
Wiki chache zilizopita Michuzi alituwekea picha hii hapa.Nia ilikuwa ni kutuonyesha watoto wakiburudika na kufurahia maisha. Nakumbuka baada ya kuiona picha hiyo nilionya juu ya michezo tunayowaruhusu watoto wetu wacheze bila kusahau sinema tunazowaonyesha au kuruhusu tu kiholela waangalie bila kujali madhara tunayotengeneza kwenye akili zao. Kero yangu kubwa imekuwa jinsi ambavyo watu wengi wanachanganya maana ya maendeleo na jinsi tunavyotengeza taifa la kesho lenye mtindio mbaya kabisa wa akili.
Kuwaonyesha watoto wetu sinema za kihuni,uvutaji bangi,umalaya,kuwanunulia matoy ya bunduki nk ndio eti tunayaona ni maendeleo. Siku zinavyopita tunazidi kutupilia mbali tamaduni,mila na desturi zetu za asili, tunavyozidi kuuona na kuwaambia watoto zetu kwamba ni wa kizamani,haufai na sio wa kimaendeleo.Hili hunikatisha sana tamaa.Nakuwa naona kiza kikubwa mbele yangu kila niliwazapo taifa letu lijalo ambalo ndio tegemezi letu kubwa.
Katika pitia pitia yangu ya magazeti ya nyumbani hivi leo nimekutana na mkasa wa ulionisikitisha sana na ambao kwa kiasi kikubwa unabeba ninachojaribu kukiongelea hapa.Mkasa wenyewe huu hapa. Tafadhali usome kwanza kisha uniambie je haya sio madhara ya wazi kabisa ya "maendeleo" ninayoyapinga mimi.Huoni kwamba si ajabu huyu mwanamke/mdada wa miaka 20 alidhani pengine anafanya kama anachokiona kwenye "Days of our lives" tu? Nani alimruhusu binti huyo mdogo awe na kitu cha moto kama bastola?Huu ndio uzazi jamani? Tunakoelekea ni wapi??
Kwa bahati mbaya hii familia iliyofanya haya ina jina sawa na mwanablogu mwenzetu Mark Msaki! Samahani Mark unamfahamu Msaki huyu ambaye binti yake amefanya dhahama hii?
Kwanza nampa pole yule mtoto wa shule ya msigi aliyesasambuliwa makalio. Mchezo aliokuwa akicheza, mpira, ndio hasa inayowafaa watoto. Wengine tulikosa mwelekeo wa michezo chanya hii kwa u-endelevu.
Pili ni ulimbukeni. yafaa nini kuizagaza bastola pahala popote katika nyumba yako. Ona imesababisha binti kugeza vizungu na kumsasambua kijana. Ama ilikuwa kaiba chumbani kwa baba yake ama huachiwa pale 'aliliapo'. Si unajua kudeka.
La tatu: yawezekana hatujajiandaa na ujio wa sinema kule Bongo. Huku nchi zilizoendelea, pamoja na ujinga wote huu kufanyika, wazazi wengi ni makini katika kujua nini watoto wanastahiki kuona na nini hawastahiki. Wamefikia hata hatua ya kuweza kuitawala TV kwa teknolojia. Yafaa tutambulishe vifaa hivi na mwamko huu Bongo.
Nne: nalo ni ulimbukeni. Kumbuka Tanzania tumechelewa sana kujua TV ni nini. "Hii maneno" imetufanya tuwe mbumbumbu wa kuchambua mema na mabaya ya teknolojia hii. Kilichokuwa ni kuwa ilipoletwa tulikuwa sasa 'tumepumua.' Lijalo na lije bila censorship ya aina yoyote kutoka serikalini hata majumbani mwetu. Hebu fikiria pale ulipokuwa na njaa kwa muda mrefu halafu ghafla waletewa chakula. Nahisi utafakamia halafu utavimbiwa.
Changamoto yangu hapa ni kuwa midhali Video Industry imeanza kupata wasaa Bongo, ni wasaa sasa tuwe na wataalamu wa kutengeneza filamu za kuwafaa watoto. Mathalani ni wasaa sasa kuweka katika filamu zile hadithi za jumamosi RTD za Mama na Mwana. Kilichopo sasa watu woote watoto wa wakubwa wanashabikia filamu zile zile za kikubwa mfano ile iliyotoka mwaka 2003 iliyoitwa girlfriend. Watengenezaji wa filamu Bongo watengeneze filamu za kuwafaa watoto na watu wazima tukumbushane umuhimu wa kulea maadili ya kibongo.