VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Wednesday, October 11, 2006
MUZIKI WA KIZAZI KIPYA, UZALENDO, UTUMWA MPYA

Hapa chini ni makala niliyowahi kuandika siku za nyuma juu ya muziki wa kizazi kipya.Mmojawapo wa wasomaji wangu aliniomba nijadili suala hili. Kwa sababu suala hili lilishawahi kujadiliwa na mimi kuliandika nimeona ni bora kuiweka hapa makala nzima.

Siku chache za nyuma niliandika juu ya kuchipuka kwa umaarufu wa muziki wa kizazi kipya. Pia niliandika kuhusu umuhimu wa kuunga mkono muziki huu unaoitwa wa kizazi kipya ama Bongo Flava. Kilio changu kilikuwa tuwaunge mkono wanamuziki hawa wa kizazi kipya kwa sababu sio tu kwamba wanatuburudisha bali pia wanatupa utamaduni mpya kupitia muziki. Kiufupi tunakuwa na chetu wenyewe ingawa kimsingi tumeiga kutoka kwenye utamaduni wa muziki wa hip hop ambao ni maarufu sana Marekani miongoni mwa jamii ya watu weusi(black Americans au African-Americans).

Nilitoa ombi kwa watu kununua cds au kaseti halali na kuachana na ule mchezo wa kurekodi ovyo ovyo bila kuzingatia jasho la msanii.Hapa ningeweza kuwaunganisha na wale wezi wa kazi za wanablogu bila idhini yao.Hoja yangu ilikuwa kama tunataka muziki huu uendelee na pengine baadaye kuwa kitambulisho cha vijana wetu duniani kote basi lazima tuunge mkono ili ukue.Njia pekee ya kuweza kufanikisha hilo ni kununua kazi halali za wasanii hao. Sina uhakika kama ombi langu lilisikika au la.

Baada ya hapo nikabakia kuwa mpenzi na mnunuzi mkubwa wa muziki huo. Ingawa mpaka hivi sasa nabakia kuwa mnazi wa muziki huu nakatishwa tamaa na jinsi wasanii wenyewe wanavyotaka kuutangaza muziki huu. Ninashindwa kabisa kuelewa kwamba kwanini muziki huo unazidi kuonekana wa kimarekani siku baada ya siku? Matumaini ya kwamba siku moja muziki huu utakuwa kitambulisho chetu kipya cha vijana wetu,sanaa zetu, tamaduni zetu nk yanakuwa finyu siku baada ya siku.

Majuzi nimeletewa baadhi ya dvd za muziki huo.Jambo moja ambalo lilikuwa wazi kabisa ni kwamba kila mmoja anajaribu kuiga utamaduni wa mtu mweusi wa marekani kwa udi na uvumba.Nimeona katika hizi video watu wamevaa vilemba( tena vya bendera ya Marekani!) hereni ,wamesuka,wakavaa masuruali makubwa makubwa,wakaghani kama vile kina 50 Cent,kina Jay Z nk. Kitambulisho kwa muziki huu unatokea Tanzania hakipo kabisa! Nimejaribu kuwaonyesha watu mbalimbali video hizi na kila mmoja anaponirudishia kaseti zangu ananiambia suala moja.Ingependeza zaidi kama wasingekuwa wanajaribu kuiga utamaduni wa kimarekani. Ni dhahiri kwamba kila mtu analiona hilo na halitii mvuto wowote kwa kweli.

Natambua kwamba zimekuwepo hoja kama upi basi ni utamaduni wa mtanzania? Swali hili linapoulizwa mimi huwa na masuala mawili kichwani kwangu.Moja kama una umri zaidi ya miaka 20 kwa mfano na bado hujui utamaduni wako kama mtanzania basi pana tatizo kubwa. Pili huwa nasikitika, nakumbuka hoja aliyowahi kuitoa Mwalimu Nyerere juu ya dhambi kubwa kupita zote walizofanya wakoloni, ya kutuambia tamaduni zetu hazifai, tusitupe jalalani. Kumbe basi tamaduni zetu zipo,zilikuwepo na tunaweza kuziendeleza kama tukitaka huku tukiziboresha.

Nimejaribu kutafuta kama kuna mwanamuziki wa kizazi kipya anayeendana na utamaduni wa kiafrika bila mafanikio.Nia ilikuwa ni kualika mwanamuziki kutoka Tanzania kwa ajili ya Tamasha la kila mwaka hapa Toronto linaloitwa AfroFest. Sasa nitaanzia wapi kama kila nimuonaye anajifanya mmarekani kuliko hata wamarekani wenyewe? Hivi kweli kuna maana yoyote kumleta mpaka hapa mwanamuziki kutoka Afrika ya Mashariki kisha akuonyeshe jinsi gani alivyo mahiri wa kumuiga Jay Z,50 Cent,Lil’ John nk? Ungekuwa wewe ungefanyaje? Najua wapo wanamuziki wanaondamana na utamaduni wa kitanzania au kiafrika,sijapata mawasiliano nao.Kama unayo tafadhali nipatie.

Ukweli ni kwamba kama wanamuziki wetu wanataka kuuza kimataifa basi ni lazima wajifunze utamaduni mpya.Tuliiga mtiririko wenyewe wa hip hop,sio lazima tuige mavazi na video zao.Kwa mtaji huu hamna mzungu au mmarekani atakayetaka kununua muziki wetu.Kwanini anunue wakati anapata kitu hicho hicho,kwa lugha yake na kwa bei nafuu zaidi kama anataka muziki wa aina hiyo? Lazima wanamuziki wetu wawe wabunifu.Kuiga kidogo sio mbaya lakini hili mnalofanya hivi sasa halitowafikisha mahali popote.Ila kama nia yako ni kuendelea kupata jina kubwa wakati huna senti mfukoni basi endelea na utaratibu wako wa kuwa mtumwa wa kiakili na kimtazamo.

Najua kuna huu utamaduni wa watu weupe siku zote kupenda kutuona sisi waafrika tumevaa majani,ngozi za wanyama tukikata viuno na kuona huo ndio utamu wenyewe.Sina hakika kama sisi wenyewe tunapenda kuonekana hivyo. Lakini kama hatupendi basi hatuna budi kuboresha muziki wetu kwa kubuni na kujivunia mavazi yetu,(sio ngozi na majani) miondoko yetu nk. Hapo ndio muziki wetu na wanamuziki wenyewe wataingia kwenye ulimwengu wa muziki kimataifa.

Nimewahi kusoma kwenye magazeti na mitandao mbalimbali inayowapa sifa hewa watanzania kwamba hivi sasa mwanamuziki fulani anakuwa wa kimataifa kwa sababu amealikwa kufanya maonyesho Marekani,Canada,Uingereza nk. Kwangu mimi kama unakuja hapa kutumbuiza watanzania waishio hapa basi wewe bado sio wa kimataifa. Utakuwa wa kimataifa pale muziki wako utakapouzika kwa watu wa jamii na tamaduni zingine,pale utakapopanda jukwaani kutumbuiza mashabiki wa tamaduni mchanganyiko. Kuna umataifa gani kuja kunitumbuiza mimi na rafiki zangu tuishio hapa Toronto? Kupanda ndege ndio umataifa ndugu zangu?

Hivi kuna ugumu gani wa mwanamuziki fulani wa bongo flava kuamua kuvaa mavazi ya kiafrika tu?Mbona yanapendeza na kukubalika dunia nzima? Hapa Canada mavazi ya kiafrika ni ghali kuliko nguo za aina zote. Unaona sifa gani kuvaa nguo iliyoandikwa Toronto,New York,Washington nk wakati hujawahi hata kufika sehemu hizo? Hivi ukionekana na nguo iliyoandikwa Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa,Arusha nk ni ushamba?

Utumwa wa akili huanzia hapo.Unapoona kwamba chako sio bora bali cha mwenzio.Unapoona kila kizuri ni cha mzungu. Jogoo lililonona ni la mzungu,kuku mweupe ni wa kizungu,nyumba nzuri ni ya kizungu nk. Kama huthamini mavazi yaliyotengenezwa nyumbani kwetu Tanzania kwa kuyanunua na kuyavaa,kama huthamini bidhaa za kwetu,kama huthamini mazao ya kwetu unalalamika nini kuona hali ya uchumi inazidi kuwa mbaya? Kwanini unaenda kununua machungwa yaliyotoka Afrika ya Kusini wakati yale ya Lushoto ni bora zaidi? Unadhani nani anastahili lawama katika hili; raisi, serikali au mwananchi?

Wenzetu wa Afrika ya magharibi wanaheshimika kwa kushikilia tamaduni zao ingawa sio wote wafanyao hivyo. Mavazi yao yanathaminiwa dunia nzima. Upuuzi huu wa kutothamini mavazi fulani ndio hupelekea siku nyingine ukialikwa kwenye tafrija fulani unaambiwa kwamba vazi rasmi ni suti nyeusi.Kataa! Shati la kitenge au wax sio nguo?Usikubali kuwa mtumwa wa kiakili ndugu yangu.Jivunie chako.

Picha nadhani zinajieleza zenyewe.Hao vijana mbele ya bendera ni watanzania?
NB.Naendelea kujifunza masuala ya photoshop. Mwalimu wangu ni Scout wa http://harper-valley.blogspot.com/
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:55 AM | Permalink |


Maoni: 3


  • Tarehe: 12:07:00 PM, Mtoa Maoni:- Anonymous Anonymous

    Kweli,kweli,kweli,kweli tupu Jeff.Nimeipenda sana makala hii.Big up

     
  • Tarehe: 2:18:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger Mjengwa

    Jeff! Hii makala imetulia, inaelimisha. Hongera!

     
  • Tarehe: 7:06:00 PM, Mtoa Maoni:- Blogger Jeff Msangi

    Ahsante Maggid,
    Naamini kwamba mijadala kama hii,japo ni migumu,haina budi kuwekwa vibarazani mara kwa mara.Tuendelee.

     
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker