
Mambo mawili muhimu sana yanatokea nchini Tanzania mwaka huu.Jambo la kwanza ni hili la uchaguzi mkuu ambao unafanyika wiki ijayo baada ya kuahirishwa kwa muda kufuatia kifo cha mgombea mwenza wa nafasi ya uraisi katika Chadema. Macho na masikio yetu bado yameelekezwa katika uchaguzi huo.Leo sina mengi kuhusu uchaguzi.
Jambo la pili ambalo ndio msingi wa habari hii ni hili zoezi adimu la kubadilisha pasipoti.Kisingizio kinajulikana.Ni amri kutoka kwa wenzetu wa magharibi katika juhudi zao za kupambana na ugaidi duniani.Tunaambiwa kwamba pasipoti zetu za zamani zilikuwa hazisomeki kwa machine kama za nchi nyingine duniani kwa hiyo ilitubidi tuzibadilishe,tupende tusipende.Nathubutu kuiita amri kwa sababu kama isingekuwa amri basi utaratibu mrahisi sana ungetumika kwamba kama una pasipoti ya zamani basi ikiisha muda wake, ukienda kubadilisha unapewa mpya. Na kama hujawahi kuwa na pasipoti kabla ya hapo basi moja kwa moja unapewa mpya. Katika kipindi cha miaka mitano watanzania wote wangekuwa na pasipoti mpya na fedha chungu mbovu zingeokolewa na kupelekwa kwenye miradi ya kimaendeleo. Lakini kwa sababu za kiusalama,sababu za kijasusi dhidi ya ugaidi duniani wafadhili wangekataa.Wangetuelewa endapo tu tungekuwa na viongozi wenye uwezo wa kutetea maslahi ya nchi bila woga.Kwa hivyo basi zoezi hili la kubadilisha pasipoti lingekuwa limetazamwa kwa undani,kitaalamu ili kujua jinsi gani lifanyike.
Badala yake zoezi hili limegeuka kuwa kero ambayo inawafanya wengi(hususani waliopo nje ya nchi na wasio na moyo) kuamua kuukana moja kwa moja uraia wao halali wa Tanzania.Siwalaumu kwa kweli. Hili lina madhara yake.Wachumi na wanajamii wanajua zaidi kuhusu masuala kama hayo.Kero kubwa ni katika utaratibu mzima wa kubadilisha pasi hizo za kusafiria. Mengi yameandikwa kuhusu uzembe, ukiritimba kuhusiana na suala zima la kubadilisha pasipoti.
Nilipokuwa nikisoma habari mbalimbali katika vyombo vya habari kuhusiana na utaratibu mzima wa kubadilisha pasipoti nilidhani ni mapungufu yetu ya kawaida ambayo yanaongeleka.Kimbembe kimekuja nilipojaribu kuyavulia nguo maji ili kubadilisha pasipoti yangu kupitia ubalozi wetu hapa Canada. Labda niseme wazi kwamba ndio kwanza nimeanza zoezi hili la kubadilisha pasipoti. Na mpaka hapa nilipo nimeshakwama.Poleni wenzangu ambao mpo kwenye hali kama yangu.Najua mpo wengi.
Nimeagiza fomu kutoka ubalozini.Nikaambiwa kwamba ni lazima niilipie hiyo fomu $ 20. Kwanza nilishtuka kwa sababu nimeshaanza kuzoea utaratibu wa hapa Canada kwamba hamna hata fomu moja utakayopewa kwa mauzo.Iwe ni ya kuomba uraia,makazi ya kudumu n.k.Unaweza kuletewa hata fomu kumi kwa mkupuo ukitaka.Kwanini uuziwe fomu??Kodi wanazokatwa wananchi zinafanya nini? Nikaona isiwe tabu nikaagiza washirika wangu waliopo huko ulipo ubalozi wetu(Ottawa- mwendo wa kama masaa sita kutoka hapa Toronto kwa gari).
Kichefuchefu kilianza kunipata baada ya kufungua hiyo fomu yenyewe na kugundua kwamba ni fomu sawa sawa kabisa na zile tulizojaza miaka ile wakati tukiomba pasipoti zinazobadilishwa.Sana sana nimeona vifungu vichache sana ambavyo vimebadilishwa.
Wakati naanza kusamehe hayo yote nikagundua kwamba hii fomu imetengenezwa zaidi na inafaa zaidi kwa mtu ambaye bado yupo nyumbani Tanzania.Haijatengenezwa kukidhi haja ya mtanzania aliyeko nje ya nchi. Sababu ni nyingi ila ngoja nijaribu kueleza chache hapa chini.
Fomu imeandikwa kwa kiswahili kitupu bila hata tafsiri ya neno moja la kiingereza. Lazima tukubali kwamba kiswahili chetu bado sio cha kimataifa kiasi cha kutumika ulimwengu mzima. Maelekezo ya jinsi ya kujaza fomu hiyo kwenye tovuti ya ubalozi yote yameandikwa kwa kiingereza! Nadhani hata wao wanakubaliana nami kwamba kiswahili hakina nafasi hapa. Lakini pia nashindwa kuelewa kwamba kwanini tovuti kama hii ya ubalozi haina uhuru wa kuchagua lugha ya kiswahili au kiingereza? Mapungufu mengine haya.Fomu inanitaka nijaze sehemu zinazouliza mtaa/kijiji.Sijui naishi kijiji gani hapa Toronto! Hamna vijiji hapa ninapoishi.
Tayari nipo hapa,fomu inanitaka nijaze madhumuni ya safari na nchi ninazokwenda.Safari gani? Siendi popote kwa hivi sasa
Fomu inanitaka nijaze kazi ninayofanya,kiswahili chake sikijui
Fomu ina kipengele cha shuhuda kwa mwombaji
ambaye anaweza akawa jaji.kabidhi wasii,hakimu.wakili/kamishna wa viapo akiwa yeye mwenyewe ni raia wa Tanzania.Nimtoe wapi mtu kama huyo hapa Canada ndugu zangu? Hata kama nitampata hakimu,jaji nk wa hapa, nani atafanya kazi ya kutafsiri fomu hiyo?
Shuhuda anatakiwa aandike nyuma ya picha kwamba hiyo ni sura yangu.
Pili zimetolewa sampuli za picha pale,sijui wazungu wa wapi wale.Yaani tumeshindwa kabisa kuweka picha za watanzania wenzetu kama sampuli za jinsi gani picha hizo zipigwe?
Maswali magumu yenye majibu haba yananijia.Hivi sisi watanzania tuna nini jamani? Hawa tunaowaita viongozi wa nchi,mawaziri,mabalozi,wabunge ni kina hasa?Wizara za mambo ya ndani na nje wanafanya kazi gani?Kuna jamaa aliwahi kuniambia kwamba Tanzania hatuna mameneja wazuri. Sijui nikubaliane naye au nikatae?
Najua serikali yetu ni bingwa wa kupuuzia mambo.Hili nadhani lisipuuziwe.Ni aibu kwa taifa letu. Lazima serikali ikiri kwamba zoezi hili halikuangaliwa kwa makini.Walioboronga wasihamishiwe wizara zingine bali wajiuzulu au waachishwe kazi kwa nguvu.
Majuzi nimesoma mahali kwamba bidhaa za kutengenezea pasipoti mpya hamna/zimekwisha! Muda wa kusubiri pasipoti mpya ni kama miezi sita hivi. Kwa nchi yenye watu milioni 37 na ambao kati yao asilimia ndogo sana wanatumia pasipoti zao ambayo ni haki yao ya kikatiba. Kwanini utake kujua mtu anakwenda wapi,kufanya nini? Kwanini hilo lisiachiwe balozi husika?Lina uhusiano gani na pasipoti?
Kero ni nyingi sana juu ya suala hili.Wakati umefika,tuseme ukweli.Tuishauri serikali yetu,tuikosoe na isione aibu kukubali kama imekosea. Tuanzie hapa kwenye ulimwengu wa blogu.
Bora umeanza kuogelea katika bahari ya Wafalme Juha wa Tanzania. Una kazi ya kuvuka mto hapo ni bado. Niko bize wiki hii lakini ngekuandikia mengi kuhusu namna nilivyotaabika kupata hicho kijitabu mwaita Pasipoti. Sasa kichefuchefu ni pale nilipokuwa napita kuingia Uwanja wa ndege sehemu ya abiria, kakaja kakijana umri wangu hivi kanauliza dokumenti zangu za kusafiria kuja Marekani! Zinakahusu nini haka utadhani kanafanya kazi ya ukonsula ubalozi wa Marekani? Nikakatazama, kisha nikakajibu kwa kizungu feki, kakanitazama pia. Sasa acha tu nikirudi huku wakati utakuwa ni kuwafanyia vituko mpaka wakome maana wamezidi hawa.