
Kuna jambo limeninyima usingizi.Nimetizama dari mpaka nimechoka.Mwishowe nikakumbuka msemo mmoja wa kizungu "Don't just sit there,do something".Nikaamka,nikatengeneza kahawa na kuketi mbele ya kompyuta yangu kuandika.Nafanya hivyo hivi sasa.
Katika pitia pitia yangu vyombo vya habari vya Tanzania hapo jana(juzi ya Tanzania) nilikutana na habari ya bunge "kuwaonya" watu wawe makini na jinsi wanavyoliongelea suala la mbunge kijana Zitto Kabwe kusimamishwa kuendelea kuhudhuria shughuli za bunge. La sivyo hatua za kisheria zitachukuliwa! Kwa maneno mengine sssshhhhh,nikusikie!
Ukiachilia mbali mshangao ambao bado ninao kuhusiana na sakata zima la kusimamishwa mbunge huyo, hili la kutoka kwa katibu wa bunge lilinitia woga kabisa.Pengine woga huo ndio unaoninyima usingizi mpaka hivi sasa.Swali kubwa lililotanda kichwani mwangu lilikuwa tunaelekea wapi? Ubabe huu unamsaidia au utamsaidia nani? Yaani sasa hata ule uhuru wa kujielezea (self expression) ndio nao unaota mbawa? Hivi ili niweze kusema siridhishwi na uamuzi wa bunge, kwa maoni yangu, kwa jinsi ninavyoona mimi kama mwananchi ni lazima nijue kanuni za bunge au niwe mwanasheria ambaye nitaketi na kuchagua maneno ya kusema kama vile nimesimama mbele ya jaji?Hivi..???
Majuzi niliandika kitu pale kwenye blog yangu ya kiingereza juu ya wenzetu wa magharibi kupenda kuripoti mabaya tu kutoka barani Afrika na kutochukua mazuri hata kidogo. Mfano niliotumia ni ule wa habari ya hivi majuzi nchini Kenya kuhusu mswada wa mabadiliko ya sheria uliokuwa unapendekezwa. Kama ulifuatilia suala lile picha ya hapo juu inajieleza kabisa. Ajabu leo nimeshindwa kutofautisha kilichokuwa kinajaribiwa Kenya na kilichotoka bungeni Tanzania ingawa kimsingi matukio haya mawili hayana uhusiano.Tunazibana midomo,tena kwa vitisho vya kisheria! Kumbe demokrasia bado ni dhana pana eeh,sikujua.
Lakini leo nimetiwa moyo kidogo kuona kwamba wameshajitokeza wanasheria maarufu tulionao nchini Tanzania kuwakumbusha wananchi juu ya haki zao na pia kuionya serikali.Sijui tunaelekea wapi kwa kweli.
Watatoa onyo mpaka nani hii arudi mara ya pili. Uhuru wa kujieleza wasidhani tutauachia eti kutokana na kuonywa. Katiba inaturuhuru na katiba ndio tunayoitazama na sio onyo toka kwa wezi wa demokrasia. Wanafikiri tunaishi enzi za gazeti la Uhuru na Mzalendo? Wanaishi nchi gani?
Kuhoji maamuzi na matendo ya viongozi wetu ni moja ya jukumu kubwa tulilonalo kama raia na wapiga kura. Ni haki na wajibu wa kila raia kuhoji kila linalofanywa na watumishi wetu.
Tutahoji maana tunataka kujua nani anasema ukweli kati ya serikali na Zitto.