
Wakati nikiendelea kujifunza, swali au maswali kwamba nini Tanzania inaweza kufanya ili kufanya mapinduzi halisi ya kimaendeleo hayaishi kichwani mwangu. Majibu bado hayatoshelezi kiu ya kujua zaidi.Lakini kwa sababu ninaishi katika nchi inayosemekana kuwa imeendelea huwa napenda pia kujiuliza,wao wamefikaje hapa walipo? Najihisi "mtenda dhambi" kama nitakaa hapa ughaibuni nikala kuku kwa mrija na kusahau kwamba nimekuja hapa kama shushushu wa jamii nikijua wazi kwamba huko nitokako nimeacha wananchi wenzangu wakitaabika kwa sababu zinazoweza kuepukwa.
Ujenzi wa jamii bora sio kazi rahisi. Pia naamini kwamba yapo mengi sana ambayo yanachangia kujenga jamii bora.Leo naomba nitaje mawili ambayo nayaona kuwa dhahiri na tofauti sana kati ya nchi zetu na hapa. Cha ajabu haya hutoyasikia yakipigiwa debe na wanaodai wanataka kuona tukiendelea( IMF,WB,UN,AU na wengineo kwenye mkondo huo).Kodi na kujitolea(tax and volunteerism). Nakumbuka hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba sifa namba moja ya serikali corrupt ni kwamba hazikusanyi kodi!. Nadhani kwa usemi ule alikiri kwamba Tanzania nayo ilikuwa corrupt kwa sababu ukusanyaji kodi wa nchi yetu una mapungufu mengi sana siku zote. Kwa ufupi hatukusanyi kodi kwa umakini na ki-uzalendo unaotakiwa.Lakini pia lazima nikubali kwamba angalau wakati wa utawala wa Bwana Ben tumeanza kufanya hivyo.
Sasa hebu tujiulize,serikali ya Tanzania kwa mfano,itaweza vipi kusukuma mbele maendeleo bila kukusanya kodi ipasavyo? Huduma za jamii zitaboreshwa vipi kama serikali haina fedha ambayo inaweza kupatikana kupitia kodi(serikali hazifanyi biashara siku hizi)? Jibu rahisi ni hakuna jinsi! Kinachofanyika kwenye zoezi la kukusanya kodi ni kwamba sisi kama wananchi tunaipa serikali hela ili iboreshe huduma zote za jamii. Mbadala wa kutokukusanya kodi ni serikali zetu kugeuka ombaomba kwa nchi za magharibi.Madhara na masahiba ya mikopo na misaada kutoka magharibi sote tunaijua hivi sasa. Hapo ndipo pale tunapoongelea suala la ukombozi wa mwafrika ni mwafrika mwenyewe.Tatizo letu kubwa ni kwamba hatuelewi ni kwa namna gani huku tunaowaita viongozi wetu hawana dira wala muelekeo.
Kama umewahi au unafanya kazi nchini Tanzania jiulize ulikuwa au hivi sasa unatozwa kiasi gani cha kodi kutoka kwenye mshahara wako kwenda serikalini katika namna iliyokuwa wazi na inayoeleweka? Utasikia "kodi ya maendeleo" tunakatwa.Lakini takwimu zake ziko wapi na jinsi gani kodi hizo zinatumika?.Kwa wale mlioko nje ya nchi mnajua jinsi gani kodi inavyokusanywa na kukatwa haraka kabla ya mambo mengine yoyote. Je,kodi zinafanya kazi yake?
Sasa nani anakwepa kodi? Jibu ni mimi na wewe kwanza kabla ya kutupa lawama kwa serikali juu ya uzembe wa kukusanya kodi.Unapokataa kulipa VAT na kumkubalia mhindi asikupe risiti ili pasiwe na kodi kisha ukaenda ukatumbukia kwenye mtaro ambao haujatengezwa(kwa kisingizio cha serikali kukosa fedha) unailaumu serikali au unatakiwa ujilaumu wewe mwenyewe? Wangapi wanafanya mchezo huu bila kujua kwamba ndio wanazidi kuitumbukiza nchi kwenye shimo? Kama watu wakibadili tabia na kuanza kutambua umuhimu wa kodi kwa maendeleo yao hapo ndipo tunapoweza kuanza kuwawajibisha viongozi wetu wa serikali kwamba kodi zetu tumewapa na hamna mnachofanya.Kinyume cha hapo kisingizio cha serikali ni kwamba haina pesa na kimsingi hakuna jinsi ya kuweza kuiambia serikali vinginevyo.
Kwa bahati mbaya masuala kama haya yanaonekana kama sio muhimu kutolewa kama mafunzo ya jamii. Kuna ubaya gani wa kuwafundisha watoto mashuleni juu ya masuala ya nchi kama haya? Au basi kama sio mashuleni vipi kwenye jamii zetu? Wangapi wanaelewa mchanganuo wa maendeleo ya wote kupitia kodi?Najua kwamba wengi wetu hawana uwezo wa kulipa kodi.Lakini vipi kuhusu wale wanaoweza kufanya hivyo na hawafanyi? Juzi nimesikia habari za vitambulisho vya wananchi kuanza kutolewa.Huu ni muelekeo sahihi wa baadaye kuweza kujua nani ni nani,anauwezo wa kulipa kodi,analipa au halipi nk.Kinachonishangaza mimi ni kwamba tulikuwa wapi na bado tupo wapi?Nasema hivi kwa sababu zoezi muhimu kama hili bado litachukua miaka mingine kumi kutekelezwa.Mengine ya kujiongezea ruzuku na masilahi hayachukui wiki moja.Kwanini?
Lingine ni kujitolea.Hawa wenzetu wanajitolea sana jamani. Huu ni moyo ambao hatuna budi kuuiga kama tunataka na sisi kupiga hatua.Wangapi kati yetu wanao moyo wa kujitolea na wasiulizie "bei gani"? Matembezi ya wikiendi iliyopita huko Kilimanjaro- Tanzania yaliyolenga katika kuchangisha kusaidia watoto wenye njaa yanaweza kuwa kielelezo tosha kwamba kujitolea ni jambo moja ambalo linaweza kutusogeza mbele. Mamilioni ya pesa yalichangishwa,hili linaonyesha kwamba pesa zipo mikononi mwa baadhi ya wananchi na wengi wao wana moyo wa kusaidia wenzao.Wakihimizwa na kuongozwa na viongozi makini wanaweza kusaidia wenzao. Niishie hapa kwa leo. Pichani ni polisi na zima moto wa jiji la Ottawa hapa Canada wakiwa kazini. Huduma hizi hutegemea kodi za wananchi.Hapo palitokea moshi kidogo tu kwenye mgahawa wa pembeni wakaja wote hao!
jeff suala la kodi ni sawa na rushwa. Tunatakiwa kujiuliza ni mra ngapi tumetoa rushwa na kisha kununua haki yetu kabla hatuajaanza kuwaza kuhusu nani anapokea. Kama tusipoweka mikono mfukoni na kutoa rushwa unadhani mpokeaji ataipata wapi? Kodi tunakwepa sisi na kisha tunaanza kulalamika, ni bora kuzungumzia ukubwa wa kodi hizo katika vitu vya huduma za msingi kwa jamii kuliko kuzikacha. Huwezi kuwa na nafasi ya kuiambia serikali kushindwa kukusanya kodi wakati ni wewe unayekacha. Ni kweli Jeff wangapi tumejiuliza baada ya mwaka kuisha kuwa tumelipa kisi gani cha kodi? Sijawahi kufanya hivi hii makala yako ya 100 imenipa mtihani hasa wa kujihoji. Tuendelee kupata habari hizi ili tujenge taswira chanya ya fikra na matendo yetu.