Friday, May 04, 2007

UNAHESHIMU UHURU WA HABARI?

Jana ilikuwa ni siku ya uhuru wa habari duniani. Kama tunavyojua, uhuru wa vyombo vya habari ni vita ambayo tunaweza kusema haina mwisho. Waandishi wa habari bado wanatishiwa, wanauawa, wanatiwa gerezani, wanapigwa, wanateswa wao wenyewe na wakati mwingine hata familia zao. Hivi sasa tunapoongelea “waandishi wa habari” hatuwezi kusahau dhana mpya ya uandishi wa umma (citizen journalism) ambamo wanablog nao wanakuwamo. Blog ni tishio jipya kwa wale wasiopenda au kuheshimu uhuru wa habari.


Tangu uandishi wa umma uanze kuchanua baadhi ya wanablog wameshatiwa ndani, wameshashtakiwa, wamenyanyaswa nk Mfano mzuri ni kesi hai ya wanablog wa huko Misri Kareem Amer na Abdul Moneim Mahmud kama ambavyo imeanishwa katika tovuti ya Maripota wasio na mipaka au kwa kizungu Reporters Without Borders ambao kazi yao kubwa ni kutetea haki za waandishi wa habari na pia kuibua hadharani madhambi wanayofanyiwa waandishi wa habari wakiwemo wanablog.

Je, wewe unaheshimu uhuru wa vyombo vya habari? Kama ndio basi tembelea tovuti ya Maripota wasio na mipaka kisha usaidie kwa kutia saini petition mbalimbali ili kusaidia kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kitu ambacho ni muhimu sana katika kujenga jamii zinazoheshimu demokrasia, haki za binadamu na maendeleo.

Kwa kumalizia hebu soma habari hii ya jaji mmoja huko Washington anayedai jamaa wa Dry Cleaner wamlipe dola milioni 65 kwa sababu walimpotezea suruali yake! Huku Marekani ya kaskazini watu wanapenda kushitakiana si mchezo.

1 comment:

  1. Anonymous1:01:00 PM

    Shukrani kwa kutukumbusha kuhusu siku hii. Nimepotea kidogo, nataka kuchangia kuhusu ile picha ya "shule" ya msingi.

    ReplyDelete