Monday, December 17, 2007

PIGANIA UHURU WA KUJIELEZEA

Miaka michache iliyopita kulikuwa hakuna blogs. Kama ulitaka kusikika ilibidi utumie mlolongo mrefu sana. Mmojawapo ulikuwa ni ule wa kuandika barua kwa "mhariri".Na yeye,kutegemea na utashi wake au hongo aliyopokea juzi pale alipokutana na "mheshimiwa" katika ile baa karibu na wanaporandaranda "madada poa"(nasikia siku hizi wameingiliwa na makaka poa pia),mara nyingi zilikuwa zinaishia kapuni.

Matumizi ya blogs au uandishi huria kama ambavyo wengine wamependa kuuita, yameleta mapinduzi mapya. Bado yanaendelea kuleta mapinduzi mapya. Leo hii naweza kuandika na wewe ukasoma bila kupitia mlolongo mrefu. Unachotakiwa kuwa nacho ni tarakilishi na muda tu. Kizuri zaidi ni kwamba unaposoma nilichoandika unaweza kuchagua kukubaliana nami,kupingana nami au kunibeza tu na kuondoka zako kwenda uendako. Katika makundi yote hayo matatu unao pia uwezo wa kuniachia "vidonge" vyangu. Unaweza ukasema kwanini unakubaliana nami au unapingana nami. Mambo yanakwenda hivyo. Bila kurushiana ngumi wala kukunjiana ndita,tunaelimishana,tunajenga jamii.

Nasi, bila kukaa ndani ya yale masinagogi ya waandishi, tunaandika. Ukiamua kutuita waandishi au wacheza mduara ni juu yako.Tunachojua ni kwamba hivi sasa tuna uwezo wa kuandika na tukasomwa kuliko yule bwana mhariri mkuu.

Tatizo linakuja kwamba watawala walio wengi, wale ambao maisha yao yamejaa longolongo kila kukicha,huwa hawataki kusikia kitu kinachoitwa "uhuru wa kujielezea' achilia mbali uhuru wa vyombo vya habari wala waandishi. Ndio maana kuna mashirika au oganaizesheni kama PEN ambazo kazi yake kubwa ni kutetea uhuru wako wa kuandika,kusomwa nk. Hebu watembelee hapa, usichelee kujiunga nao. Soma visa mbalimbali vinavyowakuta waandishi. Pigania haki yako ya kujielezea.

1 comment: