
Kwa wasomaji wa kudumu wa blogu yangu jina Adam Solomon(pichani) litakuwa sio geni. Huyu ni mwanamuziki,mzaliwa wa Mombasa,Kenya mwenye makazi ya kudumu hapa Toronto,Canada. Ni mshindi wa tuzo yenye heshima ya aina yake hapa Canada katika masuala ya muziki na raha ijulikanayo kama Junno Music Awards.
Adam Solomon hafanyi shughuli za muziki huu peke yake bali hushirikiana na bendi yake nzima ili kuunda kile kinachojulikana kama Adam Solomon & The Tikisa Band.
Wiki moja iliyopita Adam Solomon & The Tikisa Band walizindua albamu yao ijulikanayo kama Mti wa Maisha (aka Tree of Life). Uzinduzi huo uliokuwa wa kufana na wa aina yake ulifanyika katika ukumbi ujulikanao kama Lula Lounge. Huu ni ukumbi maarufu sana hapa Toronto hususani kwa wanamuziki kutoka nje ya Canada na pia wale waishio hapa Canada lakini wenye muziki uliojaa vionjo kutoka nje ya magharibi hii. Kama kuna mwanamuziki yeyote mkubwa kutokea bara la Afrika, kwa mfano, ambaye ameshawahi kufanya ziara ya kimuziki hapa Toronto basi uwezekano wa kwamba alifanya maonyesho yake Lula Lounge ni mkubwa sana.
Niliwasili kwenye ukumbi mapema iwezekanavyo kwa sababu nilijua kwa jinsi ambavyo Adam Solomon & The Tikisa Band wamejitengenezea jina hapa Toronto basi kuchelewa kungemaanisha kutokupata sehemu nzuri ya kukaa kwani licha ya kwamba nilitaka kupata picha za uhakika,nilitaka pia kucheza muziki,kubwaga moyo na kula raha.
Jambo moja ambalo lilikuwa wazi ni kwamba wazungu wanaupenda muziki wetu kuliko sisi wenyewe. Hili niliweza kuligundua tena kwa kutizama tu ramani na sura zilizokuwa ukumbini.Huu ni utumwa wa akili ambao sidhani kama nitakuja choka kuukemea. Muziki wa Adam Solomon & The Tikisa Band umejaa vionjo vya kwetu. Walichoweza kufanya watu hawa sio tu kutumia zaidi lugha yetu ya Kiswahili bali kuchukua midundo na vionjo kibao kutokea nchi zote za maziwa makuu ya Afrika. Hili ndilo linalonifanya niuuite muziki wa kwetu kwa maana halisi ya muziki wa kwetu.
Wakati nikijiweka sawa ndani ya ukumbi haikuchukua muda ukumbi ukawa umejaa. Nikapata watu ninaowafahamu,tukaanza kubadilishana mawazo huku tukiteremsha mvinyo tukishuhudia ukumbi ukizidi kufurika watu wa rika zote.
Walipopanda jukwaani siku ilianza kuwa ya aina yake.Masikioni nilianza kujihisi nimekaa pale DDC Kariakoo nikisakata rumba la Sikinde. Macho yalishuhudia wazungu wakijirusha, wakicheza kujaribu kwenda sambamba na mirindimo ya kiafrika. Kwa habari zaidi za Adam Solomon & The Tikisa Band nenda hapa.
Utaalamu wa kukung'uta gitaa,mpangilio wa ala zote za muziki,sauti katika uimbaji, kuruka majoka kwenye steji na mpangilio wa taa za ukumbi huu wa Lula Lounge ni mambo ambayo yalitosha kukonga nyoyo za watu tuliohudhuria uzinduzi huu.Kulikuwa na kila aina ya raha na sababu ya kutosha kuona mwana afrika mwenzetu anasimama kikweli kwenye jukwaa la muziki wa kimataifa. Bado ninakumbuka jinsi alivyoweza kuurudia kwa umahiri ule muziki wa Kenya wenye mashairi ya "Jambo,jambo bwana,habari gani,wakaribishwa Kenya yetu" nk.Naupenda muziki halisi wa Afrika na huu utabakia kuwa mmojawapo wa uzinduzi wa albamu ya muziki huo ambao nitaukumbuka kwa miaka mingi.
Jeff,
Huwezi amini! Kwamba leo hii nimechomoa CD ya African Guitar Summit ambapo nilikuwa nasikiliza nyimbo namba saba Pesa ni Ufunguo, iliyotungwa na Adam Solomon. Nilipotoa CD African Guitar Summit nikaingiza ya CD ya Les wanyika Amigo ambapo niliirudia nyimbo ya Sina Makosa mara mbili ili nisikilize vizuri mipigo ya drums ambayo iliyopigwa na William Muhina au Juma Iddi Mikulandi.
Wakati nasikiliza hizi cd nikakumbuka picha aliyoweka Michuzi ya pale Leaders Club kila Jumapili wanapopiga Twanga Pepeta. Nikajisemea moyoni kwamba ni lazima niwasiliane na jamaa zangu Dar ili kwamba tuanzishe klabu ya miziki ya kikweli haswa miziki kama ya Wanyika, Nuta Jazz, Afrosa, Safari Trippers, Dar Jazz, Jamhuri Jazz, Ochestra Makassi, Marquis du Zaire, Matimila, nk.
Kwa ufupi tu, mimi ni mwanaharakati wa miziki ya Kiafrika na huku ughaibuni nilipo huwa natayarisha madisko ya miziki ya kinyumbani. Ijumaa ijayo nitamwaga vumbi kwenye Klabu ya Dubrovnik (ukigoogle 'afro fusion dubrovnik' utaona matangazo yangu). Katika harakati zangu hizi nategemea kuingiza muziki wa Kiafrika katika main stream music scene ya huku nilipo. Inshaallah mambo yakienda kama ninavyotarajia mwezi wa sita au wa saba nitakuwa napiga disko la Kiafrika katikati ya jiji.
Yote tisa umenichengua kumkuta Adam Solomoni ukumbini.
F MtiMkubwa Tungaraza.