Wednesday, March 28, 2007
MUGABE NI DIKTETA?
Natizama nje kupitia dirisha langu ili kupata mandhari ya nje katika asubuhi hii inayoelekea kuwa na kila aina ya wema. Jua la asubuhi linaangaza kuashiria hali bora ya hewa katika kipindi hiki cha mvua hapa Canada. Mkononi nimeshikilia kikombe cha chai ili kuchangamsha kinywa kabla ya kuingia katikati ya jiji kutafuta. Nimefungulia luninga kwa sauti kubwa ili niweze kusikia taarifa za habari za asubuhi. Huwa napenda kusikiliza taarifa za habari ingawa najua mara nyingi huwa zimejaa ghadhabu na chumvi nyingi zenye kuvunja moyo. Leo sina bahati,nasikia wakimuongelea Robert Mugabe, hawasiti kabisa kumwita "Dikteta Robert Mugabe".Hivi kumbe...alah!
Ghafla najishtukia nikijiuliza swali lililopo kwenye kichwa cha habari hapo juu.Swali hili linazidi kuniwia gumu kulipatia jibu/majibu siku baada ya siku.Ugumu ninaoupata ninapojaribu kujibu swali hili nashindwa kuutofautisha na ule nilioupata nilipowahi kujiuliza kuhusu tofauti kati ya mpigania haki na uhuru na gaidi (terrorist). Eti Mandela alikuwa gaidi au mpigania uhuru alipokuwa na vijana wake wa Umkotho we Sizwe? Maswali kama haya yapo mengi sana,yote yanachosha na kuhemesha akili vibaya mno. Hivi Mugabe ni dikteta? Mbona kachaguliwa kwa kupitia sanduku la kura?
Mambo yanayoendelea nchini Zimbabwe hayapendezi hata kidogo.Lakini swali kubwa ni je yanatendeka Zimbabwe peke yake?Chaguzi zinazosemekana kutokuwa huru zinatokea Zimbabwe peke yake? Kwani hatukumbuki jinsi George Bush alivyoingia madarakani? Makamu wa raisi wa Bill Clinton, Al Gore siku hizi akijitambulisha anasema "I am Al Gore,I used to be the next president of the United States", unadhani anatania? Kama jibu ni hapana (naamini) tunao madikteta wangapi barani Afrika au duniani kote? Unadhani orodha hii ni timilifu? Ni nchi ngapi duniani zinazokandamiza upinzani kwa kutumia nguvu za dola za kila aina? Hivi ni nchi ngapi duniani zinazokandamiza uhuru wa kujielezea? Viongozi wangapi duniani wanaburuza tu wananchi na maamuzi yanayoumiza na hata kuua wananchi wao chungu tele?
Tunapochambua suala la udikteta viongozi kama George Bush tutawatofautishaje na kina Robert Mugabe? Kinachofanyika nchini Iraq ni ulimbwende? Wangapi tunakumbuka uongozi wa watu kama Marget Thatcher ulivyokuwa umetanda lawama? Jambo moja lililo wazi ni kwamba jamaa wa magharibi hususani Uingereza hawampendi kabisa Robert Mugabe. Ukiisoma vizuri historia ya Zimbabwe unaweza kutambua ni kwanini mambo yapo hivyo yalivyo. Usishangae basi kuona kwamba viongozi/madikteta wengi waliopo kwenye orodha kama hii hawatokei katika nchi za magharibi. Tafadhali naomba maoni yako. Unadhani haki inatendeka kwa ndugu zetu wa Zimbabwe kupitia propaganda za vyombo vya habari?Labels: Zimbabwe
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:31 AM
|
Permalink |
-
mugabe ana mapungufu fulani katika jinsi anavyotatua matatizo ya sasa nchini Zimbabwe,hata hivyo hayuko karibu kabisa na udikteta.tatizo lilopo duniani ni kwamba katika ngazi ya kimataifa kuna anarchy na mataifa fulani yanatumia mwanya huu kujinyakulia mamlaka ya kuamua mambo katika ngazi ya kimataifa.hapo ndio uwaita wale wanaofanya maamuzi kinyume na matakwa majina mbalimbali ya ajabuajabu ili tu kuvuta hisia za watu waungane nao katika kuwashinikiza juu masuala mbalimbali.ninashangazwa sana jinsi viongozi wa upinzani zimbabwe wanavyolichukulia swala zima!mataifa ya magharibi hayapiganii haki bali maslahi yao,ingekuwa wanapigania haki wangeweza kuona kuwa tatizo la kisiasa zanzibar ni kubwa zaidi ya ghasia za zimbabwe,nani amewahi kuzungumzia zanzibar kwenye vikao vya kimataifa?wanaishia kutoa tamko tu kuwa hawakuridhishwa na jinsi uchaguzi ulivyofanyika!
-
Maoni yako ni mazito na hayapishani hata kidogo na niliyonayo kichwani mwangu. Lakini kinachotokea ni ubavu mkubwa wa vyombo vyao vya habari vinavyotandaza propaganda wanazotaka. Hili ndilo tatizo kubwa sana. Kila pembe ya Afrika hukosi kuona au kusikia matangazo ya vyombo vyao vinavyoaminika sana, mfano CNN, BBC au VOA, Fox News, Sky News, DWTV na vingine. Huu ndio utumwa unaotusumbua, kibaya zaidi vyombo hivyo vinaaminika sana. Na ndivyo vinavyoeneza propaganda hizo ulizozisema na kuzijengea hoja na kutupandikiza mbegu zao!
Kwa hiyo wametuzingira na wanatusemea kuhusu viongozi wetu na wanatulazimisha kukubaliana nao na kupitia hivyo, wanang'oa na kuwapachika wanaowataka au wanaokubaliana na misimamo yao.
Mimi sijui kwenye televisheni zetu kuna siri gani, kwa mfano ITV ya Tanzania inatumia masaa chungu nzima ya usiku wa manane, asubuhi hadi mchana kurusha matangazo ya CNN na BBC lakini inatumia muda wa nusu saa tu kurusha taarifa ya habari ya kituo cha televisheni cha SABC AFRIKA cha mjini Johannesburg ambacho hutangaza mambo yetu Afrika. Sijui kuna siri gani kwenye hizi televisheni zetu.
Mugabe si Dikteta ila yanayotangazwa Zimbabwe ni upande mmoja tu wa tatizo lenyewe. Nani atutangazie upande wa pili?
-
Tofauti kubwa kati ya Mugabe na Idd Amin ni kuwa Mugabe amekwenda shule.
-
Kwa mtazamo wangu naona yote yashasemwa lakini mimi sioni kwanini Mugabe haachii madaraka.Naamini kuna mtu mwingine anayeweza kuwaraisi mzuri tu wa Zimbabwe.Naamini pamoja na kupigania maslahi ya Zimbabwe , Mugabe anatumia muda mrefu kujilinda binafsi kitu ambacho nafikiri kinagawa kipaumbele.
-
"Behind every successful man, there is a successful woman". Lazima watu waelewe kwa nini Huyu Baba tuliyemuheshimu sana zamani amebadilika sana.
Mugabe na Marehemu Mke wake (Nahisi alikuwa anaitwa Sally), walikuwa marafiki sana. Wazimbabwe wengi wanajua kuwa Marehemu Mke wake ndiye aliyekuwa "The leadership Brains behind President Mugabe". Baada ya Kifo cha mke wake, Mugabe akabadilika.
Ndiyo Mugabe amekuwa dikteta, na pia nashangaa sana kwa nini watu wanamtetea.
Ukiangalia mfano wa Mugabe na Mke wake wa kwanza(Ambaye alikuwa adviser Mkubwa wa Mugabe), Marahisi wetu Afrika lazima wajifunze kuoa wanawake wenye akili na wenye kipaji cha uongozi.
Kifupi nataka kusema kuwa: kutokana na wazimbabwe wengi nilioongea nao, naamini kuwa, "Mugabe tuliye muheshimu, alifariki baada ya kifo cha mke wake Sally".
-
Jeff,
Jibu la swali lako kwa kifupi kabisa ni: Ndiyo, Mugabe dikteka.
Labda tubishanie maana ya neno dikteka tulinganishe na yaliyotendeka na yanayoendelea huko Zimbabwe hadi leo hii kuona kama kweli anastahili wasifu huo.
Halafu vilevile ubabe wa Marekani isiwe sababu wala kisingizio cha kukwepa ukweli kwamba Mugabe ni dikteta. Siku hizi naona imekuwa fasheni kila kiongozi wa nchi yoyote akibanwa inakuwa mbona Bush hivi Bush vile, kana kwamba mapungufu ya Bush ni leseni tosha kwa viongozi wengine kujifanyia watakavyo. Kwa upande mwingine hiyo ni ibada ya sanamu kumsujudia Bush!
Kwa Miriam,
Naona hapo unataka kumtetea Mugabe kwa hoja dhaifu kabisa, yaani una maana kwamba yeye hana akili wala uwezo wowote wa kuongoza bila marehemu mkewe Sally?
Kwa mtazamo wako mwenye makosa ni mkewe Sally kwa kufariki sasa amesababisha Mugabe "abadilike", ya kweli hayo? Yaani achemshe Mugabe alaumiwe marehemu Sally, duh! hiyo kali!
Hiyo hoja inapwaya mno...
-
GK,
Ndiyo naamini Mugabe hatumii akili yake ya uongozi kama alivyoitumia zamani wakati mke wake alipokuwa hai. Namtumia mke wake maana Udikteta ulianza baada ya kifo chake. Mke wake alipokua hai, Wazimbabwe wengine wanadai kuwa hakukubali ushauri wowote bila kupitia kwa marehemu mke wake, hiyo inaonyesha Sally alikuwa na nia nzuri ya kuendeleza nchi. Sasa kapata washauri wapya na udikteta ukaanza.
Sasa anawashauri wengi na huo udikteta haufanyi yeye peke yake. Lazima anashirikiana na viongozi wenzake ambao wanafaidika kwa matatizo ya nchi yao. Kama washauri wake wangekuwa na nia nzuri ya nchi yao, na wakagundua kuwa Mugabe anaharibu nchi, wangemtoa zamani katika icho kiti. Na kama Mugabe angekuwa anatumia akili yake, angegundua zamani kuwa watu wanaomshauri wana nia mbaya ya nchi angewabadilisha.
Mugabe tuliyemjua zamani, na Mugabe tunaye mjua sasa hivi, ni Viongozi wawili tofauti.
Naona ni vizuri tuache kumlaumu Mugabe peke yake, tunaitaji kuwalaumu viongozi walio mzunguka, bila wao, Mugabe hangeweza kuendeleza udikteta.
-
Miriam,
Nakuelewa vizuri tu, ila nachosema mimi kung'ang'ania kuwa mkewe pekee ndiye aliyekuwa mshauri wake mzuri(pamoja na kuwa huenda ni kweli) kunaashiria kuonyesha kuwa mwenye makosa siyo yeye per se ila huyo mshauri kwa kufariki na kumwacha bila ushauri mzuri, kitu ambacho siyo sahihi!
Hao wote wanaomzunguka si walikuwa naye hata wakati wa uhai wa mkewe Sally? Au labda washauri wake ni ma-yes men tu wako kwa ajili ya matumbo yao wanalinda vibarua vyao na huyo mkewe pekee ndiye aliyekuwa anamwambia ukweli?! Pengine...
-
Wandugu,
Kimsingi nadhani hakuna anayemtetea Mugabe per se.Itakuwa ni ujuha kusema au kuamini kwamba anayoyafanya Mugabe dhidi ya viongozi wa upinzani kwa mfano ni sahihi au anavyokuwa "haambiliki" ni sahihi!
Tunachojaribu kubainisha ni kwamba kama Mugabe anastahili kuitwa "dikteta" basi wapo wengi sana duniani na hatuna budi kuwataja na kuwachukulia wote hatua.Mfano wa George Bush huwa unakuja kama kinara kwa sababu tupende tusipende kibra ya dunia ya mambo ya siasa ni Marekani,hatuna jinsi.
Kuhusu suala la washauri na marehemu mke wake nadhani muhimu kutambua ni kwamba watu hubadilika kutokana na mazingira na nyakati.Zimbabwe ya jana sio ya leo kwa kuzingatia mambo kadha wa kadha .Kwa maana hiyo hatuwezi kufikia mahitimisho halisia katika kunyambulisha nini kingefanyika hivi leo endapo fulani au fulani angekuwa hai au angefufuka.
-
-
@GK,
Nadhani anachosema Miriam ni kwamba Mugabe alikuwa ameoza tangu zamani, ila marehemu mke wake alikuwa na uwezo wa kufunika uozo. Marehemu alipoondoka tu, uozo ukawa nje nje.
Visenti vyangu ni hivi: Waafrika hatujafikia sehemu ya kuwa na umiliki wa shida na mafanikio yetu. Kwani wanayoandika CNN siyo kweli? Kwani siyo kweli kwamba Mugabe aliwakong'ota wapinzani wake?
Hatuwezi kuanza kukaa na kulaumu waMagharibi kwa kila kitu. Huo ni unafiki kwanza, kwa sababu kwenye hotuba zetu za SADC tunawalaani, halafu kwenye ziara zetu tunatembeza bakuli...
Kwa kiwango cha "demokrasia" ambacho kipo kwenye nchi za magharibi, Mugabe ni dikteta. Ukiachilia mbali kiwango cha nchi za magharibi, Afrika yenyewe (mfano Zambia au Tanzania) inaelekea kwenye dira ambayo inamuweka Mugabe ambako tafsiri ya vitendo vyake si vingine bali ni vya kidikteta.
-
Tatizo langu ni moja: madikteta duniani ni wale ambao hawana urafiki na nchi za kibeberu.
Kweli Mugabe alipigiwa kura kama alivyosema Jeff. Lakini mabeberu wanasema aliiba kura. Wakati huo huo wanakula na kunywa na Musharaff wa Pakistani ambaye alitwaa madaraka kwa nguvu.
Haya, wanadai Mugabe anatesa wapinzani. Lakini hawasemi lolote kuhusu Mubarak wa Misri au Zenawi wa Ethiopia ambao nao wanafanya hivyo hivyo.
Unafiki huu ndio wakati mwingine unawapa watu wengine ugumu wa kudakia kauli ya mabeberu ya kuwa Mugabe ni dikteta. Hawataki kuendeleza unafiki huo.
Nakubaliana na mawazo kuwa hakuna sababu yoyote ya kulaumu mabeberu kwa kila jambo. Tabia hii Mugabe anaipenda sana. Anataka kutumia Uafrika wetu, upenzi wetu wa Uafrika na chuki zetu dhidi ya ubeberu na tabia ya nchi fulani kutaka kuongoza nchi nyingine kwa "remote control" kwa matakwa yake.
Nina swali: Hivi ni lini viongozi wa Afrika wataacha kuogopana na kuambiana ukweli?
-
Mugabe kung'ang'ania madaraka:
unajua kuna marais ambao wangependa kutulia, kupumzika na kufurahia uzee. Lakini kutokana na madhambi waliyofanya wakiwa madarakani hawathubutu kufanya hivyo kwa hofu ya kuwa watakuwa hawana nguvu za kujilinda. Ndio Mugabe huyo.
mugabe ana mapungufu fulani katika jinsi anavyotatua matatizo ya sasa nchini Zimbabwe,hata hivyo hayuko karibu kabisa na udikteta.tatizo lilopo duniani ni kwamba katika ngazi ya kimataifa kuna anarchy na mataifa fulani yanatumia mwanya huu kujinyakulia mamlaka ya kuamua mambo katika ngazi ya kimataifa.hapo ndio uwaita wale wanaofanya maamuzi kinyume na matakwa majina mbalimbali ya ajabuajabu ili tu kuvuta hisia za watu waungane nao katika kuwashinikiza juu masuala mbalimbali.ninashangazwa sana jinsi viongozi wa upinzani zimbabwe wanavyolichukulia swala zima!mataifa ya magharibi hayapiganii haki bali maslahi yao,ingekuwa wanapigania haki wangeweza kuona kuwa tatizo la kisiasa zanzibar ni kubwa zaidi ya ghasia za zimbabwe,nani amewahi kuzungumzia zanzibar kwenye vikao vya kimataifa?wanaishia kutoa tamko tu kuwa hawakuridhishwa na jinsi uchaguzi ulivyofanyika!