Friday, July 20, 2007

MSIOGOPE,KAPIMENI!

Ninapoanza kuandika hapa nilipo ni jioni.Nchini Tanzania ni usiku wa manane.Watanzania wengi wamelala,wengine fofofo huku wakikoroma kutokana na wingi wa ndoto.Kumbuka watu wanaokoroma mara nyingi wao ndio huwa wa kwanza kwenda kulala.Hivi kwanini eti?

Kwa upande mwingine wapo walio macho.Macho yamewatoka,wanawaza na kuwazua,kijasho chembamba kinawatoka.Mambo shaghalabaghala,hakieleweki. Miongoni mwa hawa, wamo wabunge wa bunge la nchi. Kisa? Kesho ni zamu yao kumuunga mkono raisi katika kampeni ya kuhakikisha Tanzania inakuwa mfano wa kuigwa katika vita dhidi ya ukimwi duniani. Kwa hili nampongeza sana raisi wetu. Penye mema lazima nitasema. Nisiposema usisite kunikumbusha msomaji wangu.

Kwanini wabunge wetu wawe na wasiwasi? Mambo kadhaa yanaweza kuzingatiwa ili kupata jibu.Kwanza wao pia ni wanadamu. Kama wanadamu wengine na wao “wanashughulika” yaani wanajamiiana,wanasaidia kuongeza idadi ya watu. Kwa maana hiyo wapo wanaojihusisha na ngono salama na pia ngono zembe. La pili ambalo pengine ndio linaloongeza joto la tumbo ni kwamba wengi wao wanajulikana kwa kutumia vibaya (au vizuri?). Wengi wamekuwa wakilaumiwa kwa kupokea ile rushwa haramu ya ngono. Lakini pia wengi ni wenye kipato cha kueleweka hata kama wengi wetu hatuelewi wanafanya kazi gani! Sasa kipato huwa kinakuja kimeambatana na influence. Kutegemea na mtu, wapo wanaotumia influence hiyo kujipatia vimwana. Yaani hawa ndio wale wanaojiita “wazee wa kuku kwa mrija’” wakiingia baa kila mtu anafurahi kwa sababu wanajua tupa tupa kaingia.Kwa bahati mbaya au nzuri tupa tupa huwa hatoki peke yake.Lazima atoke na mwenzi wa kumsaidia kulala( sijui ni kulala au kukesha). Hapo ndipo mgogoro unapokuja.

Pamoja na jinsi zoezi zima la kupima ngoma linavyoweza kuogofya, ni zoezi muhimu sana.Ndio maana ninampa shavu JK na kuwaambia wabunge, msiogope.Zoezi hili linaweza kuwa ndio kazi ya maana na inayoonekana wazi ambayo mmeshawahi kuifanya tangu muingie bungeni. Haki ya nani vile.Kwa hiyo shime, wala usitoe udhuru. Na kama wananchi wengine, ukijua umeshaathirika basi fuata ushauri utakaopewa na ukijua hujaathirika basi chukua tahadhari kwani mwakani tunataka kupitisha sheria ambayo itasema ni marufuku kiongozi akifariki watu waseme tena “ni shinikizo la damu tu”. Kila la kheri.Mungu ibariki Tanzania.

Picha ya juu nimeiiba pale kwa Michuzi.Nimeipenda kwa sababu kwanza sijamuona mzee Lyatonga muda mrefu na pili mtoko aliotoka nao umenipa jibu,bado yupo na bado anawania uraisi. Huyu bwana bado namdai kura yangu ya mwaka uleee.Mkionana naye tafadhali mwambieni.

4 comments:

  1. Jeff, nimekutag.
    Tujulishe vitu nane tusivyojua kuhusu wewe.

    ReplyDelete
  2. Eti ukipima unaweza kufa kwa kihoro. Wajanja wanachuna tu.

    ReplyDelete
  3. Anonymous11:56:00 AM

    Naona mambo si mabaya! Bro vipi, umeshaeenda kupima lakini??

    ReplyDelete
  4. Anonymous12:51:00 AM

    Haaaaha Jeff kweli hii picha hata mie imenivutia haswa kwa ndugu yangu Lyatonga amependeza

    ReplyDelete