
Maisha bila furaha si maisha. Katika nchi zilizoendelea watu wengi sana hawana furaha wala raha ya maisha yao ukilinganisha na wale waliopo katika nchi zinazoendelea. Ndio maana inasemekana taifa lililo na furaha kupita yote duniani ni Nigeria ikifuatiwa na Mexico, Venezuela (hawa nasikia ndio wenye wanawake warembo kupita wote duniani) na El Salvador. Najua kama ulikuwa hujui hili unashangaa kwani ulidhani taifa hilo pengine lingekuwa ni Canada, Marekani au Uingereza. Maisha ya ughaibuni yamejaa presha. Ingia ndani ya gari lako au ndani ya basi kama sio treni saa za asubuhi kisha utizame sura ya jirani yako ndani ya basi au kwenye mataa uone kama anaonekana kuwa na furaha yoyote ya maisha. Utashangaa.
Watu wengi wanafanya kazi ambazo hawazipendi.Wamo kwenye mahusiano ambayo hayakidhi haja zao wala achilia mbali kukaribia japo robo ya ndoto zao. Msongo wa maisha umewajaa mpaka utosini. Idadi ya watu wanaojiua ni kubwa katika nchi zilizoendelea kuliko zinazoendelea au hata zile zilizogoma kuendelea!
Yawezekana wewe msomaji wangu huna furaha au tuseme raha ya maisha yako.Unaperuzi mtandaoni hivi leo ili tu kupunguza msongo wa maisha. Sasa ufanyeje ili kuwa na furaha au kufurahia maisha? Hebu jaribu kufanya yafuatayo;
- Fanya mazoezi angalau kwa nusu saa tu mara tatu kwa wiki.
- Hesabu Baraka zako. Siku inapofikia ukingoni jaribu kujiuliza ni mangapi ambayo wewe umebarikiwa kuwa nayo ambayo wengi hawana.
- Tafuta muda wa maongezi- Jitahidi kupata muda wa kuketi chini na rafiki yako wa karibu au mpenzi wako mkaongea kwa uhuru na kinagaubaga.
- Panda mti au ua na kisha lipalilie.
- Tabasamu kwa mgeni utakayekutana naye leo.
- Cheka-cheka kwa nguvu zako zote kila upatapo fursa.
- Tenda jambo moja jema kwa siku.