Monday, May 01, 2006

TORONTO MWEZI WA NANE!


Mwaka huu kongamano la kimataifa la ukimwi linatarajiwa kufanyikia hapa Toronto,Canada. Ninatarajia kushiriki kikamilifu. Kuanzia ijumaa iliyopita nimekuwa nikihudhuria kongamano zingine ndogo ndogo za kijamii...hususani za watu weusi wanaotokea Afrika na wale wa visiwa vya Caribean hapa Ontario. Kongamano hili limefanyikia kwenye hoteli ya Ramada hapa Toronto(pichani kulia)...picha za ndani ya kongamano na vyombo vya habari vilikuwa marufuku ndio maana picha niliyoambulia ni hii ya nje.

Ni wazi kwamba vita dhidi ya ugonjwa huu bado haimthamini vilivyo mtu mweusi. Hapo ndipo tumekuwa tukiongelea kujikomboa sisi wenyewe,kusaidiana sisi wenyewe na pia kuacha kutegemea "huruma" za wenzetu. Chini kabisa ya moyo wangu naamini tunaweza.Tunachotakiwa kufanya,hapa ughaibuni na hata kule nyumbani ni kusema hapa,imetosha. Tuachane na tabia ya kutegemea na kusubiri mpaka tusaidiwe basi ndio na sisi tuonyeshe kwamba tunaweza.

Maswali ambayo ninajiuliza hivi sasa kabla ya mwezi wa nane ni kwamba nini kitabadilika baada ya mkutano kama huu unaokuja ambao maandalizi yake hugharimu mabilioni ya dola ambazo zingeenda kwenye elimu na uwezeshwaji kuhusiana na mbinu za kupambana na ugonjwa huu? Nafasi za wewe kushiriki kwenye kongamano hili nadhani bado zipo. Angalia kwenye
tovuti hii hapa uone kama utaweza shiriki nasi hapa. Ukikubaliwa, malazi na usafiri wa kwenda kwenye mkutano niachie mimi.

Mwisho je unamkumbuka Philly Bongole Lutaaya? Tunao bado watu maarufu wenye moyo kama wa huyu bwana?

6 comments:

  1. Jeff namkumbuka Phili Lutaya na kibao kile moto moto I was Born in Africa. Kama kuna mtu anaweza kuniweka kwenye mtandao au kunisaidia nikipate jamani anisaidie maana lile rege lilinikuna sana nyakati hizo na kila nikirejea maneno kama Iwas born to dance, dance music and singo songs, au music is a topic today na mengine yaani namkumbuka sna shujaa huyu wa Uganda. Huyu nikifananisha na Tanzania katika Muziki namuweka kundi la Kalikawe na lile songi la Nichakwizuka! Yaani we acha tu, watu ufa muziki hubaki na kuishi milele.

    ReplyDelete
  2. Ulipomtaja Philly Rutaya umenikumbusha umuhimu wa filamu katika kupambana na vitu hatari kama Ukimwi. Mimi niliiona filamu yake zamani kidogo na kwa kweli iliniliza. Ni filamu iliyokuwa ikiratibu safari na maisha yake kwa jumla na jinsi Ukimwi ulivyomla taratibu mpaka kukatisha maisha yake. Wakati tunaiangalia, tulikuwa kundi la watu, na kipindi kile ilikuwa ni tunaangalia TV uwani kwa jirani yetu mmoja ambaye alikuwa ni fundi wa TV kwa hiyo kila usiku kuanzia saa 2 usiku alikuwa anatoa TV watu tunaangalia sinema tunashangilia mpaka basi! Lakini filamu ya Philly Rutaya ilipoisha ikabidi watu tuombe mwenye TV aweke mkanda wa Pepe Kalle tujiliwaze, kila mtu alichanganyikiwa na hakukuwa na kushangilia kama kawaida yetu!
    Ile ilikuwa ni NGUVU YA FILAMU!
    Na ndicho kitu ninachotamani kukipigania.
    Ninachowaza mimi ni kwamba UKIMWI ni tatizo linalotokana na tabia zetu na namna ya kupambana nalo ni ushawishi wa akili za watu kubadilika. Kwa mawazo yangu, filamu ni moja kati ya nyenzo muhimu za kupambana na UKIMWI, kuonyesha ubaya wa tabia na elimu za UKIMWI.
    Huku nyumbani, kuanzia Mei 20 hadi Juni 10, ninaingia 'location' kurekodi filamu yangu nyingine. Na kwa bahati nzuri hii ni filamu ya UKIMWI. Inaeleza kuhusu umasikini unavyochangia kusambaa kwa UKIMWI vijijini na elimu nyingine muhimu za ugonjwa huu sambamba na wajane na yatima. Nitafurahi kama maoni yako yalivyosema, nikutumie baada ya kushoot, kisha editing ifanywe huko. Mimi niko tayari na nitafurahi kama utaniunga mkono.

    ReplyDelete
  3. Anonymous10:50:00 AM

    Philly nilitazama senema yake ilipotoka. Wakati ule ukimwi ulikuwa kama hadithi fulani hivi. Yeye ni watu wa kwanza kwanza kabisa wa Afrika kujitokeza hadharani. Kuna maswali fulani uliwahi kuuliza kuhusu ukimwi na waafrika. Muda tu, nilitaka sana kuchangia zaidi. Nakumbuka nilikulengesha kwa Nkya ambaye anafuatilia kwa karibu masuala haya.

    ReplyDelete
  4. Sinema ya Phil Lutaya niliiona Arusha enzi zile, nakiri ilikuwa ndiyo sinema yangu ya kwanza juu ya ukimwi. Ilinisukuma sana, pamoja na wanafunzi wote wa pale Ilboru tuliokusanyika lecture theatre.

    ReplyDelete
  5. hata mie sinema ya philly niliiona. ila sema tulikuwa tunaona kama aibu kuonekana kuishabikia. vile vile bonny kumbuka ni katika muda ule ule ambapo dakta remmy ongalla alizua rabsha na wimbo wake wa 'mambo kwa soksi'. nasikitika rekodi hiyo nasikia imetupwa na kwa afya (na itikadi ya dini) aliyo nayo dakta remmy sidhani kama ataweza kuupiga tena ukanoga

    ReplyDelete
  6. Michuzi umeibua hoja ambayo inaonekana kunyong'onyea miongoni mwetu. Serikali yetu mara nyingi inakuwa na watu wengi wana vichwa kama umbo tu lakini ndani yake ama ni vacuum tu ama kuna uji wa ulezi. Hivi kulikuwa kuna haja gani ya kuupiga marukufu, sorry marufuku, wimbo wa Dk.Remmy Ongala Mtoro? Tena isitoshe aliimba kwa mafumbo tu. hakutamka neno 'kondom'.

    Ingawaje ni takribani miaka 15 au 16 sasa tokea niusikie kwa mara ya mwisho. Sehemu ilikuwa-ga hivi:

    Dude hillooo (kwa soksi)
    Likikuvaa (kwa soksi)
    Unaondoka (kwa soksi)
    Na kilo mbili (kwa soksi)
    Bila kitambi (kwa soksi)

    Labda nimekuwa ama kipofu (siwezi kusikia) ama kiziwi (siwezi kuona) lakini silioni baya lolote katika wimbo huu. Leo usiku na mchana hao hao vichwa vacuum wanapigia chapuo kondom tena wao sio kwa tafsida kama Remmy Mtoro.

    Michuzi RTD wanao wimbo huu. Ni wakati sasa uchezwe hadharani upya ili mjinga tumbaini kati ya serikali na Dk Mtoro.

    ReplyDelete