

Naomba nianze kwa kukutakia kheri ya mwaka mpya. Kwa takribani wiki tatu nilijaribu kukaa mbali na mtandao ili kupumzisha akili,kutafakari yaliyojiri mwaka tulioupa kisogo hivi majuzi na kupanga mikakati mipya ya 2007 kama ikibidi. Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu sijaweka malengo maalumu.Nataka uwe mwaka shaghalabaghala kama itawezekana.Wewe unasemaje? Lakini jambo moja ambalo nipende nisipende tayari lipo kwenye malengo
na ajenda za mwaka huu ni suala la
kuendelea kublog.
Wakati wa kufunga mwaka nilitembelea kwa Joji Kichaka kama ambavyo Ndesanjo hupenda kumuita. Katika pita pita zangu nilitembelea mojawapo ya ile "miji shoka" ambayo mingi imegeuka kuwa namna ilivyo baada ya kuhamwa na watu weupe. Historia ndio inayosema hivyo,sio mimi.Kuhamwa huko kulipewa jina "white flight" ikimaanisha wazungu kuhama na kuwaacha weusi waendelee kukaa wenyewe katika miji yao.Kilichochangia sana ni ubaguzi wa rangi ambao mpaka hivi leo ungali upo na pengine utaendelea kuwepo milele.Wachumi wanasema sababu za kiuchumi ndio zilizochangia "white flight".
Jiji la Gary(mpaka hivi sasa sielewi nini kinasababisha sehemu moja kuitwa jiji na nyingine kuitwa mji au kijiji) lipo katika jimbo la Indiana mpakani kabisa na jimbo la Illinois lenye jiji maarufu la Chicago ambapo mwanamama Oprah Winfrey huendesha shughuli zake. Nia yangu ya kutembelea Gary,Indiana ilikuwa kuanzisha kasumba ya kutembelea kule wanakoishi "wenzetu" na kuachana na kasumba ya kutembelea majiji makubwa peke yake( yale ambayo wenyewe hupenda kuyaonyesha kwenye sinema zao na kurubuni wengi duniani kwamba Marekani ndivyo inavyomeremeta).Pia nilitaka kuona mahali mwanamuziki maarufu wa muziki wa pop Michael Jackson na ndugu zake kina Janet Jackson,Tito Jackson,LaToya Jackson, Marlon Jackson,Randy Jackson,Jackie Jackson na Rebbie Jackson walizaliwa na kuanzia maisha yao ya uanamuziki.
Pichani juu ni nyumba walimozaliwa nyota hao wa muziki ambapo baadaye kaka yao Michael Jackson alikuja kuwa na umaarufu wa aina yake wenye mchanganyiko wa mambo chungu tele. Tofauti na nyumba zingine zilizopo katika jiji la Gary nyumba walimozaliwa nyota hao wa muziki inaonekana kuwa safi,inayotunzwa na ina hata majani ya kupandikiza. Sababu ni kwamba familia ya wanamuziki hao imeamua kuitunza nyumba hiyo kwa ajili ya kumbukumbu (souvenir ) kama ilivyokuwa enzi hizo.Hivi sasa kuna mpangaji anayeishi humo.Nyumba hiyo iko katika kijimtaa kidogo ambacho kwa heshima ya familia ya Jacksons nacho kinaitwa Jackson Street. Mwaka uliopita(2006) jiji la Gary lilitimiza miaka 100 na hivyo kuchukua jina la jiji la karne!
Jambo ambalo litakushtua ukifika Gary,Indiana ni hali ya maisha,uchakavu wa majengo,vichaka,uchafu na kila aina ya takataka za dunia hii. Picha ya pili hapo juu ni mfano wa nyumba nyingi nilizoziona. Nyumba hiyo ni makazi ya mtu ndani ya Marekani.Ilikuwa vigumu kwangu kuamini kwamba hii ndio Marekani ambayo inatumia mabilioni ya dola kupigana vita inavyojua kabisa kwamba kamwe haitaweza kuvimaliza bila kurekebisha sera muhimu za ndani na nje.Hii ndio nchi ambayo viongozi wake wanajifanya hawaoni umasikini na uharamia unaojiri nyumbani na hivyo kuyafumbia kabisa macho masuala hayo.Nilichokiona mimi ni kama uwanja wa vita au jamii ambayo imehamwa baada ya mapigano ya muda mrefu. Hapana,nilikuwa nimekosea; hapo ni Gary,Indiana jiji lenye wakazi zaidi ya laki moja na nusu. Damu ilikuwa inasisimka huku vinyweleo vikisimama kila mara.Au ni uoga wangu tu?
Kama nilivyoeleza hapo juu,jiji la Gary ni mojawapo ya majiji mengi ya Marekani ambayo yalikumbwa na "white flight", mengine ni kama vile Philadelphia, Atlanta, Houston, Miami, Cleveland, Boston, Detroit, Memphis, St.Loius, Milwaukee, New Orleans(Katrina), Magharibi na Kusini mwa jiji la Chicago, maeneo kama Bronx, Oueens(Coming to America), Brooklyn na kwingineko. Kitakwimu (wakati mwingine sipendi kuziamini) miji kama hiyo niliyoitaja hapo juu inaongoza kwa kuwa na ghasia,mauaji na gharika chungu mbovu za kijamii. Kwanini ni swali gumu kujiuliza lakini muhimu. Hivi sisi weusi hatuwezi bila wazungu? Nini kilitokea katika historia ya binadamu,historia yetu? Kuna mkono wa mtu?
Mwishoni swali la kwamba kwanini Marekani haisaidii wananchi wake kama hawa wa Gary,Indiana jiji ambalo kila mara limo kwenye orodha ya miji hatari kupita yote nchini Marekani, inahangaika kuihadaa dunia kwamba inapeleka maendeleo na demokrasia duniani? Hivi ni kweli kwamba zipo Marekani mbili tofauti kabisa ndani ya Marekani tunayoijua sisi?Tuendelee kublog,2007 ndio hiyo.
Jeff, msikilize John Edwards (aliyekuwa mgombea mwenza wa Kerry uchaguzi uliopita) ambaye ametangaza kugombea urais. John Edwards (ambaye yeye na mke wake ni wanablogu) amekuja safari hii na ujumbe mmoja mzito: Marekani mbili. Ulichozungumzia hapa ndicho anachoongelea huyu bwana. Anasema ndio ugonjwa mkuu wa Marekani. Nchi hii ni sawa na nchi mbili. Nchi ya wachache ambao maisha yao yanadhaniwa kuwa yanawakilisha maisha ya Wamarekani wote. Na wamarekani wengi ambao, ingawa unaweza kuona wana magari na wanaishi ndani ya nyumba, wanaandamwa na madeni hadi mvunguni. Jamaa mmoja aliyekuwa jirani yangu hivi sasa kawa ombaomba. Aliachishwa kazi, akawa anaumwa, mwenye nyumba hakusikia kitu anachotaka ni fedha yake. Akamletea polisi, huyo akatolewa nje. Sasa anaombaomba huku akitafuta kazi!
Ndio ulichosema hapo. Kuna nchi mbili Marekani. Pengine tatu. Ndio mabilioni hayo yanatumika "kueneza demokrasia" (demokrasia ya kuua kwa kamba ya katani kama vile tunaishi karne ya kwanza) kule Iraki.
Mkongo mmoja rafiki yangu alikuwa akisema Marekani ni sawa na barabara ya lami. Unapoendesha gari kwenye barabara ya lami wakati wa jua kali unaona kama barabarani mbele yako kuna maji. Ukifika hapo panapoonekana kama pana maji unakuta hakuna kitu. Kwa lugha yao wanaita "mirage." Ndio Marekani hiyo yenye Gary, Indiana na miji mingine ambayo wanaishi akina Cheney na wezi wenzake na vibosile vya makampuni makubwa yanayohonga wawakilishi hapa ili kusipitishwe sheria ya kima cha chini.