Jogoo anawika, anawika tena.Namsikia kwa mbali.Mvua inanyesha na usingizi bado umenitawala. Jana nilichelewa sana kulala.Nilikuwa kwenye kikao cha harusi cha mfanyakazi mwenzetu. Ameamua kufunga pingu za maisha.Ama kweli dunia hadaa ulimwengu shujaa, hakuna mtu alikuwa anapinga kuoa kama huyu bwana. Leo hii kakata shauri, anadai hakuna mafanikio katika mwanaume yoyote bila mwanamke! Hatuna budi kumuunga mkono.Michango inahitajika.
Nafumbua macho na kuangalia saa yangu, kumekucha na nikifanya mchezo nitachelewa kibaruani. Nimehamia nyumba hii siku si nyingi. Nimeanza juzi tu maisha ya kujitegemea baada ya miaka mingi ya kuishi na wazazi wangu pale Sinza-Makaburini. Nimehamia Kimara-Baruti.Nimepanga chumba kimoja-self contained.
Nakaa kitandani na kuwaza, utumwa huu utaisha lini? Hivi ni lazima niende kazini kila siku ndio niweze kuishi? Na kazi hii namfanyia nani kama sio yule yule mkoloni aliyetesa babu zangu? Hivi kizazi changu kimemkosea nini mwenyezi mungu? Utumwa uliisha kweli?
Nimesimama kwenye kituo cha daladala.Mkononi nimeshikilia shilingi mia na hamsini zangu,ndio nauli hiyo.Naogopa isije ikaniponyoka.Kugombana na kondakta wa daladala yataka moyo.Nimeketi dirishani,nawaza siku itakavyokwenda. Natazama abiria wenzangu, naona wote wamenuna.Ninatabasamu, huenda siko peke yangu mwenye kuonja makali ya maisha.Mbona hatuungani basi tukajikomboa kwa pamoja? Umoja sio nguvu tena?
Kutokea dirishani naona mengi.Naona picha za wagombea ubunge na uraisi zimetanda kila kona.Zina rangi za kila namna.Karibuni kila picha mgombea anatabasamu.Anacheka nini huyu?Au anatucheka sisi kwa ujinga wetu? Tutamchagua hata kama tunajua anatoa na kupokea rushwa kwa kwenda mbele.Tutamchagua kwa sababu tumeshakula pilau lake,hatuna jinsi.Anatudai kura yake.
Pembeni namuona jamaa anajisaidia haja ndogo.Hivi ustaarabu huu unatoka wapi?Au tuitupie lawama serikali kwa kutokuwa na vyoo vya kutosha mitaani? Ama! Namuona kibaka anamwibia dada mmoja mkufu wake.Asubuhi yote hii jamani.Dada anapiga makelele lakini hakuna anayemsaidia.Hasira zinanishika,natamani nishuke nikamsaidie huyu dada. Nikishuka nauli nyingine nitapata wapi? Sina jinsi.Kondakta ananipigia filimbi yake ya sarafu kiganjani.Usilale mkuu,kumekucha!
Nyuma yangu jamaa wawili wameanzisha mjadala wa kisiasa.Kila mmoja ana lake la kusema wakati huu.Nakumbuka jioni mtaani kwetu kuna mkutano wa kampeni.Itabidi niwahi kurudi nyumbani.Nasikia jamaa atagawa tisheti za bure.Nataka pia kumuuliza swali fulani.Sijui swali gani kwa sasa.Ninayo mengi.
Tunakata kona ya maktaba.Tayari tupo katikati ya jiji.Wauza magazeti wametapakaa kila sehemu.Wametoka kuchukua magazeti tayari kuyatembeza na kuuza.Siku hizi sinunui magazeti,yamejaa uongo na umbeya.Sijui unatusaidia nini. Kituo kikuu cha mabasi Posta mpya,tayari tumefika
Nanunua vitumbua kutoka kwa mama mchuuzi.Nimekumbuka sijapata kifungua kinywa.Sina mke na ukapera hauniruhusu kujitengenezea chai bado. Tutaendelea baadaye.
Kaka hapa umenipeleka nyumbani. Ndio maisha ya kila siku. Hilo la kupora mkufu linahitaji makala nzima. Dar unaporwa halafu kila mtu anaangalia tuu. Ukiweza kupiga kelele jamaa akikamatwa anaweza akachomwa moto. Kazi ipo. Umenifurahisha sana kwa kila mgombea kutabasamu kwenye picha ya kampeni. Inafurahisha sana. Kila mmoja anaonyesha tabasamu.Tabasamu ya nini kwenye kampeni tuu?