Kama kuna faraja yoyote ambayo nimeipata tangu nilipoiweka hadharani picha ya watoto-wanafunzi waliokalia mawe hivi majuzi (kama hujui nazungumzia nini bonyeza hapa) ni jinsi gani sote tumekerwa na kudhamiria kufanya kitu ili kubadili hali hii.Maoni yaliyomiminika, simu mlizonipigia baadhi yenu, barua pepe mlizonitumia zilitosha kunihakikishia kwamba vita hii inawezekana kupiganwa.Tunachohitaji sasa ni kuazimia kuianza rasmi. Serikali zetu, tawala na zote zilizopita haziwezi kukwepa lawama kwa kushindwa kwake vibaya katika kuleta mabadiliko ya kijamii yanayostahili,yaliyo ya haki na yanayotarajiwa.Tunapoongelea serikali tunaongelea suala zima la uongozi.Tunakuwa na viongozi ili sio tu kuheshimu dhana nzima ya demokrasia bali pia kupata watu wa kutusaidia katika kuijenga dira, kuleta mabadiliko ya kijamii, na kuzivusha jamii zetu kutoka upande mmoja mpaka mwingine.
Picha ya watoto-wanafunzi waliokalia juu ya mawe, ndani ya jengo chakavu kabisa huku wakionekana na kuwa na kila dalili ya njaa, ukosefu wa matumaini na ambao inaonekana jamii imewasahau imetukera, imetuhuzunisha na kutukumbusha wajibu mzito tulionao kama watanzania.
Ukiwauliza jamaa wa serikalini,viongozi,wabunge,mawaziri nk hawatokosa majibu. Hiyo ndiyo sheria ya kwanza ya taaluma ya siasa. Usishangae pia ukisikia lawama zikienda kwa wafadhili, IMF na Benki ya dunia na mara nyingine kwa kufoka kabisa,wakiwatupia wananchi lawama.Imeshatokea hata mwananchi kukabiliwa na kifungo kwa sababu alimuuliza mbunge wake swali gumu!
Japokuwa naafiki kuna mantiki fulani katika kuzitupia lawama jabali hizo za masuala ya fedha duniani kuhusiana na mustakabali mzima wa maendeleo, zaidi naamini kwamba wanasiasa na viongozi wetu siku hizi wanazitumia zaidi kama ngao ya kukwepa lawama na majukumu tu.Yapo mambo chungu mbovu ambayo yanawezekana bila kutegemea ufadhili wa mtu au nchi yeyote.Mbona hata hayo hayafanyiki? Tuna viongozi kweli? Kama serikali yetu inatoza kodi, inapiga tambo za kukua kwa uchumi na wakati huo huo inaweza kuwapatia viongozi wake vitendea kazi vyenye thamani kubwa mara dufu kushinda sio tu kipato chao bali pia kipato cha taifa, inashindwa vipi kuhudumia sekta muhimu kama ya elimu?Tunapata wapi fedha za kutupa kwenye kashfa nzito kama Richmond na ununuzi wa rada lakini tukashindwa hata kuwachongea wanetu madawati achilia mbali kuwapatia walimu na vitendea kazi vingine?
Tufanye nini? Hili ndilo swali ambalo hatuna budi kusaidiana kulijibu kwa pamoja. Jambo la kwanza ambalo naamini tunaweza kulifanya ni kutochoka kuhoji,kukemea na kusaidia kwa kutoa mchango wetu wa hali na mali. Tusiishie kuandika tu huku kwenye mitandao na wakati mwingine kutupiana lawama hata miongoni mwetu sisi wenyewe.Jambo moja ambalo ni muhimu sana ni kumuuliza mbunge kwa mfano wa jimbo hilo la Morogoro Kusini Hamza Abdallah Mwenegoha kwanini hali katika jimbo lake ni ya kukatisha tamaa na kutia aibu kwa kiwango kile? Binafsi nimeshafanya hivyo kwa kumuandikia barua pepe nikiambatanisha picha ile na kuhoji kwa kina,kulikoni? Ingawa bado sijapata majibu na pengine sitopata majibu kamwe nina uhakika kwamba ujumbe umemfikia na hivyo atatambua kwamba dunia inamtizama. Ukipenda kumtumia barua pepe pia unaweza kwa kutumia anuani ya hmwenegoha@parliament.go.tz
Usiishie kwa Mwenegoha peke yake bali pia mbunge wa jimbo lako, kule utokako au kule ilipo familia yako,asili yako nk. Kwa bahati nzuri anuani za barua-pepe,simu za nyumbani, za ofisini, za kiganjani za wabunge wetu zimeorodheshwa katika tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Utaratibu mwingine wa kusaidia ni ule wa hali na mali. Ingawa ni vigumu kujua taasisi gani tunaweza kuiamini na kupeleka mchango wetu huko, naamini tukiulizana miongoni mwetu tutapata majibu tunayoyahitaji.Tupeane habari, tubadilishane uzoefu.
Mwishoni baadhi yenu mliomba kuona kama ninazo picha zingine za shule hiyo ya Kibogwa.Picha inayoambatana na ujumbe huu ni Shule ya Msingi Kibogwa kwa nje.Double click kwenye picha uione vizuri.Picha na Mathew Membe na nimeipata kupitia kwa Yahya Charahani, mwanablog, mwandishi wa habari aliyeko Tanzania.