Leo siwezi tena kuomba msamaha kwa kutokuandika hapa mara kwa mara.Kama mnataka na mimi nijiuzulu kama waheshimiwa huko Tanzania….we acha tu.Vyeo vitamu bwana…si mlisikia wenyewe jinsi sauti za waheshimiwa zilivyokuwa zikitetemeka na kujaa mwangwi wakati wakitangaza kujiuzulu? Si mliona pia jinsi wengine hadi wake zao walivyoangua chozi?Unafanya mchezo nini? Hapo mimi ndipo ninaposhangaa,kama cheo au ukubwa unaupenda hivyo,kwanini usiwe mwadilifu basi?Eti kwanini? Kama wewe unajua kwamba hapa duniani unapenda kubebewa briefcase,unapenda kufunguliwa mlango wa gari na wa nyumba,unapenda kufungwa mkanda kama vile mtu uliye hoi kitandani,kwanini unaleta uzushi na uzabinabina unapokuwa madarakani?
Okei,sasa jamaa wametangaza kujiuzulu,mkuu wa nchi kakubali maombi yao..what next? Next ni kwamba jamaa bado wapo bungeni,tena bado wanachangia mijadala.Hii ndio bongo bwana.Changa la macho kama kazi. Hivi si ni ajabu kwamba unapojiuzulu,baada ya kukumbwa na kashfa nzito kama ya ufisadi,ubunge nao unatakiwa ukome mara moja? Mpiga kura gani anataka kuendelea kuwakilishwa na “fisadi’. Halafu Tanzania hamna hata ile sheria ya kuweza kum-recall mbunge.Yaani mkishamchagua,mnalo kwa miaka mitano.Linakuwa tsunami lenu tena. Halafu huko bungeni aliyemwaga manyanga jana leo anachangia na kusema Rais amechagua “mtu kama mimi”.Yaani wazi wazi kabisa mtu anasema,mmeuvaa tena mkenge.Na anapigiwa makofi na virungu! Ee bwana ndio…hii ndio bongo…kila mtu inabidi ajifanye hamnazo ili angalau kesho aweze kuamka na kwenda kazini. Hebu kwanza cheki hapo kama umeme upo bado au ushakata na kompyuta yako inatumia ule wa kudandia tu unaposoma habari hii.
Haya sasa,PM mwingine huyooo..anajinadi..anasema yeye ni mtoto wa kwanza(hata sijui hii inahusiana na nini).Anasema yeye ni mtoto wa mkulima.Alikuwa au bado ni mtoto wa mkulima? Kiswahili lazima tukitanue wajameni.Ahaaa…kumbe huyu naye anatoka pale pale…yaaani pale pale kwenye ofisi ya waziri mkuu! Halafu sura ni miongoni mwa zile zile.Bila woga na yeye anasema kumbe keshakaa sana pale ikulu..yaani anapajua kuliko hata nani sijui. Sasa hapo ndipo utakapochoka…kumbe sasa nini kipya hapa? Hapo hujazingatia jinsi mambo yalivyokwenda fasta? Hivi unataka kuniambia mambo yote haya,kimstakabali wa nchi..nasema nchi sio kijiji,yanafanyika ndani ya masaa kama 16 tu?? Kama ni kweli basi nchi yetu inastahili medani ya hali ya juu sana kwenye suala zima la disasters preparedness.
Wale wanaoitwa wapinzani…masikini hawa nao naona wamepigwa ganzi kiaina.Yaaani hata kuguna hawakuguna! Ingekuwa mimi ningesema haya ninayoyasema hapa.Eti nini…anaitwa nani?Pinda? Ofisi ya nani..Waziri Mkuu?
Sasa subiri baraza jipya la mawa-siri.Hapo ndipo utaweza kuthibitisha hizi hoja zangu.Kama unabisha tizama kama yule jamaa mwenye jina linalohusiana na vita vya majimaji hatarudi tena kwenye “kebineti”.Ni kama vile hakuna watu wengine wanaoweza kuwa mawaziri na manaibu waziri.Utasikia tu.Tena nasikia ule msururu wa mawaziri unarudi tena,tena na zaidi.Hii ndio bongo.
Aisee ukiona kimya sana hapa usidhani nimetoweka duniani..huwa pia naandika pale http://bongocelebrity.com.
Jamani nimeuliza kuwa Ndesanjo kakumbwa na nini? Maana hata blogi yake siipati mimi, hebu nisaidieni wajameni