
Kama mtanzania, leo sina budi kuungana na watanzania wenzangu duniani kote kuadhimisha miaka 7 tangu Mwalimu J.K.Nyerere aage dunia kule Uingereza. Nafanya hivi kwa heshima niliyonayo juu ya kiongozi huyu aliyeongoza mapambano dhidi ya ukoloni na ukombozi wa bara zima la Afrika. Kinachomtofautisha Nyerere na viongozi wengine ni nia safi, imani halisi katika ukombozi wa muafrika.
Kinachotakiwa kufanyika hivi leo ni tafakuri za dhati juu ya uongozi wa Mwalimu,nini alikisimamia,nini alikiamini na kwa namna gani alifanikiwa au alishindwa. Tafakuri za namna hii sio tu zitatusaidia kujua historia bali kupanga vizuri mikakati ya taifa letu. Hatuwezi kuepuka kirahisi (pengine hatuna hata sababu) misingi waliyotuwekea Mwalimu na viongozi wenzake wa wakati ule. Mwalimu alijaribu. Kama binadamu yoyote yapo aliyokosea.Mimi nimemsamehe kwa sababu aliposhindwa alikiri, japo inawezekana kwamba alichelewa kukiri au kukubali kwamba amechemsha.
Kwa bahati mbaya siku hii ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imetekwa nyara ya wakora wa siasa. Leo hii utasikia hotuba chungu mbovu,utasikia neno "tumuenzi" kuliko neno lingine lolote. Hili hutia hasira kupita kiasi.Ukitaka kujua kiwango cha unafiki miongoni mwa viongozi wetu basi nenda tu viwanjani,majukwaani nk ukasikilize hotuba za viongozi katika maadhimisho haya. Naamini kabisa kwamba endapo viongozi wetu wangeitumia siku hii kujifanyia personal analysis ya uongozi wao basi "nchi ya ahadi" haingekuwa mbali kama ilivyo sasa.
Katika maadhimisho haya mwaka jana niliandika namna hii (usisahau kusoma maoni ya wachangiaji). Ningeweza kabisa kuiweka makala ile kama ilivyo kwa sababu hakijabadilika kitu. Pengine swali ambalo sote tunabidi tujiulize ni unafiki umepungua au umeongezeka? Jibu sahihi unalo wewe msomaji. Hivi unadhani Nyerere angekuwa hai na kiongozi wa nchi angeweza kutokea Cuba kwenye mkutano wa nchi zisizofungamana na upande wowote na kisha kukimbilia Washington kupiga stori na "mkuu wa mabepari"? Unapoongelea kumuenzi Mwalimu unakuwa unamaanisha moja au mbili?
Tupende, tusipende jina la Nyerere limebakia kuwa nembo ya kisiasa tu.Viongozi wetu wa sasa wameamua,kwa makusudi, kulizika jina lake kwa "kutomuenzi" kama ahadi zao za kisiasa zinavyosema kila siku. Wanaolia na kumkumbuka kwa dhati ni wananchi wa kawaida ambao nao wanafanya hivyo kwa imani tu kwamba huenda angekuwa hai hili na lile lisingekuwa kama lilivyo hivi sasa. Huenda angeshazidiwa nguvu na majangili. Dalili za kuzidiwa nguvu zilianza kuonekana tangu akiwa hai. Unakumbuka msururu wa watu waliotaka kwenda ikulu mwaka 1995? Unajua wako wapi aliowakemea? Unajua mali wasizoweza kuzitolea hesabu zimeongezeka au zimepungua? Sasa nani anakudanganya kwamba kuna falsafa ya Mwalimu iliyobakia?
Yana mwisho haya.Tafakari.
Hapana shaka kwamba hakuna falsafa ya Mwalimu inayofuatwa, ni blabla tu, wakubwa wanaona aibu kuhusu siku hii, ila hawana jinsi, maana isipoadhimishwa itakuwa aibu kubwa zaidi. Lakini ukweli falsafa za mwalimu zimezikwa pamoja naye! Nikiangalia utawala mpya ulivyoanza, nina wasiwasi kwamba matabaka yataongezeka kuliko wakati mwingine wowote ule! Sasa hivi Rais na serikali yake wanakumbatia matajiri wa ndani na nje! Mifano iko mingi. Muda si muda, pengine haitazidi miaka mitano, masikini atakuwa hana chake tena katika nchi hii! Na hii italeta matatizo makubwa sana. Sasa hivi serikali inamwandama masikini katika namna ambayo ni dhahiri. Kwa mfano angalia sakata la wamachinga, wamefukuzwa kutoka katikati ya jiji wameelekezwa waende sehemu inaitwa Kigogo Sambusa, Mchikichini na huku relini nyuma ya stendi ya mabasi ya Scandinavia!
Hapo Kigogo Sambusa ninapopita (maana mimi nakaa Magomeni kwa hiyo karibu kila siku hupita hapo), naona wamachinga wamejijengea wenyewe vibanda vya mbao tena bila mpangilio wowote, mbaya zaidi hili ni eneo la mkondo wa mto Msimbazi, ikija mvua biashara zote pale zitakufa maana Bahari huwa inahamia pale! Hata hivyo tangu vimejengwa hivyo vibanda hadi leo inakaribia mwezi, lakini hakuna hata mfanyabiashara mmoja aliyeanza kuuza! Hawapataki na kwa kweli hapafai! Wote wamekimbilia Mchikichini! Na sasa Mchikichini kumefurika! Umati uliojazana hapo, anajua Mungu na Mitume Yake! Mpaka barabara ya Uhuru inakaribia kutopitika!
Kwa upande wa huku Relini, serikali imekwenda kuwavunjia tena, wanadai kwamba hawastahili kuwepo hapo na walipelekwa kwa makosa!
Achilia mbali tatizo la Umeme!!
Yaani ukiangalia masikini hawa wameshatupwa! Hakuna sera za Mwalimu zinazofuatwa. Na naamini mwalimu akifufuka leo halafu ajionee mwenyewe kilichoendelea baada ya yeye kufa, atakufa tena kwa mshtuko!