Mwaka mmoja uliopita wanablogu wa kitanzania tuliweka historia mpya.Siku kama ya leo,yaani tarehe 18 Novemba 2006 kuanzia saa sita mchana kwa saa za Tanzania,wanablogu wa kitanzania tuliotapakaa dunia nzima tulikutana kwa minajili ya kuunda jumuiya yetu rasmi na kuwa na siku ya blogu Tanzania.Katika mkutano ule tuliipitisha rasmi siku ya tarehe 18 Novemba kila mwaka kuwa siku ya blog Tanzania.Kwa maneno mengine,leo ni Tanzania Blog Day.
Naikumbuka vyema siku ile kwani sio tu nilidamka asubuhi na mapema(ili niwahe mkutano uliokuwa umetegwa kwa masaa ya Tanzania ingali nipo Canada) bali pia sote tuliohudhuria mkutano ule tulikuwa tuna shauku ya kuunda jumuia ambayo italeta mabadiliko ya kijamii hususani kuhusu jinsi tunavyopashana habari na pia kuchangia katika uundwaji au ubomoaji wa sera za nchi.Huo ndio muelekeo wetu ambao nina uhakika bado tunalo jukumu la kuuendeleza kwa hali na mali.Siku ile sote tulikuwa na mioyo ya kimapinduzi na upendo wa aina yake kwa taifa letu,jamii zetu na dunia yetu kwa ujumla.
Usingeweza kututofautisha na kina Fidel Castro,Che na wenzao walipokuwa wakipanga mikakati ya kimapinduzi enzi zile.Tofauti kati yetu na wao ni kwamba wao walikuwa na silaha za wazi wazi kama bunduki na mijeledi.Sisi tulichokuwa nacho na ambacho naamini bado tunacho ni uhuru wa kupashana habari na kuwasiliana kwa minajili ya kuleta mabadiliko ya kijamii.Hii ndio jamaa wa Global Voices wanaiita Blogging For Social Change!Ingekuwa zamani tungesema tulikuwa tunachukua ule msimamo kwamba A Pen is Mightier Than A Sword.Tatizo ni kwamba zama hizi zinatumia zaidi “keyboard”kuliko kalamu ya kawaida au Bic kama wengi wetu tulivyozoea enzi zile.Kwani mmesahau kwamba kuna wakati tulikuwa tunahitimu kutumia penseli na kisha tunahamia kwenye kutumia bic?Hivi ilikuwa darasa la ngapi vile?
Tungekuwa tunaenda kwa ule mwendo wa kichama chama, leo ingekuwa ndio siku ya gwaride,mapambio,mashati au t-shirts za rangi za vyama,hotuba,vipeperushi, ahadi na mambo kama hayo. Tungekutana pale bwalo la maofisa na kutumia fataki za ule mvinyo wa kizungu(champagne) utadhani tumeshafanikiwa kuitokomeza vita ya njaa,maradhi na umasikini.Ungetuona usingedhani kama tunaishi kwenye nchi yenye raia kibao wanaolala njaa,wanaolala nje,mitaani,chini ya magari,yenye raia wengi wanaopoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma za afya na kero zingine chungu mbovu.Hapo sijataja wanaopasua kichwa badala ya mguu.Hebu tuachane na hayo,ngoja niendelee na ajenda ya leo ili nisije nikakukwaza ndugu msomaji bure.
Baada ya mkutano ule wa kihistoria tulichagua viongozi.Palikuwa na kampeni,japo za chini chini,tukapata fursa ya kukagua wasifu wa baadhi ya wagombea nk.Demokrasia ikachukua mkondo wake,tukapata viongozi.Hapakuwa na shampeni wala ulanzi lakini sote tulifurahi na bado tunafurahi kwamba tunao viongozi.Lakini nisingependa tusahau kwamba hata kabla ya kukutana rasmi na baadaye kupata viongozi,kuna wakati tulishapata “Azimio la Dodoma”.Si unakumbuka tulivyowekeana maadili ya maana?Tatizo wale jamaa waliokutana Dodoma na baadaye sisi kuamua kulikubali azimio lao,wote wamepotea kwenye ulimwengu wa blog hivi leo.Blog zao zimeanza kuwa kama zile ofisi za masijara za ile wizara pale karibu na wanaposhinda kutwa nzima vijana wanaoojiita “misheni tauni”.Najiuliza hapa,hivi nikiwatajia yale majina ya wana-Dodoma mtanisaidia kuwauliza nini kimewasibu?Au na wao kuna mlungula umetembea ili kuwazima?Sijui.
Pamoja na kupata viongozi na matumaini mapya,leo naomba nisiwe mnafiki bali niseme wazi kwamba,kuanzia pale mambo kwa kiasi fulani yakaanza kwenda taratibu mno.Sababu zaweza kuwa nyingi na tofauti.Lakini ukweli utabakia(kwa mtizamo wangu) kwamba kuna kasi imepotea ambayo hatuna budi kuirudisha kwa kasi pia.Mfano mzuri ni jinsi ambavyo siku hii ya leo tunaikumbuka.Si unakumbuka kwenye mkutano kuna jamaa aliniahidi kwamba leo atanipa mvinyo tani yangu?Au wewe umesahau?
Yote tisa,kumi ni swali ambalo leo limegubika moyo wangu.Swali hilo ni je wangapi kati ya wanablogu waliohudhuria mkutano ule na hata wale ambao hawakuhudhuria lakini baadaye wakatambua yaliyojiri mkutanoni siku ile wanaikumbuka siku hii muhimu?Na je mbona viongozi wetu hata hawakuchukua jukumu la kuikumbusha jamii kuhusiana na siku hii?Nini kimetokea?Kama na wewe msomaji wangu umesema,ah hivi kweli eenh,todei wi wea sapozidi tu rimemba endi selebreiti bulogu dei,basi jua tuna tatizo.Mimi na wewe.Wala usipande darini ukadhani utakuwa salama.Kunguni wako kila sehemu,shauri yako.
Kwa mfuatiliaji wa maendeleo ya blogu za kitanzania,atakubaliana na mimi kwenye jambo moja muhimu.Msisimko uliokuwepo hapo mwanzo mwanzo,haupo tena.Unazikumbuka enzi zile za kumkaribisha kila mwanablogu mpya kwa maneno matamu na ya kutiana moyo?Kila mtu mpya “alipokata shauri” na kuamua kufungua blogu sote tulifahamishana.Tukachukua dakika chache za kukaribishana na kutakiana heri.Tulikuwa na ujamaa wa aina fulani ambao binafsi niliupenda sana.Mpaka leo hii napata faraja nikitembelea “post” yangu ya kwanza kabisa na kuona jinsi wanablogu walioanza kabla yangu walivyonikaribisha na kunitakia kheri.Whati hapenedi?
Ni wazi kwamba tunafanya makosa.Tunafanya makosa ya kuzipuuza zama hizi mpya za mawasiliano ya umma(mtazamo wangu).Kwanza sitaki kuamini kwamba tunazipuuza au tumeanza kuzipuuza. Sitaki kabisa kuwaza namna hiyo kwani nikifanya hivyo siku si siku itabidi mnipeleke Dodoma.Wenzetu,kwa mfano wakenya na waganda wanaendelea kuzikumbatia zama hizi kwa marefu na mapana.Sisi bado tunaenda kwa mwendo wa kinyonga.Tuna haja ya kuanza tena kukimbia.Tuna kila sababu ya kuzidi kuungana,kuzidi kuwaalika watanzania wengine wenye maarifa tofauti tofauti kufungua blogs zao,tena za Kiswahili ili sio tu tukuze lugha yetu bali tuongee tuelewane.Tusipofanya hivyo tunazidi kuwaachia wenzetu fulani fulani,wa ndani na nje ya nchi,waamue mustakabali wa maisha yetu.Nasema hivi kwa sababu moja,usiposema kupitia kwenye mawasiliano ya umma kama blogs,utasema kupitia wapi?Kwenye pishi la pilau na kanga kutoka barahindi?
Ubaya au uzuri wa zama mpya mara nyingi huwa zinahitaji kuoteshwa ili baadaye ziweze kuota mizizi na kutupa matokeo tunayoyahitaji.Raisi Museveni wa Uganda ana kitabu chake kizuri sana kinachoitwa Sowing The Mustard Seed(ukikipata kisome).Jukumu hilo la kuotesha ni letu sote.Viongozi kazi yao ni kutuongoza tu,watendaji ni sisi sote.Tusikubali kutupa mti na jongoo wake. Kama umekaa pembeni ukisubiri wenzio wakuoteshee mbegu kwanza unafanya lisilo jema.Fikiria upya.
Mwisho naomba niwatakieni wote Happy Tanzania Blog Day.Najua hata kama hakuna shangwe na vigelegele mwaka huu,basi mwakani huenda tukawa nao.Tutazichagua blog bora na kuwapa waongozaji wake japo bilauri ya mpingo ili wakanywee ndani yake wakikumbuka kesho yake wanatakiwa kuendeleza libeneke kama rafiki yangu Issa Michuzi anavyopenda kusema.Tuko pamoja ndugu zangu katika blogu.Nalia lakini..usinione hivi.
Ni furaha kuu kwamba wanajumuia ya log Tanzania sasa tumekuwa na umoja wa uhakika. Ni vyema tukatafakari namna nzuri ya kuimarisha zaidi umoja huo ili kuwa na sauti moja ya kuoigania uhuru wa kuzungumza, na zaidi sana uhuru wa uchumi kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe bila kutegemea wawekezaji na 'wajomba' wafadhali. Kila jema wanablog wa TZ