Tuesday, March 13, 2007
BARIDI INAPOANZA KUPUNGUA.......
Hali ya hewa ni habari kubwa sana katika hizi nchi za magharibi.Kuna watu ambao hutazama luninga ili tu kupata utabiri wa hali ya hewa!Siku hizi hata mimi hujishtukia nikizingatia kwa makini utabiri wa hali ya hewa tofauti na nilivyokuwa kwetu.Sina uhakika kama huu ndio ule utaratibu wa "ukikuta wenzio ni chongo na wewe fumba jicho moja" au la!Usishangae sana basi kuona kwamba mara kwa mara nimekuwa nikikuhabarisha au kukuletea picha za hali ya hewa kutoka hapa.Nilipokuwa Tanzania jamaa wa hali ya hewa walikuwa wakishaanza utabiri wao baada ya taarifa ya habari ungetarajia mambo mawili yatokee;nizime televisheni au nibadili channel.Inawezekana kwa sababu hadithi yao kila siku ilikuwa ni ile ile..."kanda za juu kusini mvua za hapa na pale, mikoa ya Dar-es-salaam,Pwani,Morogoro itapata mawingu na mvua za rasha rasha".Tofauti na kwetu ambapo masuala ya hali ya hewa huwekwa mwishoni hapa wakati mwingine(kama sio mwingi) hali ya hewa huwa ndio "breaking news".Huwa inatokea jamaa wakautisha umma mzima na wala hali ya hewa isiwe mbaya kama walivyosema.Bahati nzuri au mbaya ni kwamba utabiri wa hali ya hewa ni mojawapo ya taaluma chache sana duniani ambapo mtu anaweza kukosea na wala asiwajibike kwa yeyote.Hivi sasa baridi imeanza kupungua.Majira ya baridi kali ndio yanayoyoma ili kupisha masika za huku kabla ya kuyakaribisha majira ya joto (summer). Jambo moja la aina yake huku ughaibuni ni jinsi maduka yanavyobadili bidhaa kuendana na majira yaliyopo. Hivi sasa ukienda madukani karibuni kila kitu cha kusaidia kupambana na baridi kama masweta,makoti nk vishaondolewa kwenye shelves. Msimu mpya vitu vipya.Hii ni tofauti kabisa na kwetu ambapo bidhaa nyingi hudunda dukani miaka nenda,miaka rudi mpaka atokee atakayezinunua. Hapa nakumbuka jinsi lile duka la "mangi" pale mtaani kwetu lilivyosheheni bidhaa hususani alipoacha kutukopesha! Pichani juu ni mall kubwa ijulikanayo kama Eaton Centre iliyopo jijini Toronto ambayo huhesabika kama mojawapo ya vivutio vikubwa vya utalii.Huko ndipo wengi wanapoelekea ili kujiandaa kwa majira yanayokuja.Kazi kweli kweli.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:42 AM
|
Permalink |
-
Hatimaye winter inaaga, tupumzike kupambana na barafu na kujigubika makoti mazitomazito!
Hatimaye winter inaaga, tupumzike kupambana na barafu na kujigubika makoti mazitomazito!