Mara nyingine huwa naota ndoto za usawa duniani. Nathubutu kuziita ndoto kwani ni wazi kabisa kwamba katika siku za maisha yangu dunia haitokaa isheherekee "usawa na haki" ambazo wengi tunazipigia mbinja kila kukicha. Lakini hili lisitukatishe tamaa kwani imani ni kwamba vizazi vitakavyofuata vitaweza kufaidi matunda ya vuguvugu tunalolianzisha hivi sasa.
Leo nimekutana na habari ambayo imenigusa kidogo. Imenigusa kwa sababu sio tu muathirika wake ni Afrika bali kwa sababu chembe chembe za "usawa hazipo. Habari yenyewe inahusu kupigwa marufuku kwa baadhi ya ndege za abiria za Afrika kuruka na kutua katika nchi zilizopo kwenye Umoja wa Ulaya.
Nilipoisoma habari hii baada ya kuwa nimeisikia kwenye vyombo vingine vya habari kama televisheni mara moja nikakumbuka suala la uchakavu wa ndege za "Ulaya" zinazorandaranda katika bara la Afrika.Kama umewahi kusafiri kutokea Afrika kisha ukatua Ulaya kabla ya kubadilisha ndege kuelekea huku America ya Kaskazini ni wazi kabisa utakuwa umegundua kwamba ndege zinazofanya safari zake baina ya Ulaya na Afrika(za mashirika ya ndege ya Ulaya) ni za viwango vibovu kabisa ukilinganisha na zile unazopanda ili kuja Marekani au Canada. Hili wao hawalioni au wanadhani sisi hatulioni. KLM inayokutoa Dar-es-salaam mpaka Uholanzi ni tofauti kabisa na inayokutoa Uholanzi kuja Toronto. Hali ni hiyo hiyo ukipanda British Airways,Swissair,Lufthansa nk. Rafiki yangu mmoja aliwahi kuziita majeneza yanayopaa. Kwa maana hiyo naushangaa umoja wa Ulaya unapoona viwango kwa macho ya makengeza (samahani).
Kwa maana hiyo nchi zetu za Kiafrika nazo ziwe na haki kabisa ya kupiga marufuku ndege hizi kuruka au kutua barani Afrika. Ni nani anazikagua za kwao? Mbona hata kwa macho tu zinaonekana kuwa majeneza yanayopaa??
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:59 AM | Permalink |