VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Wednesday, October 12, 2005
NIMEITWA KWENYE USAILI
Nimesimama mitaa ya posta,hapa ndipo inasemekana ni katikati ya jiji.Zamani niliwahi kuambiwa kwamba pale kwenye mnara wa askari ndio katikati ya jiji lakini naona siku hizi mambo yamebadilika.Vijana wa kisasa wanapaita Zero Brain hapa posta mpya.Huwa wanakutana hapa nyakati za jioni.Wote wamesuka nywele,si wavulana si wasichana.Kizazi cha .com hiki.

Kijua cha saa tano asubuhi kuelekea saa sita mchana kimepamba moto.Kijasho chembamba kinanitoka.Pembeni kuna jamaa anauza anjifu. Natamani kununua moja ila kwa bahati mbaya mfuko umetoboka.Nina nauli yangu tu ya kunirudisha nyumbani.Nauli kanikopesha mchaga mmoja mwenye kiduka pale mtaani kwetu. Kila siku ananiambia ingawa yeye hajasoma sana anathamini sana wasomi.Ananitakia kila la kheri katika kutafuta kwangu kazi. Ila hajanipa nauli hii bure,kanikopesha.Usicheze na wachaga kunako pesa.Wote wanazaliwa na shahada za uchumi hawa.

Tangu nimemaliza chuo kikuu leo ndio kwa mara ya kwanza nimeitwa kwa ajili ya usaili au interview.Nimeshawakilisha maombi ya kazi kwenye kampuni zaidi ya hamsini na asasi za serikali zaidi ya thelathini.Mengi ya maombi hayajajibiwa na yaliyojibiwa naambiwa sina uzoefu.Niupate wapi uzoefu bila kupewa kazi basi?Natamani niingie kwenye ofisi yenye kiyoyozi kidogo ili kupunguza jasho.Najaribu kupiga hesabu ni ofisi gani ya rafiki yangu yeyote iliyopo karibu.Oooh nimekumbuka,rafiki yangu Mtoi anafanya kazi wizara ya mambo ya ndani,ipo karibu na niliposimama.Taratibu naanza kuikaribia wizara.Loh,nje kuna foleni ile mbaya,watu wanaenda kuomba passport.Duh hii si ni haki ya kila mtanzania?Inakuwaje anaanikwa kwenye jua kali namna hii ili kupata haki yake?Nakata tamaa,kijasho kinazidi kunitoka.Mtoi siwezi kumuona kwa mwendo huu.Ofisi yake inatisha,haina mazingira yanayotia amani kwa mwananchi wa kawaida kama mimi.Naweza kamatwa kwa kosa la kusingiziwa bure.

Basi naamua kujificha kwenye kivuli cha muuza machungwa pale pale nje ya wizara.Navuta pumzi na kuvuta muda kabla ya usaili,Posta House gorofa ya nne.Pembeni yangu namuona askari anachukua hela kutoka kwa jamaa.Nasikia wanazungumza kwa sauti za chini.Askari anasema hazitoshi.Kazi anayotakiwa kufanikisha ni ngumu na inaweza hatarisha kibarua chake.Jamaa anamuahidi kuongeza kitu kidogo akikamilisha kazi.Askari anatabasamu na kumuita jamaa mkurugenzi...ah mimi nilijua mkurugenzi wangu huwezi kuniacha nife njaa' Ghafla jamaa kapata cheo cha ukurugenzi,cheo kikubwa kuliko vyote kwenye ulimwengu wa rushwa. Rushwa inafanyika mbele ya wizara ya mambo ya ndani,mbele ya makao makuu ya jeshi la polisi! Napiga miayo,sijala kitu tangu jioni ya jana nilipodoea futari pale msikitini Magomeni Mwembechai.Kila mwaka mwezi kama huu jina langu naitwa Hamza.Usiulize sana kwanini.
Nabisha hodi mlangoni kwa katibu muhtasi wa kampuni hii ya madini.Kampuni ya kigeni hii,ndio hawa wanaoitwa wawekezaji.Kama wewe unawaita wanyanyasaji shauri yako.Katibu muhtasi huyu anavutia ile mbaya.Mavazi aliyovaa hayaendani na ofisi hii.Nashindwa kumtofautisha na yule dada wa kwenye kamari.Nazungumzia Casino iliyopo katikati ya jiji. Najichekesha kidogo,kimsingi sina cha kuchekelea.Nicheke nini na sijapata kazi mwaka wa pili sasa tangu nimalize chuo?Nanyanyasika bila kupenda.Shuleni elimu niliyopewa imeniandaa kuajiriwa tu.Shuleni hamna practical tena,serikali ilishaziondoa siku nyingi.Kisa,eti pesa hamna.
Binti ananiambia nisubiri kidogo.Usingizi unanijia taratibu,kiyoyozi kinafanya kazi yake.Njaa pia inachangia isitoshe jana sikulala vizuri.Wezi walivamia kwa jirani yetu.Ilibidi tutoke kupambana na wezi.Polisi wakaja masaa manne baada ya wezi kuondoka.Tulikosea tulipopiga simu na kuwaambia kwamba wezi wana silaha. Huwa hawaji haraka ukiwaambia hivyo.Waoga kuliko kunguru.
Usaili umeanza,jamaa anaongea kizungu cha wapi sijui.Nasikia neno moja moja tu.Hamna mkalimani karibu.Ama kweli nimepatikana.Ananiuliza kuhusu ujuzi nilionao.Namwambia mimi ni bingwa wa geographia. Ananiambia huo sio ujuzi,anataka kujua kuhusu ujuzi nilionao,sina jibu,hasira zinampanda.Kwanini?Sielewi hata mimi.
Ananiambia kwamba anaweza kunipa kazi ya udereva kama najua kuendesha gari.Anasema kwa nguvu kidogo,can you drive a car????Jamani yaani mimi injinia mzima nikaanze kazi ya udereva?Mambo gani haya?Kudharauliwa gani huku?Nchini kwangu kabisaaa?Nafikiria nimtwange ngumi ya uso lakini kwa mbali naona walinzi wa ile kampuni ya group4.Watanirukia kama hawana akili nzuri,wakinishindwa watawaita wale wala rushwa.Nitafanya nini wakati senti tano sina? Segerea sitaki kwenda.Nasikia wanaume kwa wanaume wanafanya michezo mibaya.
Kimya natoka,sikumbuki hata kuaga.Mapambano yanaendelea,kazi bado naitafuta.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:06 PM | Permalink |


Maoni: 5


  • Tarehe: 4:09:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Indya Nkya

    Mchaga safi sana huyo. Alielewa siasa ya ujamaa na kujitegemea isitoshe asingeweza kumpa mpare bure labda amnunulie Denge. Rushwa mbele ya makao makuu ya jeshi la polisi! Ndiyo mara nyingine hata chenji unarudishiwa kabisa. Kama umetoa elfu kumi na mmekubaliana elfu tatu atakupa chenji ya elfu saba!

     
  • Tarehe: 4:49:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Uaridi

    My dear Jeff: Ashamed to say that it will take me three years to translate what you have written. But keep on blogging - we need more Swahili writers on the web.

     
  • Tarehe: 2:22:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger mloyi

    wanasema wamezoea, lakini siku akifa mjomba wao anayewanunulia chakula sababu atakuwa anaumwa, hawezi kufanya kazi, na hana pesa akiwategemea wao wasio na kazi, kama wewe,ambao hawawezi kutoa rushwa kwa daktari ili watibiwe kwenye hospitali ya serikali... hata chenji ya rushwa ambayo hawakutoa wataikataa kwa hasira -- unajua ukimpa konda mia mbili akakurudishia mia nane utashuka kituo kinachofuata hata kama hujafika uendako--- . Unajua wataondokaje?.... sio kimya kimya kama mchungaji akidai watu waongeze sadaka, au wakijua wameliwa kwenye kamari...labda ndesanjo anajua, muulize.

     
  • Tarehe: 1:30:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Ndesanjo Macha

    Neno "anjifu" limenivunja mbavu na kunikumbusha nyumbani. Pole kwa kutolala mkipambana na wevi, kumbe askari wakisikia askari wana silaha hawathubutu kuleta pua.

    Mloyi naye kanimaliza anaposema ukimpa kondakta mia mbili akakurudishia mia nne unashuka kituo kinachofuata hata kama hujafika unakokwenda. Ndio dalili za ufukara unaokabili wengi. Siku hizi mtu akiangusha mkoba wa fedha, mtu anatazama huku na kule kama kuna wanayemtazama, anaunyanyua na kuutia kibindoni kama ni mkoba wake.

     
  • Tarehe: 7:56:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger FOSEWERD Initiatives

    Jeffy, kila mara nikisoma makala zako ninagundua kuwa wewe ni mtaalamu wa fasihi na inawezekana wewe na bwana Tx moshi william ni mapacha! una uwezo wa kumjengea mtu mazingira fulani ya kwa hisia. niliposoma makala hii nikajiona niko pale dar kwenye kugaragazana halafu nikalisikia jua linavyowaka na joto linavyochoma japo huku kiangazi bado! halafu nikahangaika sana kuona jinsi ninavyoteseka kupata kazi wachilia mbali kulipa mkopo wa nauli toka kwa bwana muuza duka! nilisikitika sana pale nilipoulizwa kuuhusu kuendesha gari wakati kama mzee wangu angekuwa mmoja wa wateule wahishimiwa sana, pengine ningekuwa ninajua kuendesha (kwani gari si mpaka muwe nalo kwenu?) au la kazi ningalipatiwa kwenye waya (simu).


    nitamalizia na kipande cha winbo wa TX moshi william...

    nimesimama kwenye kona ya uhuru na msimbaziiii

    natizama wanaopita wanaorudi maaaamaaa!

    huenda nikaiona sura yake tumaaa!

    nikasimama nikiwazaa ahadi yetu tuliyopangaa!!

    tukutane darisalaaama mamamaa tuma maaama!!!

    nia na madhumuni wazazi watuonee!!

    cheers,

    mark

     
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker