Tuesday, November 08, 2005

NIAZIMENI AKILI ZENU

Wandugu,
Kuanzia wiki hii nitakuwa naweka hapa kwenye tovuti yangu mashairi ambayo nimekuwa nayaandika mara kwa mara.Nitakuwa nikiweka shairi angalau moja kwa wiki.Nikisahau ruksa kunikumbusha. Ukiniita mshairi sitakataa.Ila naomba ufahamu kwamba mashairi yangu hayana kanuni, naandika nitakavyo, kwa raha zangu,kero zangu,hasira zangu nk.Unaweza pia usinielewe naongelea nini.Hiyo itakuwa ni sehemu ya sanaa ya ushairi. Hili hapa chini nimeliita NIAZIMENI AKILI ZENU.

Udhia huu unatoka wapi na unatokana na nini?
Adhama hii itadumu mpaka lini,au ni ya muda mfupi tu?
Jana tumeadhimisha sikukuu gani au shujaa gani kazaliwa?
Au pengine amechipukia wapi,kaambiwa na nani ukweli?

Kengele ya adhuhuri imepigwa,waungwana waende kujisafi
Maadili yangali yanahitajika, ingawa naona kama yameshatuponyoka
Au yamekuwa adimu na bila maafikiano ya kiungwana
Lakini tusiahirishe mkakati wetu wa ukombozi, tusitende dhambi hiyo kamwe
Noeni visu na kuweka ala zenu mahali pake, hatujui mbeleni kunani

Ambatana na ufananao, lakini usikatae usiofanana nao pia
Tutakuita mbaguzi, tafadhali usikatae tukifanya hivyo
Anga limejaa harufu mbaya, pua zangu zinanusa damu zaidi
Najiapiza kwamba sitaki kuona vita, halafu najiona mbumbumbu
Vipi kama wenzangu wanataka vita, mimi ndio nibaki ndani?

Ardhi hii ni ya nani?
Au mpaka wale waketio Areopago waamua kunikabidhi?
Wanipe na kipande cha karatasi chenye jina langu?
Ishara hizi ni za nini ,wewe unaziamini?
Unataka na mimi niasi? Majuha si watanishangaa?
Nimechanganyikiwa kwa sababu napinga uzungu

Au nisimame madhabahuni kama askofu
Nipayuke kwa nguvu zangu zote
Kisha nisitende hata moja nisemalo, nipunge mkono niende zangu
Hivi hapo awali mambo yalikuwa ya aina gani?
Nataka kujua lakini sioni wa kumuuliza
Wengi wananitazama kwa jicho baya, wananiombea dua mbaya

Nimeazimia kukomboa wengi,nimeanza na kaya yangu kwanza
Naomba mnikopeshe akili kwenye vichwa vyenu nyote
Masikio siihitaji,yanaingiza na kutoa
Nataka kubatilisha kitendawili, hiki kigumu kuliko vyote.

8 comments:

  1. Jeff waweza himili, akili zetu hifadhi?
    Nadhani wataka jina, siri zidi fukiani
    Jinalo ukurasani, vema tulishakupani,
    Kisha akafika yule TUME, ushindi kakunyimani?

    Funuka sasa tazama, hapana kuogopani
    Kunywa damu ya kiama, umimi umezidini
    Kwa sasa ninainama, Natulia Kasirini
    Karibu Malenga Jeff, zindiko tuligangeni.

    ReplyDelete
  2. Ama kweli Hapa si mchezo.

    ReplyDelete
  3. Za dhati kwako Boniphace,
    Ulingoni nakaribia.

    ReplyDelete
  4. Ndio Boni, nakuunga mkono:

    Zindiko tuligangeni
    Bila alika wageni,
    Kalamuyo uinoe
    Kwa beti ututuze
    Ewe Malenga wetu.

    ReplyDelete
  5. Naye mwana uleleta,
    Mwezi sasa unapita,
    Yapaswa achezwe kwata,
    Tenzi apaswa kamata,
    Ili babaye muenzi.

    ReplyDelete
  6. Naona sasa mnatupa vitu vikali, maana ushairi si utalaam wa kila mtu, lakini mie nashukuru kwa mchango wenu hasa katika kukuza ushairi na lugha ya Kiswahili.

    ReplyDelete
  7. Anonymous12:43:00 PM

    Mmh! Hapa kakosekana Mwandani tu.

    ReplyDelete
  8. Usema ulijualo
    upendalo lifanyike
    masikio yetu tyayatega
    malengayo kuyapokea
    zetu akili zikonawe
    zikusaidie nazako
    mashairi kutuingia

    kiswahili bado chetu
    sirahisi kukiachia
    maneno yake matamu
    hata kwa asokijua
    kukichukua wajaribu
    lakini utumwani twakikomboa.

    ReplyDelete