VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Monday, February 27, 2006
UMELETA NINI.......

Kijua cha magharibi kimeanza kuzama.Nimesimama pembeni ya bahari juu ya kijiwe nikiangalia feri ikiondoka kuvusha wananchi wanaoishi Kigamboni. Harufu ya samaki imetanda,wabichi na wale wanaokaangwa.Kila mtu anaonekana mwenye haraka,wengine wanakimbilia kupanga foleni ili feri ikirudi waweze kuvuka na kuwahi makwao.Wanakimbizana na kupishana na magari.Madereva nao wanakuwa kama hawawaoni wananchi wenzao.Ni juzi tu jamaa mmoja alikanyagwa vibaya na gari katika heka heka hizo hizo za kuwahi usafiri huu wa majini.Mzungu mmoja kutoka Uholanzi majuzi aliwaacha watu midomo wazi aliposema kwamba anakikumbuka hicho kiferi kwani kiliwahi kufanya kazi huko kwao miaka mingi sana iliyopita kabla hakijapigwa marufuku kutumika.Imekuwaje serikali yetu ikanunua kitufe hicho?Mzungu kuhakikisha kwamba ana uhakika na analolisema aliingia na kuwaonyesha mashuhuda mahali alipowahi kuweka “chata” yake enzi hizo za ujana wake.Yaani hata rangi ilishindikani kupakwa! Watu walibaki midomo wazi.

Wachuuzi wa samaki nao wanakazana kufanya biashara ya jioni au mwisho wa siku.Ule msemo wa biashara asubuhi nadhani hauna maana kwao.Kibaka mmoja anapora pochi ya mwanadada mmoja na kukimbilia majini.Kelele za dada huyu wala hazimsumbui mtu.Kwanza kelele za kila aina zinasikika kutoka kila upande.Sijui lini vibaka hawa wataacha mchezo huu wa kupora na kukimbilia majini.Jumatatu iliyopita mmoja wao alichomwa moto na kufariki hapo hapo.Inasemekana waliomchoma moto ni vibaka wenzie ambao alikuwa amewadhulumu katika mgao baada ya kufanikiwa kukwapua pochi ya mtalii fulani kutokea Italia.

Honi kubwa ya meli inasikika upande wangu wa kulia.Ni meli kubwa ya mizigo kutoka Ulaya.Naiangalia bila hata kuchezesha kope.Namkumbuka mjomba wangu Kandiko aliyeondoka nchini miaka mingi sana iliyopita.Enzi hizo bado nilikuwa sijaja jijini Dar ila naambiwa alifanya kinachoitwa “kuzamia” meli.Mpaka leo hii hakuna anayejua kwamba yu hai au alishakufa.Mara ya mwisho tunasikia alionekana nchini Sweden akiwa ameambatana na rafiki yake wa kike mzungu.Jirani yake mjomba wangu mwingine,ambaye ndipo nimejihifadhi hivi sasa,ndiye alikutana naye huko Sweden.Moyo unanienda mbio kwa sababu hata mimi naona karibuni nitafanya hivyo hivyo.Maisha yanazidi kunikaba koo.Sioni mbele na hata huko nyuma nishaanza kupasahau.

Leo ni mojawapo ya zile siku mbaya kabisa kwangu.Nimezunguka mji mzima nikitafuta kazi.Kazi yoyote jamani,natafuta hata kazi ya kusafisha vyoo vya jiji lakini sipati.Naambiwa ni lazima umjue mtu hapa.Kama humjui mtu basi jiandae “kuzama” mfukoni na kutoa chochote. Hebu niambie ndugu yangu,dunia hii ina maana tena? Yaani kupata kazi kwanza utoe hela.Utaipata wapi hiyo hela?

Mfukoni sina nauli ya basi.Inanibidi nianze safari yangu kwa mguu kuelekea Kinondoni,pale karibu na makaburini. Najua safari ni ndefu tena nikizingatia kwamba mlo wangu wa leo mchana ulikuwa “chips dume” kwa kachumbari. Nakatiza pembeni ya ukuta wa Ikulu kuu ya Tanzania.Humo ndimo anamoishi raisi na wapambe wake. Naliona kwa ndani hilo jumba linaloitwa “white house”. Askari wametapakaa humo ndani.Wakati bado nikishangaa jengo hilo jeupe askari wengine wananitokea kwa mbele yangu na kunisimamisha. Wananihoji maswali chungu mbovu kabla ya kuniweka chini na kunisachi mwili mzima.Eti mimi ni nani na ninafanya nini kwenye kuta za ikulu.Nawaeleza kwamba naelekea nyumbani baada ya siku ngumu ya kutafuta kisichopatikana.Wananiambia inakuwaje sina hata senti tano mfukoni,lazima niwe mwizi mimi.Baada ya kuniweka kwa karibuni nusu saa wananiachia na kuniamuru nipotee. Ndani ya nchi yangu mwenyewe,tabu zilizoje hizi?

Nakatiza viwanja vya mpira wa kikapu.Huwa natamani na mimi nijifunze mchezo huo.Rafiki zangu wa kijiweni pale Kinondoni kwa manyanya wananiambia kwamba kwa urefu nilionao ninaweza kucheza vizuri mchezo huu.Ingawa kiza kimeshaanza kuingia bado kuna vijana wanacheza.Nahisi hawa wanauhakika wa mlo wa jioni.Au wazazi wao wanakuja kuwachukua.Hii ndio ile mitaa ya wenye nacho au wenye nchi.Najaribu kuwaomba nauli lakini wananisakama kwa maneno kwamba mie mwizi.Hivi kwanini kila mtu ananiambia habari za wizi?Au niwe mwizi kweli nini?Wee ngoja tu

Nakatiza maeneo ya Seaview sasa. Mbona kila nimuonaye hapa ni mhindi? Hivi nipo India au mitaa ya Dar-es-salaam nchini Tanzania?Sitaki kuliongelea zaidi hili wasije wakanisikia na kuniita mbaguzi.Maombi yote ya kazi ambayo nimeyafanya ni kwenye kampuni wanazomiliki hawa jamaa.Niseme nini?Nikisikika je? Nazidi kuchapa mguu huku nikijiimbia nyimbo mbalimbali ili nisisikilizie uchovu.Cha ajabu wimbo uliotawala kichwa changu ni ule unaoitwa Shida.Hivi nani aliimba wimbo huu?Nishamsahau lakini wimbo wenyewe una maneno kama “ shida hizi mpaka siku ya mwisho……”’

Moyo unanienda mbio zaidi na zaidi,karibuni nikatishe kwenye kituo cha polisi Salendar Bridge. Nitapitaje pale,askari wakinisimamisha watanifanya nini,wataniuliza nini?Makundi mawili huko nyuma yashaniita mwizi.Tizama amani ilivyonitoka ghafla.Lakini mbona nasikia Tanzania ni nchi yenye amani?Hili neno amani lina maana gani kwani?

Napiga moyo konde,naanza na kupiga mruzi.Wimbo unabakia ule ule…shida. “Wee kijana,kuja hapa” Roho kidogo inipasuke.Kumbe siitwi mimi bali kijana mmoja muuza kahawa. Polisi bwana,kwani hawezi kumuita mtu kwa heshima na adabu? Naongeza mwendo na kuanza kuvuka hili daraja maarufu. Upepo kutoka baharini unazidi kuwa mkali.Lakini harufu kutoka huko nayo sio nzuri.Wanamazingira naona washalala usingizi.

Miguu inatetemeka kwa uchovu.Ndio nakatiza makaburini Kinondoni.Aisee naona mwanamke na mwanamume wanakokotana kuelekea makaburini.Mtindo wa kufanya mapenzi makaburini unazidi kujipatia umaarufu usio rasmi.Hivi kwanini?Nasikia majuzi askari walipofanya doria katika makaburi haya walikuta pea za watu kama kumi hivi makaburini.Nimefika nyumbani.Sauti kali ya shangazi inauliza “haya mwenzetu umeleta nini kutoka huko kwenye kupuyanga???”
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 7:32 PM | Permalink |


Maoni: 6


  • Tarehe: 8:36:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger John Mwaipopo

    Wimbo huo uliimbwa na hayati Mbaraka Mwinshehe. Hapo umenikumbusha pia "Mtaa wa Saba", ambamo analalamika kuwa amehamia mtaa wa saba baada ya kuchoka na ulozi (uchawi)kulee
    "nilikokuwa nikikaa zamani,
    Ile nyumba sio nyumba,
    Iilikuwa na mikosi oooohh.."

    Samahani nimetoka nje ya mada kidogo. Ni kumbukumbu tu ndiyo iliyonifanya hivyo.

     
  • Tarehe: 10:38:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger boniphace

    Jeff hapo ulipomalizia tu ndipo panaponikuna. Miwsho wa riwaya huwa mgumu sana kuupata lakini hapa umefanikiwa kabisa kupafikia. kAZI NZURI SANA BADO INALALA KATIKA MAUDHUI YA KUTANUA FIKRA ZA KUMJENGA MASKINI MZAWA WA TANZANIA, TUFANYE NINI NA NAFASI INAPOTEA HUKU MUDA UKIKIMBIA KWELIKWELI?

     
  • Tarehe: 10:55:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger Jeff Msangi

    Makene,
    Tufanye nini ndilo swali gumu lisilo na majibu rahisi.Muda unavyozidi kututupa ni tishio la kizazi chetu na kijacho.Naamini tumeanza,labda tuongeze kasi,twende kwa mwendo wa kangaroo

     
  • Tarehe: 8:51:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger FOSEWERD Initiatives

    shot kulia kavimba mkia daima mbele kwa kasi mpya nyuma kurudi mwiko!

     
  • Tarehe: 4:44:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger MICHUZI BLOG

    jeff we ni bonge moja la mwandishi wa riwaya, hujajistukia tu. hebu weka pamoka vijimaneno vya kujaza kurasa 100 uone, hasa ukizingatia toka elvis musiba alipokoma na wille gamba wake, hakuna simulizi za kusisimua. usilaze damu ndugu yangu. najua nasema nini

     
  • Tarehe: 5:48:00 AM, Mtoa Maoni:- Blogger mloyi

    Unasema ile pantoni ilishapigwa marufuku miaka mingi iliyopita! Inawezekana kwani tumrjisahau tulivyokuwa na tulivyo sasa?
    Mimi ni mmoja ya watumiaji wakubwa wa pantoni hizo, ninavuka nazo siku sita kila juma. Unajua kulivyokaribu, kama sio maji ni mwendo wa dakika chini ya tano kwa miguu, lakini huwa tunatumia kama ishirini kwa hiyo pantoni! siku nyingine walichukua masaa mawili kuvuka pale, hii inaashiria kwamba siku nyingine hawatafika ng'ambo siwezi sema wataishia wapi! ila wenye akili! na wanaotakiwa kufanya maamuzi wafanye hivyo. Siku hizi ninaona linaelea na mafundi ndani .Dereva hawezi kubadili gia bila ye mafundi kugongagonga ingini kwanza ndio wampe ishara ya kuendelea au utakuta inabidi ligeuke upande mwingine likiondoka(siri yake ni kwamba ingini moja haifanyi kazi) na wakati wa kuteremsha magari inabidi yatoke kwa rivesi.
    wakati mwingine nafikiria hivi hawa watu hawaoni umaarufu na umuhimu wa hili dude unavyozidi kukua, kwanini hawachukui hatua madhubuti kuliimarisha.
    Labda wanangojea litoke la kutokea kama MV Bukoba ndio waunde tume ya kufuatilia kilichotokea na kutoa maamuzi. sijui..

     
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker