Mtanisamehe kama ninalotaka kutoboa hapa ni gumu kama paa la zege.Nimepata ndoto,nimeota nimekaa pembeni mwa bahari.Sina uhakika kama ilikuwa ni maeneo ya kigamboni au pwani ya raha leo pale jijini Tanga.Ninachokumbuka ni kwamba nilikuwa kifua wazi huku nimevaa msuli fupi.Nadhani wale mnaojua shughuli za uvuvi mnaelewa nilikuwa nimevaa nini.Ni majira ya jioni,karibuni jua linazama.Bado sijafanikiwa kupata samaki angalau wa kutosha kwa mlo wa familia na wengine nipeleke pale gulioni ili nipate faranga za kununulia mitumba ya waitaliano,nasikia ni mizuri kuliko ile ya waingereza.Kikwapa kinacheua harufu ya mferejini maana siku nzima pembeni ya maji chumvi sio mchezo,hata ukikoga hutakati,shombo ya samaki bwana,ah!
Cha ajabu bahari imejaa samaki mpaka nawaona wakielea juu juu.Wengine wanacheza kama vile kiwi,dolphino na chamaki nchanga.Nadhani ushawahi kumkurupusha chumbani mwako chamaki nchanga ukaona jinsi anavyotoka mkuku.Kijasho kitakutoka kwa sababu utabinua vitanda na makabati karibuni yote.Nguvu kipindi hicho unakuwa nazo maana chamaki huyu ashakutia hasara sana tu.Ashararua viwalo vyako vyote vya kutokea. Samaki wanazidi kunichenga ingawa nyavu yangu bado ni mpya. Au labda ujuzi wa uvuvi umeanza kunitoka?Mbona???? Taratibu jua linaanza kupotelea magharibi,miayo na uchovu vimenitawala. Nashtuka huku nikiwa nimeloa jasho.Nini maana ya ndoto hii??
Blogu naifananisha na bahari.Wavuvi ndio wanablogu wenyewe yaani waandishi.Wanunuzi wa samaki ni wasomaji,wachangia mada na hoja,wapambe,warekebishaji wetu. Na kwa sababu wavuvi nao hutokea wakawa wanunuzi(hususani katika zile siku wanaposhindwa kwenda kuvua au wanapokuwa kama mvuvi mimi niliyetoka kapa) basi sote tunahusika.Haijalishi kama tunafunga safari kwenda sokoni au tunaketi tu nje ya vibaraza vyetu tukisubiri sauti ya mchuuzi "haya tena samaki wa reo reo, kina baba na kina mama samaki kwa afya zenu,hero hero baba juu,mama chini, samaaaaaaki" nk
Sasa kama sisi ni wavuvi,wanunuzi wanatutegemea sana.Na wanatutegemea tuwaletee kila aina ya samaki sokoni.Wanataka changu,kambale,pweza,nk.Lakini hali inakuwaje kama wanunuzi wanakuja sokoni na kukuta hakuna samaki wa aina yoyote ile?Ni wazi kwamba watakuwa hawana jinsi zaidi ya kusaka mlo wa aina nyingine,pengine watakula dengu au choroko watulie wasubiri mashuzi.
Hii inaweza kuwa ndoto tu, ndoto ambayo haihitaji kwenda kwa babu chalii kupatiwa tafsiri.Msamaha niliouomba hapo juu unahusiana zaidi na kuona kwangu kwamba kuna "ubaridi" fulani katika uwanja huu wa blogu.Nimejaribu kupitia blogu kadha wa kadha,naona wengi shughuli zimewawieni nyingi.Wengi hamuandiki tena,hamtoi hoja,hampiti uwanjani,hata peku huku umande ukiwa umetanda.Wanunuzi tumewasahau.Najua hili jukumu ni la kujitolea,halina malipo ya moja kwa moja ingawa malipo ya kijamii ni mengi sana.Kwa vizazi hivi na vijavyo,vyetu na visivyokuwa vyetu.Naizungumzia dunia hapa.Nawasihi tuendelee kujitolea. Makene na Ndesanjo wamesimama mstari wa mbele katika kuleta wanablogu wapya.Hili ni jukumu letu sote. Lakini litawezekana tu endapo mualika anakuwa hima kuandaa mazingira ya mwalikwa.Kama ambavyo Ndesanjo amesema leo katika blogu yake,safari ni ndefu na sisi ndio tumeianza tu.Tunachojenga hapa ni msingi.Sasa kama mnavyojua zege halilali.Ninachoomba wanapokuja wanunuzi sokoni,wasikose samaki.Wakikosa hawatokuwa na hamu ya kugeuka kuwa wavuvi.Watahisi bahari imekauka! Ikiwezekana kila siku tutume japo chochote,hata kama ni dagaa wa kigoma.Hii itasaidia kuleta mapinduzi tunayoyatarajia. Aluta Kontinua!
Nimesoma Jeff, nimesoma....