Sunday, February 12, 2006

USINIUZE KWA DINARI

Hata wewe ulidhani nimeghairi,
Wanadamu ndivyo mlivyo, kidogo mnifungulie daawa
Sijaghairi kama vile mkimbiza baghala anapokutana na kisiki,
Tafadhali usije nibagua,nibainike kuwa tofauti
Nikaja chinjwa kama vile mtusi,
Itakuwa rahisi kubainika,wajua pua yangu ni ndefu
Siku zote nimekataa balaa hizi,tatizo zenyewe hazijanikataa bado

Nitabambua lipi ndugu yako?
Wenye nchi wanasema mimi baradhuli
Nabatilisha uongo kuwa ukweli,si wamesema wao jamani?
Wakaweka bayana kwenye runinga ya serikali,
Eti mimi siachi kupayuka,kijinga cha moto wakadhani kimezimika
Loh! Wamenoa,naogelea kwa kutumia kope sasa
Nakuwa kama beberu la mbegu,halichinjwi kamwe

Bedola zangu kwapani,sina kingine zaidi ya kichwa
Mwili mzima ni mabehewa,mwisho wake haujulikani
Mioyo yao imejaa beliari, midomo yao myekundu kwa damu
Eti nafa kwa njaa, dunia imejaa unaa
Bado wanapeperusha beramu zao, wanakenua kama ngiri

Yanibidi nianze kukimbia, nisije kuwa kiburudisho
Nijivike bushuti, nipake na manukato
Nisije enda kama buu
Mafedhuli wakaja nibwaga,mwalimu usinifunze upuuzi!

5 comments:

  1. Anonymous11:43:00 PM

    Jeff,
    Ngoja nikale nije kurudia kusoma ulichoandika. Da! Nikiwa na njaa huwa sifikirii vizuri. Na uliyoandika yanahitaji kufikiri. Jeff, saa nyingine tunataka mambo mepesi mepesi...au hujui sababu gani tunapenda magazeti ya upashkuna na uzabizabina?

    Nakutania, kufikiri ni aina ya zoezi fulani la ubongo.

    ReplyDelete
  2. Jeff kuna malenga wawili wamesusa baada ya mimi kukaa kimya kujibu. Umenikumbusha sasa kutumia shairi langu la zamani kesho lisome kibarazani kwangu.

    ReplyDelete
  3. Ndugu yangu naona hisia kali.
    Nahisi uliandika ukiwa mtuliivu.
    Nimelipenda shairi.

    ReplyDelete
  4. Anonymous4:59:00 AM

    Mstari wa mwisho huo: mwalimu usinifunze upuuzi...
    Hiyo ni kauli nzito sana. Hivi nani atamfunza mwalimu?

    ReplyDelete
  5. kha hata mie nimechoka sana sasa hivi...nadhani nikapate msosi kwansa halafu nije kusoma upya hii habari...

    Jeff, bwana Makene aliuliza pale bloguni kwangu utupe maelezo kuhusu chuo cha polisi Ontario, baada ya kuianika Cv yake pale...maana huku ndiko CV ya bwana Omari Mahita inasema alihitimu...

    1. je kipo hiko chuo?
    2.je kinafundisha nini siasa au upolisi? na kama upolisi ni huu tunaoujua sie ?
    3.je kiko kwenye viwango vya kimataifa?

    ReplyDelete