wangapi leo hapo nyumbani na huku ughaibuni wanajivunia mila na tamaduni zetu, iwe mavazi, lugha na vyakula?

Si kwamba mambo yetu tunayaona ni ya kishamba? Tunataka kufanana na wazungu kwa udi na uvumba. Tunashindwa kujivunia uraia wetu, hata tukiwa na Waafrika wenzetu? Au ndiyo maana tunawathamini zaidi jirani zetu? Wakenya na Waganda wangapi hivi leo wanapata kazi za maana sana hapo Tanzania kwa sababu tu ni Wakenya na Waganda?

Lazima tubadilike. Tukiwa nje au ndani ya nchi yetu; kama tunataka Tanzania iendelee lazima tuipende na kujivunia utaifa wetu. Najua wengi tunakatishwa tamaa na viongozi wetu ambao ndio viongozi wa kutoithamini lugha yao; na nchi yao.

Mbona wakipata homa wanakimbilia kutibiwa nje, wakati hospitali zipo nyumbani? Mbona mavazi yao, lugha zao hazina mwelekeo wa kujivunia Utanzania wao?

Hiyo ndiyo iwe sababu ya sisi wengine pia kukubali utumwa huo wa kiakili? Maana kama tunawalaumu viongozi kwa hayo, mbona hatujibidishi kuyarekebisha? Tuipende Tanzania yetu. Jumapili njema.

jeffmsangi@sympatico.ca
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 6:01 PM | Permalink |


Maoni: 0


   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker