
Ni jioni ya tarehe ya leo kwa saa za hapa Toronto. Jua ndio linazama(picha kulia shahidi) huku manyunyu nayo yakitiririka( kwa bahati mbaya kamera yangu imeshindwa kuyapata manyunyu-Michuzi utaniambia wakati ujao nifanyeje).Kwa hadithi na simulizi zile za zamani,simba anazaa! Leo ni mojawapo ya zile siku zenye mchanganyiko wa hisia kadha wa kadha,siku zenye maswali mengi yenye majibu machache.Sina uhakika kuhusu machozi ya huzuni au ya furaha kwa sababu sikumbuki mara ya mwisho kupata machozi ilikuwa ni lini. Hii isije ikakudanganya kwamba sijawahi kulia kamwe,la nilishawahi na nilipata ahueni nilipohakikishiwa siku moja kwamba kulia ni sawa,ndio ni sawa hata ukiwa mwanamume! Nadhani hii ni tofauti na tulivyolelewa kuamini tangia utoto wetu..."mwanaume halii bwana,jikaze" Kuna haja ya kuwaambia watoto wetu msemo huu kwa umakini siku hizi.Wakijikaza,wakifa kiume matokeo yake huwa ni yale wanayoyapenda sana watengeneza habari wa vyombo vikubwa vya habari..ni damu na maafa.
Mchanganyiko huu wa mawazo niliuanza jana baada ya kuongea kwa simu na Makene. Lazima nikiri kwamba Makene amekuwa akinipa mwamko wa mawazo yenye msingi sana kila mara tunapopata nafasi ya kuongea. Hivi sasa anamalizia kitabu chake, namuahidi kuwa mmojawapo wa wanunuzi wake wa mwanzo. Jana tukajadili suala moja ambalo mara nyingi huwa hatulitilii maanani sana. Hivi kwanini katika mitaala na orodha ya vitabu vya kusoma shule za sekondari hususani kwenye somo la kiingereza hakuna kulichoandikwa na mtanzania? Kwanini watanzania hawamo katika lile kundi la African Writers Series? Kwanini tusome vya akina Ngugi, Soyinka, Achebe, Kwei na wengineo bila kuwepo kina Msangi, Macha, Makene, na wengineo. Kama tumeshindwa kuandika kwanini basi tusitafsiri tu hata kazi kama za Kuli (unaweza kukisoma kitabu kizima hapa mtandaoni,shukrani kwa tekinolojia!) na vile vya akina Ngoswe vikawa katika kiingereza?Nia ni kuwa na upande wa shilingi ambao una picha zetu,historia yetu,hadithi za tamthilia zetu,tamaduni zetu,shida na raha zetu nk.
Wakati tukiyajadili hayo nikamuuliza Makene kama amewahi kusoma vitabu vya mtanzania Godfrey Mwakikagile? Wangapi tunamjua huyu bwana na kwamba vitabu vyake vinatumiwa hata katika vyuo mbalimbali duniani? Kitabu chake kimojawapo nilicho nacho ni kile kiitwacho "Africa is in A Mess: What Went Wrong and What Should Be Done" Ni kwanini hiki kisiwemo kwenye orodha ya vitabu vya kusomwa nchini mwetu? Au ukweli unauma? Katika kitabu chake kingine kiitwacho "Relations Between Africans and African Americans: Misconceptions, Myths and Realities",Mwakikagile anatoa hoja nzuri sana kuhusu mahusiano ya waafrika na wamarekani weusi au waafrika wamarekani. Kama unafuatilia maandiko yangu mara kwa mara utakuwa umegundua kwamba hii ni hoja ambayo huwa napendelea sana kuijadili. Soma "chapter five" ya kitabu hicho kwa kubonyeza hapa.Ukivutiwa na hoja zake basi nenda dukani ukanunue kitabu hicho na kile pale juu, uwe nacho kwenye maktaba yako.Kwa bahati mbaya sijui G.Mwakikagile yuko wapi wala anafanya nini hivi sasa.Kuna mtu anafahamu hilo?
Nikiwa bado mwenye mawazo tele,napata ahueni kusoma kwamba mwanablogu mwenzetu,Ndesanjo Macha,amepata tuzo kutoka kwa jirani zetu Wakenya. Hili linanitia moyo na kuamini kwamba tunachokiandika hapa sio bure,ujumbe unawafikia wengi na mapinduzi yapo njiani. Watanzania huwa tuna sifa ya kuanza mbio taratibu kabla hatujawapita washindani wengine kwa kasi ya ajabu. Nikiwaita wakenya washindani wetu nadhani nitakosea,hivyo nitawaita wakenya wenzetu na jirani zetu.Washindani wetu,daima watabakia kuwa wamagharibi.
Nikiangalia vyombo vya habari vya nyumbani Tanzania vyote vitejaa habari za ujambazi,ushujaa,na kupandishwa vyeo kwa polisi waliohusika. Ni habari ya kusikitisha lakini yenye kutia matumaini kwamba angalau safari hii tuna raisi ambaye anajitahidi kuwa karibu na wananchi. Angalau anatambua kwamba kuwa raisi haimaanishi kuunguza mwili na suti masaa 24!
Mwezi ujao tarehe tatu kuna majadiliano kuhusu kitabu cha Mwakikagile kuhusu mahusiano ya waafrika wamarekani na waafrika. Mwenye wasaa anaweza kusikiliza majadiliano hayo mtandaoni. Tangazo la mjadala huo hili hapa:
Wednesday, May 3rd, from 6 - 7:30pm EST
TUNE IN VIA INTERNET to the
'Voices from the Drum' (VFTD) Radio Book Club
on WCLM 1450/AM Radio with host, GLORIA TAYLOR EDWARDS
VFTD interviews Professors:
ALBION MENDS and Adisa Alkebulan
Subject: Relations Between Africans and African Americans
Tune in at:
http://www.wclmradio.com/pages/home.html and click on the 'Listen Live' tab.
Details...
Focus: GODFREY MWAKIKAGILE’s book, 'Relations Between Africans and African Americans: Misconceptions, Myths and Realities'.