Monday, April 23, 2007

UMESHAWAHI KUUMWA NJAA?:MSAIDIE ANAYEKUFA NA NJAA!


Jaribu kukumbuka siku ambayo ulishikwa na njaa isiyo ya kawaida na hukuwa na hata maji ya kunywa kupoza kiu. Jaribu pia kufikiria ni mateso ya kiasi gani kukosa chakula mpaka ukakata roho kwa njaa.Kila mwaka mamilioni ya watu duniani wanafariki kwa njaa pamoja na kwamba juhudi mbalimbali za kimataifa zinafanyika ili kunusuru hali hii.

Zaidi ya watu 24,000 duniani wanafariki kila siku kwa njaa. Robo tatu ya watu hao ni watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.Nchi kama yetu ya Tanzania kwa mfano, ni mojawapo ya nchi ambazo raia wake, hususani wanawake na watoto, wanafariki kwa magonjwa mbalimbali yanayotokana na ukosefu wa chakula na njaa kwa ujumla.

Sasa kwa kuzingatia nguvu ya mtandao, mwaka 1999 tovuti iliyopewa jina la “Tovuti ya Njaa” ilianzishwa ambapo kila unapoitembelea tovuti hiyo na kubonyeza kitufe kinachoonyesha “bonyeza hapa” sahani au kikombe cha chakula huchangiwa na mashirika wadhamini ili kumlisha mtu mwenye njaa mahali fulani duniani (sio lazima iwe Tanzania) Kwa hiyo unachotakiwa kufanya ni kujitahidi kuitembelea tovuti hiyo kila siku na kubonyeza mahali palipoandikwa Help Feed The Hungry .Inawezekanaje?

Ni hivi, mashirika ambayo ndio wadhamini wakubwa wa kuwepo kwa tovuti kama hii wanaweka matangazo ya biashara zao (naamini unajua kwamba matangazo ya kwenye mtandao ni biashara ya mabilioni ya dola) na kubakia na imani (sio imani bure hii) kwamba umeyaona matangazo yao na huenda ukanunua au kutumia bidhaa au huduma wanazozitoa. Ni rahisi namna hiyo kumsaidia mwenzako mwenye nja!Kwanini wasitoe basi fedha au chakula hicho bure kama wanajali? Swali zuri lakini kumbuka ubepari haujali utu wa mwanadamu bali faida.

Katika miaka mitano ya mwanzo tangu kuanzishwa kwa tovuti ya njaa, watembeleaji (surfers) wanaokadiriwa kufikia milioni 200 waliweza kuchangia zaidi ya sahani milioni 300 za chakula. Jamaa wengine wajulikanao kama Mercy Corps nao ni wazuri kuwatembelea na kuona jinsi gani wanapambana katika kuitokomeza njaa.Usisahau kumwambia pia rafiki,ndugu na jamaa yako afanye hivyo hivyo pia.

Picha na Cedric Kalonji.

1 comment:

  1. Anonymous2:49:00 PM

    Jeff,
    Hongera kwa juhudi zako za kuukomboa ulimwengu kwa kuamsha watu wageuke kuwa binadamu.Kila mara ninapoitembelea hii blogu yako nimekuwa nikijifunza kitu kipya,kujua harakati mpya duniani nk.Naomba uendelee na moyo huo huo.Inshallah mbingu zinakuona.Nitakuwa natembelea tovuti hiyo na kukong'oli japo mara moja kwa siku.

    Mugasa

    ReplyDelete