VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Sunday, December 18, 2005
HIVI NYERERE YUKO WAPI?
Asubuhi na mapema,nimesimama nje ya kibanda changu cha nyasi.Usiku wa jana sikulala,kunguni hawakunipa nafasi kabisa.Isitoshe mlo wangu wa jana haukuwa mzuri.Mlo mzuri wa mwisho nilikula juzi kwenye siku ya mwisho ya kampeni kabla ya uchaguzi wa jana.Mgombea wa ubunge aliandaa pilau kwa wanakijiji wote.Mjukuu wangu anayeishi jijini Dar-es-salaam anapenda kuuita mlo huu "pilau ya rushwa".Sijui kama namuelewa au anaweza kueleweka kwa wengi.Mwenye njaa huwa na hasira,na mtu akiwa na hasira hasikii wala haelewi.
Nataka kunawa uso niende zangu shambani.Na njaa hii pamoja na usingizi, sijui kama nitaweza fanya chochote huko shambani. Nagundua sina hata tone la maji nyumbani kwangu ingawa pembeni ya kibanda changu kuna bomba la maji.Nasikia ulikuwa ni mradi wa enzi zile za vijiji vya ujamaa na kujitegemea.Miradi ambayo haikutimia na hivyo maji ya bomba yakabakia kuwa ndoto za senene.Namkumbuka mke wangu. Maisha ya hapa kijijini yalimshinda hivyo akaamua kukimbilia jijini Dar-es-salaam.Nasikia huko anafanya biashara ya kuuza mwili.Sijui mwili anauuza vipi,kwa jumla au kwa dakika chache tu? Masuala haya ya mjini huwa yananiogopesha sana.
Kwa mbali namuona balozi wetu wa nyumba kumi na moja anakuja. Uso umempauka,suruali ina matundu kibao ila alhamdululahi juu kavaa tisheti mpya. Ni hizi tisheti alizotugawia mgombea wetu,zimeandikwa "Chagua CCM,Ari mpya,Kasi mpya....nk".Nimesahau hayo maneno ya mwisho maana kusoma na kuandika sijui.Vijana wa shule ya hapa kijijini ndio waliotuambia maneno hayo. Sijui mwakani watasomea wapi na wao maana tetemeko la juzi liliangusha madarasa yote mawili ya shule.Mwalimu mmoja waliyekuwa naye nasikia na yeye ameamua kuondoka kijijini kwenda kutafuta maisha huko mjini.
Balozi ananiambia kwa sababu mgombea alitupa tisheti na pilau tukala basi tunatakiwa kwenda bomani kusikiliza matokeo ya uchaguzi mchana huu.Sina jinsi,lazima nihudhurie na ikibidi nishangilie kwa nguvu endapo atashinda.Eti najiuliza endapo "atashinda".Kwanini asishinde wakati mgombea mwenzake wa chama gani sijui kile hakuweza hata kuwapa wanakijiji maji ya chupa? Na isitoshe tukasikia kwenye radio kwamba ni mchawi? Nasikia mwenyewe analalamika kwamba hizo ni njama tu za kuhakikisha anashindwa.Namuonea sana huruma lakini sijui nifanye nini kumsaidia.Labda mjukuu wangu akija tena nitamueleza.
Jua linawaka kweli.Tumeketi chini kwenye mavumbi.Tunasubiri watu wa uchaguzi watangaze matokeo.Kama nilivyotabiri, huyu mwenye shati la kijani na suruali nyeusi anatangazwa mshindi.Anaruka juu na kushangilia(kama alikuwa hajui atashinda vile) Kwa sababu tumbo lake ni kubwa basi shati aliyovaa inachomoka kutoka kwenye suruali.Watoto wachache waliokuwa pale wanacheka kuona tumbo la mtu mzima halafu lenye ukubwa kama ule mtungi wa pombe kwa "mama muuza".
Balozi anatuamsha tushangilie! Mawazo yamenitinga,lakini najishtukia nasema ...oyeeee.Walinzi wake wameshamzunguka,hata balozi wetu anakatazwa kumpa mkono.Walinzi wanasema "mheshimiwa" anataka kwenda kupumzika,kesho asubuhi anarudi Dar-es-salaam.
Kwa madaha anaingia kwenye gari lake la kifahari.Anatutimulia vumbi.Anaondoka zake.Kichwani najua hiyo ndio imetoka. Kama tutakuwa hai tutamuona tena baada ya miaka mitano. Pembeni namuona yule mgombea mwingine.Amekusanya watu anawaelezea madhara ya tisheti na pilau.Anaeleza jinsi ambavyo tumenunuliwa na hivyo hatuna haki ya kuuliza kuhusu hospitali,maji,elimu,barabara wala chochote.
Namuona balozi kwa pembeni.Macho yamemtoka,pembeni yake mjukuu wake kasimama.Balozi ananifuata ananiambia mjukuu kaleta habari mbaya.Bibi yake kazidiwa huko nyumbani.Anaomba tukamsaidie kumpeleka kwenye zahanati huko wilayani.Ni mwendo wa masaa saba kutembea.Naona kasahau kwamba ile zahanati ilishafungwa kwa kukosa daktari na vifaa vya kutendea kazi.Naona mtu mzima analia.
Njaa imenishika bado,sijatia kitu tumboni zaidi ya mhogo niliodoea kwa jirani yangu.Nifanye nini?Tufanye nini kubadili hali hii? Namfuata mzee wetu wa kijiji nipate busara zake. Namkuta kajikunja kwenye mkeka wake.Baada ya salamu naanza kumueleza fikra zangu.Ananiuliza, hivi yule "Kambarage Nyerere yuko wapi siku hizi?".Nahisi kizunguzungu.Mjukuu wangu,nitakueleza baadaye.Bado swali la Nyerere linaniletea maruweruwe.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:28 AM | Permalink |


Maoni: 13


 • Tarehe: 12:56:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger Boniphace Makene

  Jeff kama ni mbinu za ghani za kiriwaya hapa nivua miwani. Nakumbuka makala za Freddy Macha, masimulizi. Naomba hii itume Bongo kwenye kibaraza chako cha gazeti lile linalokuwa na wasomajin wengi kwa sasa. Sijui kama litadumu maana uchaguzi ushaisha na hiki ni kipindi cha magazeti kufa Tanzania. Hii ni makala, makala ichomayo moyo, makala itikisayo maini, makala iamshayo fikra, makala itiayo chuki, makala ipasuayo kama radi, makala itemayo sum,u mithili ya bafe, makala ya hayawani!!! Nimetumia neno hayawani hapo, nifahamike kuwa heshima ya hayawani ni kutamka yupasuayo moyo, kutokuogopa kusema na kuweza kupanga visa na kuvipa ridhimu chanya. Hapa umenipata na nina kila sababu pale nifikapo Toronto kuanzia tarehe 28, 12. 05 kukutafuta huko huko ili niweze kuweka mikono yangu kwapani na kusubiri kupakwa mafuta. Nahitaji tohara la motoi, nahitaji tohara litakaloamsha mapambazuko mapya Afrika. Nahitaji tohara litakalohamasiaha haki na maendeleo. Wakati wa kufungua maendeleo ya kiuchumi Tanzania na Afrika ni sasa, unasubiri nini...

   
 • Tarehe: 2:28:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger Ndesanjo Macha

  Umenikumbusha ndugu Ndimara Tegambwage. Huwa ana namna yake ya kuelezea maisha ya vijijini na masahibu yake. Jeff, bila kuficha nimependa sana mtiririko wa kisa hiki. Nimesoma bila wala kuweka nukta. Kifupi lakini umesema mambo mazito kweeeeeli. Inasikitisha lakini ni kweli. Ni kutokana na ukweli huu ndio linakuja swali la: tufanye nini?

  Nakubaliana na Boniphace kuwa tuma kwenye safu yako na pengine urefushe kidogo.

   
 • Tarehe: 5:18:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger mark msaki

  Kaka Jeff,

  ni jana tu nilikuwa nimemuandikia bwana Freeman kupitia freeman@chadema.net (chadema wanapatikana www.chadema.net) kuwa ni hatari sana kwa kiongozi kama yeye kusema kuwa upinzani umekufa rasmi! huu ndio muda wa kuchanua! nilimueleza pia kuwa jambo kubwa la kufanya pamoja na kuweka muungano wa upinzani pia ni kwamba elimu ya uraia ni muhimu kuosha bongo za wananchi! kuna haja ya kufuta vitisho miongoni mwa wananchi ili waweze kusema msimamo wao bila kujali kikosi cha yanga! suala lingini ni kuwa sasa tunahitaji walimu wa siasa (makada) na wakuu wa propaganda! - hawapo kabisa kwenye kambi ya pili hawa!wakuu wa propaganda ambao husema maneno yanayochoma bila kuangalia makunyanzi! bwana Jeff, uko kama mie, nakwenda mbele nikisema siasa basi lakini ninaathirika zaidi! tafadhali pokea rasmi jukumu la kusaidia kitengo hiki cha propaganda! sijui kitawekwa lini na kitazinduliwa vipi, lakini kazi iko mbele yetu!

   
 • Tarehe: 8:03:00 AM, Mtoa Maoni:- Anonymous phabian

  phabian,nimefurahishwa na mpangilio mzuri na mtiririko wenye mantiki anoutumia bwana jeff na kama sikosei ninahisi mfumo huu ni mzuri kwani haumtaji mtu ila unaiweka bayana dhambi au uhozo unaofanywa na watu na ninatumaini baada ya muda si mrefu mfumo huu utatawala blogu nyingi kwani nimekwisa liona hilo katika makala mpya ya bwana boniface na dada mmja kutoka Dodoma.Kazi ya kuuzindua umma wa waTanzania ni ngumu mno kwani wahitaji wa elimu hii wengi wao wapo vijijini ambao kwao kununua gazeti ni anasa au kitu ambacho hakipo kabisa katika bajeti zao finyu,pia na wale waliopo mijini bado tatizo la kutumia kompyuta ni kubwa ukizingitia tekinologia hii ni mpya uku kwetu na mwisho hawa vigogo ambao ndiyo walengwa hasa pia nao internet bado ni jambo la kujishauri kutumia.Ka hivyo tuwe makini isije kuwa wasomaji wa makala hizi za blogu wakawa wanablogu wenyewe kitu ambacho si hasa lengo .Ila msife moyo kwani tatizo hili ni la kitaifa. mwanzo sikuzoie huwa ni mgumu.

   
 • Tarehe: 8:58:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger mwandani

  Nimesoma kama natazama sinema. Mpangilio wa ligha ya picha safi sana, inabidi nikupe alama ya zote.

   
 • Tarehe: 7:44:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger Jeff Msangi

  Ahsanteni sana wachangiaji wote.Mlioniomba kuchukua silaha na kuweka begani(kama Mark kutoka kule bondeni) napenda kukuhakikishia kwamba nipo tayari.Unajua hii huwa ni darubini yangu nikiangalia nchi yetu Tanzania.Kimakusudi kabisa kuna watu hawataki watanzania(hususani walio vijijini) wasifunguke macho na kujua kwamba viongozi ni watumishi wetu na sio vinginevyo.Upofu huo ndio unasababisha kuwe na "wabunge wa maisha" bila ya kufanya lolote la kujivunia katika majimbo yao.Inawezekana vipi?Ni kwamba wanacheza na akili za watu tu.Ndio hizo pilau za usiku na chai kavu,isiyo na sukari wala maziwa asubuhi yake.Kuendelea tu kusema kwamba "yana mwisho haya" kama vile Kuli haitoshi.Ilitosha enzi hizo.Mazingira ni tofauti,lazima tumulike ili sote tuone na asiwepo anayepapasa.

   
 • Tarehe: 12:58:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Boniphace Makene

  Jeff nimekuwa hapa tangu jana nikipitia kitabu cha Mandela Long Walk to Freedom, sikuwahi kukisoma hiki. Nimshukuru kwanza huyu bibie aliyeniona sina la kufanya jana akaamua kuingia katika shubaka lake na kukitoa hiki na kunipa. Nampongeza huyu maana amekuwa moto wa msumari katika hamasa za mapigano ya mfumo wa kimapambano katika maisha yangu. Hakuna njia fupi, tunatakiwa kutokulala na tunatakiwa kusoma sana fikra za watu wengi. Kuna bwana anaitwa Analaeskas alikuja Marekani baada ya kukimbia siasa za Urusi na huyo jamaa kaichambua Marekani katika Discovering America as it is na utaona umuhimu wa mfumo Nyerere aliokuwa katupandikizia watanzania. Hata haya machungu yanatokana na hamu ya maisha ya mfumo huo. N ahakuna kukata tamaa. Kushindwa kwa vyama vya upinzani Tanzania kulitegemewa hii haina maana kama Watanzania hawaoni wala hawajali shida zao. Hwajamuona masiha na hawajaonyeshwa njia, huwezi kutangaza kuitoa CCM kuwa ndio upinzani. Upinzani ni kuingia katika hamasisho la Uchumi na njia bora za maisha ya watanzania. Upinzani hauna maana ya kupambania dola, waache washikamane na dola lakini nguvu ipelekwe katika kuwahasisha wananchi kutafuta nguvu za uchumi. CUF wanafanya jambo moja kimya kimya lakini kibaya chao wanalifanya kwa upande mmoja wa nchi. Wanasaidia kielimu vijana wao wa Zanzibar ughaibuni. Elimu ni njia na tangu nimefika huku nimeweza kujua yale yaliyokuwa yamefungwa katika mfumo wa siasa za Tanzania. Watanzania wamepofushwa wasione na vyma vinahitaji watu wenye kuweza kuwasaidia Watanzania waone kisha kuwapa ujasiri wa kuona tofauti. Siasa si kuvaa suti, watanzania wanataka kuona mbadala wa maisha na mifumo ya viongozi wao, hii ni kazi ya vyama, sioni haja ya vyama hivi kuwa lukuki au kwa kuwa ni shilingi 50000 za Tanzania zinazotumika kama ada ya kufungua chama? Jeff ikishindikana kuna haja ninyi mlioko huku mrudi na kundi mbadala na hii ndiyo agenda ya 2010. Tuanze sasa kujipanga naamini mambo yatakuwa. Narudia tena tatizo si chama suala ni mhimili upi mbadala wa chama hicho na maendeleo sadifu kwa wananchi.

   
 • Tarehe: 3:20:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger mark msaki

  kaka jeff!!

  tunashukuru sana sana kwa kukubali kufanya kazi hiyo ngumu!! tunashukuru kwa jinsi ulivyoipokea bila hata kupoteza muda!! unanikumbusha jinsi Masiha alivyokipokea kikombe cha uchungu!!tuendelee na mchakato wa jinsi muundo mbinu wa kuendelea mbele! sasa tunaachana na kingunge na sozigwa!! karibu sana kaka jeff!!!wewe hakika ni mkuu wa propaganda!! ufanye kazi hiyo na ukuze vijana katika zoezi hili zima la kubadili kanisa kuwa taifa huru!!!!

   
 • Tarehe: 7:16:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Phabian

  kaka jeff asante kwa kukubali kuwa mkuu wa msafara,HATUA YA KWANZA KATIKA JAMBO LOLOTE MARANYINGI HUANDAMWA NA VIKWAZO NA PINGAMIZI ZA KILA AINA,LAKINI NI HATUA HIYOHIYO INAYOKUPELEKA KWENYE MAFANIKIO YA KWELI.

   
 • Tarehe: 5:19:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Mija Shija Sayi

  Ipo kazi! ninaamini hadi leo huko vijijini kuna watu hawajui Nyerere aliko. Ni aibu kwamba bado hatujaweza kusambaza vyombo vya habari vya kutosha nchi nzima, Nasema ni aibu kwa vile uwezo tunao ila ubinafsi tumeutanguliza mbele.

   
 • Tarehe: 5:56:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Bwaya

  Bwana Jeff, unachokisema ni kweli tupu. Nimesoma nikasikia kuguswa sana na namna ambavyo umeuweka ujumbe wako bayana, kiasi kwamba unaposoma unalihisi tatizo vilivyo. Na kusema kweli ndivyo ilivyo.
  Nasikitika sana kwamba hiyo ndiyo hali halisi ya Wananchi tuliowengi, ingawa ni "Ujinga" tu nadhani, unatufanya tuendelee kukipa ushindi wa kishindo chama tawala.
  Ni chama hiki hiki kimemsababishia wmwananchi huyu matatizo yote hayo aliyonayo, lakini ni fulana hiyo ya njano tu imetosha kuhalalisha wizi mpya kwa kasi mpya na nguvu mpya.
  Jambo hili nimeandika kidogo katika blog yangu,naomba unitembelee tubadilishane mawazo kidogo.

   
 • Tarehe: 7:14:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger picha zenu

  Unauliza Nyerere yuko wapi? Kwani hujui kama kadead?

   
 • Tarehe: 4:12:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger Dickens

  nyerereangali mzima kifikra ata kama alikopy na kupesti idia za kirusi na kichina, alifanya mambo yake ama maajabu yake akaondoka hakufa kama watu wengine wafikiriavyo hatakufaje mwenye fikra.

  ukienda matombo na kaguru utaambiwa mkapa kauvaa unyerere ndio watakuelewa vivyo vivyo kwa kikwete naye ameuvaa unyerere.

  kama tukiamua kuleta mashindano ya hotuba za hawa mababa wa tanzania hawa watatu wawe wanaongea (mbichi)(moja kwa moja) wazungu wanaita live ma tuiweke caseti ama kitu chochote ambacho kimerecodi sauti ya marehemu nyerere nakwambia hapo nyerere atawathibitishia ya kwamba ni mzima hajafa ila wengine ingawa ni wazima tutakuwa na mashaka nao na ni rais kusauliwa kama waliwahi kuwa marais wa tanzania

   
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker