Thursday, July 05, 2007

AFROFEST

Wikiendi hii hapa Toronto ni tamasha la AfroFest. Hili ni tamasha ambalo waafrika huwa tunajisikia kama tupo nyumbani.Tunajivinjari kwa muziki kutoka kwa wasanii mahiri wa bara la Afrika huku tukila vyakula vya kwetu. Jirani zetu wakenya huwa wanapata muda muafaka wa kutafuna githeri,sukuma wiki huku sisi tukijidai na chapati, sambusa,kachori nk. Kwa bahati mbaya sijawahi kukutana na makande.Ipo siku, mama ntilie wa A-Town au MS watatia timu hapa, we subiri tu!Waganda huwa wanatesa na matoke yao huku wenzetu wa afrika magharibi wakijing'ata na fufu .


Pamoja na raha za AfroFest, huwa nakerwa na tabia ya baadhi ya waafrika kujidai sio waafrika.Hususani watanzania.Si unakumbuka siku zile nilipokuambia kwamba wakati bendera za nchi zingine zilikuwa kibao zinapepea wakati yetu ilikuwa moja tu mkononi mwangu? Eti watu wanaona noma kuonekana watanzania.Kisa! aah bwana kwani wewe hujui sisi ndio nchi masikini wa kutupwa barani Afrika? Huwa wakiniambia hivyo hata mimi nanywea kidogo lakini wakati huo huo kuzidi kuipandisha bendera.Nyumbani ni nyumbani tu na mkataa kwao ni…..Lakini mwaka huu nadhani wakereketwa wa nchi tutaongezeka. Si katibu mkuu msaidizi wa umoja wa mataifa ni mtanzania? Si timu yetu ya taifa imemfunga muafrika magharibi hivi karibuni? Nyerere si anakaribia kutangazwa mtakatifu?au?

Mwaka huu wanaotarajiwa kulipanda jukwaa ni Samba Mapangala & Orchestra Virunga, Zale Seck Source w/ Abdoulaye Diabate, HAJAmadagascar & The Groovy People, Nawal-The Voice of the Comoros, Ruth Maniang Samba Squad na wengineo kibao. Mahotella Queens walikuwa waje ila wamechomoa dakika za majeruhi. Kwa habari zaidi unaweza kutembelea musicafrica.org

3 comments:

  1. Samba Mapangala naye yuko kwenye orodha... Ingekuwamimi ningemuomba acheze vunja mifupa kama meno bado iko...
    Anyway vyovyote vile endeleeni kupata culture

    ReplyDelete
  2. Jeff,umekutana n aZubeda niliye,tuma akutafute?

    ReplyDelete
  3. Anonymous8:47:00 AM

    Simon,
    Nimekutana naye na tulikuwa sote kwenye AfroFest.Nitakuandikia kwa habari zaidi.

    ReplyDelete