
Wakati viongozi wa dunia wanakutana New York,Marekani yapo machache ambayo yananivutia. Kubwa ni hotuba ya raisi wa Iran Mahmoud Ahmadinejad kuhusu anachokiamini,kinachofanyika nchini mwake kuhusiana na tekinolojia ya nyuklia na jinsi ambavyo anaelezea ubabe wa nchi za magharibi. Unaweza isoma hutuba yake kamili kwa kubonyeza hapa.
Bado nasubiri kusikia atakachokisema(pengine ninavyoandika ashasema) raisi wa Tanzania-JK. Mpaka leo sijaweza kupata hasa msimamo wa raisi wangu. Nadhani hili linatokana na wingi wa siasa katika maneno yake. JK hapendi kuudhi mtu,anapenda kupendwa na kusifiwa tu. Ukimuuliza swali atakujibu unachotaka kusikia.Alichokisema huko Havana-Cuba siku chache zilizopita kilionekana kuwa cha maana. Lakini umaana huo unapotoshwa kabisa unapoona kutoka Havana alikimbilia Washington kuonana,kusabahiana,kunywa kahawa na kujikomba kwa raisi George Bush wa Marekani ambaye kimsingi nchi yake ndio adui mkubwa wa nchi zinazosema hazifungamani na upande wowote. Sishabikii viongozi wa dunia kuonyeshana ubabe kila mara ila nadhani kuna wakati maneno ya majukwaani lazima yaendane na vitendo. Msimamo wetu,wa raisi,au nchi yetu ni upi hasa? Nadhani lazima tufikie mahali tueleweke. Tutaheshimika zaidi namna hiyo. Political prostitution sio sifa nzuri hata kidogo.
Yote hayo tisa. Miezi michache iliyopita sinema ya Darwin's Nightmare ilizua janga huko Tanzania. Wimbo wetu wa taifa ukawa "mapanki". Wanasiasa kupitia bunge wakatuonyesha rangi zao halisi juu ya nini wanakijua,nini wanakizingatia nk. Wapiga kelele kama mimi tukaandika. Ukitaka kusoma nilichoandika bonyeza hapa.
Sasa majuzi nimetumiwa sinema nyingine. Hii ni kuhusu child labour. Imepigwa kule Mererani,kule kule yanakochimbwa madini adimu ambayo serikali yetu imeshindwa kabisa kuyaona kama urithi wa kipekee wa nchi yetu. Najaribu kujiuliza,je safari hii raisi wetu atasema nini? Wabunge wetu watasema nini? Unaweza kuitazama sinema yenyewe kwa kubonyeza hapa. Pia unaweza kusoma ripoti ya jamaa wa IRINnews kwa kubonyeza hapa.
Picha ya juu kwa niaba ya Michuzi wa www.issamichuzi.blogspot.com. Pichani ni vijana wa Mererani wakisaka Tanzanite. Huko ndiko child labor inapozidi kuota mizizi.
Jeff waweza msoma hapa http://www.un.org/webcast/ga/61/pdfs/tanzania-e.pdf
Kwa ujumla utahukumu mwenyewe mimi sina comment