Wandugu,
Kuanzia wiki hii nitakuwa naweka hapa kwenye tovuti yangu mashairi ambayo nimekuwa nayaandika mara kwa mara.Nitakuwa nikiweka shairi angalau moja kwa wiki.Nikisahau ruksa kunikumbusha. Ukiniita mshairi sitakataa.Ila naomba ufahamu kwamba mashairi yangu hayana kanuni, naandika nitakavyo, kwa raha zangu,kero zangu,hasira zangu nk.Unaweza pia usinielewe naongelea nini.Hiyo itakuwa ni sehemu ya sanaa ya ushairi. Hili hapa chini nimeliita NIAZIMENI AKILI ZENU.
Udhia huu unatoka wapi na unatokana na nini?
Adhama hii itadumu mpaka lini,au ni ya muda mfupi tu?
Jana tumeadhimisha sikukuu gani au shujaa gani kazaliwa?
Au pengine amechipukia wapi,kaambiwa na nani ukweli?
Kengele ya adhuhuri imepigwa,waungwana waende kujisafi
Maadili yangali yanahitajika, ingawa naona kama yameshatuponyoka
Au yamekuwa adimu na bila maafikiano ya kiungwana
Lakini tusiahirishe mkakati wetu wa ukombozi, tusitende dhambi hiyo kamwe
Noeni visu na kuweka ala zenu mahali pake, hatujui mbeleni kunani
Ambatana na ufananao, lakini usikatae usiofanana nao pia
Tutakuita mbaguzi, tafadhali usikatae tukifanya hivyo
Anga limejaa harufu mbaya, pua zangu zinanusa damu zaidi
Najiapiza kwamba sitaki kuona vita, halafu najiona mbumbumbu
Vipi kama wenzangu wanataka vita, mimi ndio nibaki ndani?
Ardhi hii ni ya nani?
Au mpaka wale waketio Areopago waamua kunikabidhi?
Wanipe na kipande cha karatasi chenye jina langu?
Ishara hizi ni za nini ,wewe unaziamini?
Unataka na mimi niasi? Majuha si watanishangaa?
Nimechanganyikiwa kwa sababu napinga uzungu
Au nisimame madhabahuni kama askofu
Nipayuke kwa nguvu zangu zote
Kisha nisitende hata moja nisemalo, nipunge mkono niende zangu
Hivi hapo awali mambo yalikuwa ya aina gani?
Nataka kujua lakini sioni wa kumuuliza
Wengi wananitazama kwa jicho baya, wananiombea dua mbaya
Nimeazimia kukomboa wengi,nimeanza na kaya yangu kwanza
Naomba mnikopeshe akili kwenye vichwa vyenu nyote
Masikio siihitaji,yanaingiza na kutoa
Nataka kubatilisha kitendawili, hiki kigumu kuliko vyote.
Jeff waweza himili, akili zetu hifadhi?
ReplyDeleteNadhani wataka jina, siri zidi fukiani
Jinalo ukurasani, vema tulishakupani,
Kisha akafika yule TUME, ushindi kakunyimani?
Funuka sasa tazama, hapana kuogopani
Kunywa damu ya kiama, umimi umezidini
Kwa sasa ninainama, Natulia Kasirini
Karibu Malenga Jeff, zindiko tuligangeni.
Ama kweli Hapa si mchezo.
ReplyDeleteZa dhati kwako Boniphace,
ReplyDeleteUlingoni nakaribia.
Ndio Boni, nakuunga mkono:
ReplyDeleteZindiko tuligangeni
Bila alika wageni,
Kalamuyo uinoe
Kwa beti ututuze
Ewe Malenga wetu.
Naye mwana uleleta,
ReplyDeleteMwezi sasa unapita,
Yapaswa achezwe kwata,
Tenzi apaswa kamata,
Ili babaye muenzi.
Naona sasa mnatupa vitu vikali, maana ushairi si utalaam wa kila mtu, lakini mie nashukuru kwa mchango wenu hasa katika kukuza ushairi na lugha ya Kiswahili.
ReplyDeleteMmh! Hapa kakosekana Mwandani tu.
ReplyDeleteUsema ulijualo
ReplyDeleteupendalo lifanyike
masikio yetu tyayatega
malengayo kuyapokea
zetu akili zikonawe
zikusaidie nazako
mashairi kutuingia
kiswahili bado chetu
sirahisi kukiachia
maneno yake matamu
hata kwa asokijua
kukichukua wajaribu
lakini utumwani twakikomboa.