Friday, April 13, 2007

IJUMAA YA TAREHE 13!


Leo kuna watu hawatoki majumbani kwao,hawayagusi magari yao,hawatizami luninga zao,hawali samaki wenye mifupa,hawatoki hata kitandani.Kisa? Leo ni Ijumaa yenye kubebwa na tarehe 13,tarehe ambayo imani za (sijui niziite za kishirikina?) zinatabiri kwamba leo ni siku mbaya kabisa.Ukitoka utapata ajali,jambo baya sana litakutokea aidha wewe au wanajamii wako.

Imani hii imesambaa zaidi kwa jamii za waingereza,wajerumani na wareno.Wagiriki na wahispania wao wanaiogopa zaidi Jumanne yenye tarehe 13.Siku hii ya ijumaa 13 inabebeshwa lawama kutokana na mambo kadha wa kadha ya kihistoria.Wanaoigopa siku hii wanasema mgeni wa kumi na tatu,Yuda Iskariote, ndiye alipelekea kufa kwa Yesu, siku ya ijumaa. Wanasema yule mama yetu wa kwanza yaani Eva alimpa Adam "tunda" siku ya ijumaa.Wanasema Abel(mtoto wa kwanza wa Adam na Eva) aliuawa na kama yake Kain siku ya Ijumaa(hivi ushawahi kujiuliza kama watoto wa binadamu wa kwanza wote walikuwa wa kiume,dunia iliongezekaje baada ya hapo?)

Wachumi wanatabiri kwamba takribani dola za kimarekani milioni 900 huota mbawa kwenye ulimwengu wa biashara siku ya leo kwa sababu ya hofu ya siku hii kwa sababu watumiaji,wanunuzi wa bidhaa na huduma leo hawatoki majumbani mwao nk.

Sasa hizi ni imani za kizungu.Sisi waafrika tunazo zetu,unazikumbuka zipi?Mimi nazikumbuka kadhaa, ukikojoa vichakani unaambiwa titi la mama yako litakatika, ukiona mvua inanyesha huku jua linawaka unaambiwa ujue simba anazaa.Ukimruka mtu lazima umruke tena ama la atakuwa mfupi.Ukimcheka mkweo utaota kisenene kwenye jicho.Hapo sijataja zile imani kwamba fulani akioa kutoka ukoo fulani au kabila fulani basi mambo yatakuwa vinginevyo.Unazikumbuka zipi?Unadhani imani hizi zina ukweli ndani yake au ni ushirikina na hofu zetu kama wanadamu tu?Ijumaa 13 njema!

6 comments:

  1. Anonymous7:12:00 AM

    Jeff acha uchokozi hapa ulipouliza:
    (hivi ushawahi kujiuliza kama watoto wa binadamu wa kwanza wote walikuwa wa kiume,dunia iliongezekaje baada ya hapo?)!

    Halafu Jeff, najua jibu ambalo utapewa. Tusubiri tuone kama kuna atakayejibu. Kisha tuendeleze majadiliano na huyo ndugu.

    ReplyDelete
  2. Anonymous7:17:00 AM

    Jeff:
    Nimependa hili wazo la kujadili imani ambazo tumekuwa nazo. Naamini wengine watachangia maana zinatukumbusha mbali.

    Zipo imani kama hizi ambazo kazi yake ilikuwa ni kufunza heshima na adabu. Unaona kama hiyo ya kukojoa kichakani kazi yake ilikuwa ni kutunza mazingira. Kuna nyingine ilifanana na hiyo ambayo ilisema ukimchungulia mtu mzima akijisaidia titi la mama litakatika.

    Nyingine:
    ukimuona zeruzetu lazima utemee mate kifuani.

    ukiweka ndulele golini timu pinzani haitafunga

    ukibinya korodani wakati wa penalti, timu pinzani itakosa goli

    ukisema jambo baya, tema mate ili kupitiliza mbali (jambo hilo lisitokee)

    ReplyDelete
  3. Anonymous8:46:00 AM

    Ndesanjo,
    Asante kwa kutukumbusha hizo imani nyingine.Hiyo ya kubinya korodani nadhani ilikuwa inafanya kazi,au unasemaje?
    Hilo la binadamu wa kwanza hata mimi nina hamu ya kupatiwa elimu yake maana huwa najiuliza sana swali hili.

    ReplyDelete
  4. Ah! Jeff,
    Inafurahisha, lakini huu ni mjadala muhimu. Maana nasikia hata wazungu hawapiti chini ya ngazi wakiamini hali hiyo inaleta mikosi. Haya ni mambo ya kibinadamu

    ReplyDelete
  5. Jeff, Ndesanjo,

    Kuhusu binadamu wa kwanza kuwa wanaume tu wala msikonde, kumbukeni enzi hizo na mpaka leo sehemu zingine wanawake hawahesabiwi kwa sababu na visingizio mbalimbali, kama hilo ni jambo baya au zuri sasa huo mjadala mwingine.

    Kwa mfano wa Wayahudi(maana Jeff umelenga kwao kuhusiana na Kaini na Habili) kuanzia yale makabila yao utaona ni majina ya watoto wa kiume tu, wa kike pamoja na kuwa ni damu yao hawatajwi ng'o.

    Koo zao ukisoma Biblia utaona Obedi kamzaa Yese, Yese kamzaa Daudi, Daudi kamzaa Sulemani, n.k. wanawake hawatajwi ila kwa nadra sana lakini kama wote tujuavyo wanaume hawazai peke yao.

    Kwa mantiki hiyo kusema kuwa Kaini na Habili ndio watoto wa pekee wa binadamu wa kwanza siyo sahihi.

    Natumaini nimejibu swali.

    ReplyDelete
  6. Anonymous11:26:00 AM

    Patrick,
    Umeeleweka lakini bado kuna jambo.Ina maana katika wakati fulani kaka ilibidi alale na dada yake ili kuongeza ulimwengu?

    ReplyDelete