Leo siwezi tena kuomba msamaha kwa kutokuandika hapa mara kwa mara.Kama mnataka na mimi nijiuzulu kama waheshimiwa huko Tanzania….we acha tu.Vyeo vitamu bwana…si mlisikia wenyewe jinsi sauti za waheshimiwa zilivyokuwa zikitetemeka na kujaa mwangwi wakati wakitangaza kujiuzulu? Si mliona pia jinsi wengine hadi wake zao walivyoangua chozi?Unafanya mchezo nini? Hapo mimi ndipo ninaposhangaa,kama cheo au ukubwa unaupenda hivyo,kwanini usiwe mwadilifu basi?Eti kwanini? Kama wewe unajua kwamba hapa duniani unapenda kubebewa briefcase,unapenda kufunguliwa mlango wa gari na wa nyumba,unapenda kufungwa mkanda kama vile mtu uliye hoi kitandani,kwanini unaleta uzushi na uzabinabina unapokuwa madarakani?
Okei,sasa jamaa wametangaza kujiuzulu,mkuu wa nchi kakubali maombi yao..what next? Next ni kwamba jamaa bado wapo bungeni,tena bado wanachangia mijadala.Hii ndio bongo bwana.Changa la macho kama kazi. Hivi si ni ajabu kwamba unapojiuzulu,baada ya kukumbwa na kashfa nzito kama ya ufisadi,ubunge nao unatakiwa ukome mara moja? Mpiga kura gani anataka kuendelea kuwakilishwa na “fisadi’. Halafu Tanzania hamna hata ile sheria ya kuweza kum-recall mbunge.Yaani mkishamchagua,mnalo kwa miaka mitano.Linakuwa tsunami lenu tena. Halafu huko bungeni aliyemwaga manyanga jana leo anachangia na kusema Rais amechagua “mtu kama mimi”.Yaani wazi wazi kabisa mtu anasema,mmeuvaa tena mkenge.Na anapigiwa makofi na virungu! Ee bwana ndio…hii ndio bongo…kila mtu inabidi ajifanye hamnazo ili angalau kesho aweze kuamka na kwenda kazini. Hebu kwanza cheki hapo kama umeme upo bado au ushakata na kompyuta yako inatumia ule wa kudandia tu unaposoma habari hii.
Haya sasa,PM mwingine huyooo..anajinadi..anasema yeye ni mtoto wa kwanza(hata sijui hii inahusiana na nini).Anasema yeye ni mtoto wa mkulima.Alikuwa au bado ni mtoto wa mkulima? Kiswahili lazima tukitanue wajameni.Ahaaa…kumbe huyu naye anatoka pale pale…yaaani pale pale kwenye ofisi ya waziri mkuu! Halafu sura ni miongoni mwa zile zile.Bila woga na yeye anasema kumbe keshakaa sana pale ikulu..yaani anapajua kuliko hata nani sijui. Sasa hapo ndipo utakapochoka…kumbe sasa nini kipya hapa? Hapo hujazingatia jinsi mambo yalivyokwenda fasta? Hivi unataka kuniambia mambo yote haya,kimstakabali wa nchi..nasema nchi sio kijiji,yanafanyika ndani ya masaa kama 16 tu?? Kama ni kweli basi nchi yetu inastahili medani ya hali ya juu sana kwenye suala zima la disasters preparedness.
Wale wanaoitwa wapinzani…masikini hawa nao naona wamepigwa ganzi kiaina.Yaaani hata kuguna hawakuguna! Ingekuwa mimi ningesema haya ninayoyasema hapa.Eti nini…anaitwa nani?Pinda? Ofisi ya nani..Waziri Mkuu?
Sasa subiri baraza jipya la mawa-siri.Hapo ndipo utaweza kuthibitisha hizi hoja zangu.Kama unabisha tizama kama yule jamaa mwenye jina linalohusiana na vita vya majimaji hatarudi tena kwenye “kebineti”.Ni kama vile hakuna watu wengine wanaoweza kuwa mawaziri na manaibu waziri.Utasikia tu.Tena nasikia ule msururu wa mawaziri unarudi tena,tena na zaidi.Hii ndio bongo.
Aisee ukiona kimya sana hapa usidhani nimetoweka duniani..huwa pia naandika pale http://bongocelebrity.com.
Hadithi za chaguzi zisizo huru barani Afrika zinazidi kuwa kama vile hadithi za kila jioni alizokuwa akitusimulia bibi wakati wa utotoni. Si unakumbuka zile;jioni baada ya msosi bibi anawaweka pembeni ya moto na kutupigia hadithi tamu.Wakati mwingine tulikuwa tukisinzia kutokana na uchovu na wakati mwingine hatukuthubutu hata kupekua kope kwa jinsi hadithi zilivyonoga.Binafsi nilikuwa natoa macho zaidi kama hadithi inakuwa ya kutisha tisha hivi.Uoga!
Tofauti ni kwamba hadithi za bibi zilikuwa na mafunzo tele.Kila jioni tulipenda kuzisikia kwani zilitupa maarifa na elimu ambayo Mwalimu yeyote yule shuleni asingeweza kutupa.Kwanza walimu walikuwa wanapenda sana mchezo wa kuchapana.Ukikosea kidogo tu,unacharazwa viboko.Nadhani walikuwa wanatumia staili ya kimarekani-kutishana,kupigana mkwala ili kuzibana mdomo na kuendelea kutawala.Lakini si unakumbuka jinsi na wewe ulivyokuwa mjanja kwa “kujaladia”? Hujaelewa? Namaanisha kuvaa nguo kadhaa ndani ili viboko vifanye kudunda tu…Okay nasema hadithi za bibi zilikuwa hazichoshi.Hizi habari za chaguzi zisizo huru zinachosha. Kama hujachoka kuzisikia ni wazi umekuwa ukiangalia zaidi sinema badala ya taarifa za habari.
Kinachotokea nchini Kenya hivi sasa ni mwendelezo tu wa wizi wa kura na demokrasia.Ndio maana jamaa mmoja amesema labda demokrasia sio mambo ya kwetu.Hatutaki au hatutakiwi kuwa na demokrasia. Huyu tumemjia juu,tumemuuliza mbona hata huko kwa bwana mkubwa (US) raisi wao hakuchaguliwa na wananchi bali mahakama? Sasa nani wa kumvalisha paka kengele?Mwai au Kichaka?Hapo ndipo mchezo unapokuwa mgumu.Si ndio maana mumewe Lucy kakataa hata kufuata ushauri wa yule mwakilishi? Mwakilishi alipofika na kushupaza mishipa kwa mumewe Lucy,jamaa akacheka sana.Akamwambia look who is talking.Likawashuka!
Sasa ni jinsi gani mtu anaiba uchaguzi?Kama ulifuatilia kilichojiri Kenya, ni wazi utakuwa umepata picha mbaya kuliko.Hata negative huwa haipo hivyo.Kilichofanyika pale ni uhuni,wa wazi wazi kabisa.Halafu jamaa wakasimamisha ndude zao wakasema “mwanaume kweli apite mbele”.Jamaa wanavyoogopa habari za “popo bawa” wote wakanywea.Ngoma bado mbichi.Kitakachotokea jumatano ijayo tunasubiri kuona. Lakini nahisi hata kule kwa bwana Madevu aliyeuawa bila kwa hatia hiyo hiyo ya wahukumu na wanyongaji wake kutakuwa salama.
Hata twende sasa. Ukitaka kuiba uchaguzi au kura kwanza unachotakiwa kufanya ni kuchagua mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ambaye ni swahiba wako.Kisha unampa maelekezo kwamba makamisaa wote wawe ni watu mnaojuana.
Pili wale ambao unadhani watapigia kura wapinzani wako unawaundia kesi.Kesi za kutunga zipo kibao.Msingizie kwamba kachukua rushwa au kabaka vitoto vidogo.Yeye na wanae wote.
Tatu kwenye daftari la wapiga kura weka majina unayoyajua wewe.Waliokufa,walio chini ya umri wa kupiga kura nk…wote twende kazini.
Jamaa wa nje wakisema wanaleta wasimamizi wa kimataifa waambie kumeshajaa.Hakuna nafasi.Waambie tayari unao wasimamizi wa kutosha.Wakikuuliza wanatoka wapi usiwafiche.Waambie ukweli kwamba wasimamizi wako wanatoka China,Urusi,Iran,Zimbabwe nk.
Kisha tumia watu kama wanajeshi na wanausalama.Wote hawa siku hiyo wapigishe kura hata kama sheria inasema vinginevyo.Si unajua kule ni amri kwanza maswali baadaye?Eenh fanya kweli hapo.
Usisahau kuongeza “vituo vya kupigia kura” viwe maradufu.Weka vituo mpaka kule ambako una uhakika hakuna mgeni yeyote anaweza kuthubutu kufika.Kule Ngalilo ndani ndani huko.Sema kuna wananchi kibao huko wamekuchagua kwani wanasema umewapelekea maendeleo mengi sana.Umepeleka vyandarua huko kwa sana tu.
Kama vyote hivi vinashindikana basi fanya kama mumewe Lucy.Mwambie mshikaji wako atangaze kwamba umeshinda.Kisha,bila kuchelewa, jiapishe.Usisubiri upuuzi wa kualikana kwa ajili ya sherehe za kuapishwa zilizo na gwaride na hotuba ndefu.Za nini?Wakati huo huo uwe ushaagiza kwamba hakuna matangazo ya tv na redio zaidi ya yale ya washikaji wako wa karibu kwa ajili tu ya kutunza historia ili vijukuu vyako siku za mbeleni vijue babu alikuwa mtemi.Mchezo unakuwa umekamilika.
Vipi wewe? Sherehe za xmas ulizisheherekea vipi?Mwaka mpya umeuanzaje?Hapa nilipo ni baridi mtindo mmoja.Wakati mwingine unatamani uishi ndani ya friji ili ujue moja.Huu ndio ule wakati wa korodani kunyweeea.Kama huna nguvu ya ziada,kazi kwako.Unaweza paniki ukakimbilia kale ka kidonge kanakoanzia na herufi V.Nyakati nyingine huwa najiuliza kama ulikuwa mpango wa Mungu watu waishi upande huu wa dunia.Nasema hivyo nikizingatia jinsi zama hizo zilivyokuwa.Hakuna nguo za sufi kama tulizonazo hii leo,hakuna magari yenye vileta joto kama hivi leo.Hakuna nyumba zilizo na majiko ya humo kwa humo.Sasa waliishije hao watu wa mwanzo huku?
Kwa upande mwingine,hainishangazi kusikia zile habari za kisayansi na historia kwamba fuvu la kale kabisa lilipatikana kule Tanzania.Naam..kule kunafaa kuishi,ndio mpango wa Mungu.Ajabu sisi wenyewe hatujui uzuri wa kwetu.Tukiona vinaelea tunadhani vimeshushwa..kumbe.Ndio maana profesa mmoja aliwahi kuuliza Waafrika Ndivyo Tulivyo? Wengine wakamjia juu...sijui walikuwa wanafikiria nini.Hata hivyo kwetu kunabakia kuzuri.Kwetu unaweza ukalala mzungu wa nne na wala usikauke kwa baridi kali.Tatizo mbu watakavyokutandika..utakoma.Hutorudia tena.
Sasa usije ukadhani sipendi kabisa kuishi huku.Ama!Ughaibuni kuna raha zake.Karaha nazo zipo lakini wenzetu wanajitahidi sana kila siku kuzidhibiti.Mpaka kahawa unaweza kununua ukiwa umekaa ndani ya gari yako tu.Kama sio uvivu ni nini hicho?Halafu wenyewe wanashangaa kwanini wananenepeana kama viboko.Kila unachokiona kwenye luninga ni kuhusiana na unene vs wembamba.Mwaka mpya unapoanza kama hivi,mamilioni ya watu(hususani wanawake) wanadhamiria kupunguza uzito wao.Yaani huku mwanamke asiye na nyama au minofu ndio anayevutia zaidi.Haingii akilini hii..au sio? Kama nakuona vile.Huku ughaibuni husikii kitu umeme umekatika wala maji.Ukifungua bomba...hayoo..meupee.Umeme ukikatika inakuwa ni breaking news.Utawasikia wazungu..can you believe this?Nami nawajibu..I know..I can’t believe this!Kichwani nawaambia..mngejua kwetu umeme unakatika kutwa mara sita na wakati mwingine unakaa hata wiki bila kurudi na bila kusikia neno lolote achilia mbali samahani kwa wahusika,mngebana ngenge.
Enewei,nakutakia kheri ya mwaka mpya.Tusukume sote gurudumu la maendeleo...hata kama limekwama kwenye lindi la tope zito.Kabla sijasahau,umesikia ahadi kutoka kwa wapinzani nchini Tanzania?Wamesema huu ni mwaka wa kupigania katiba mpya nchini Tanzania.Katiba iliyoandikwa na wananchi na sio hii yenye harufu mbaya ya kikoloni na sisi kwa ujuha wetu tunaishia kuweka viraka tu kila kukicha! Wapinzania wanataka pia tume huru ya uchaguzi.Hii ya sasa ndio kama hivyo ilivyo.Haina meno,jaji wa serikali ndio mwenyekiti wa tume.Kwani hujasikia yaliyotokea huko Kenya?Mwenyekiti wa Tume anasema eti alipomtangaza mshikaji wake Mwai Kibaki kuwa mshindi alikuwa “under pressure”.Msalie mtume,hivi lini tutastaarabika sisi?Wenzetu wakitushangaa eti tunakasirika,tunawaita wabaguzi na wachimba chumvi.Mitusi inayotutoka huku mishipa yote ya fahamu ikiwa imetutoka,sio ya kawaida.
Kheri ya mwaka mpya msomaji.Kama unapenda uandishi wa namna hii niambie niendelee.Nimechoka ule uandishi wa kiprofesa.Simple 2008.Ndio azimio langu.
Mwaka mmoja uliopita wanablogu wa kitanzania tuliweka historia mpya.Siku kama ya leo,yaani tarehe 18 Novemba 2006 kuanzia saa sita mchana kwa saa za Tanzania,wanablogu wa kitanzania tuliotapakaa dunia nzima tulikutana kwa minajili ya kuunda jumuiya yetu rasmi na kuwa na siku ya blogu Tanzania.Katika mkutano ule tuliipitisha rasmi siku ya tarehe 18 Novemba kila mwaka kuwa siku ya blog Tanzania.Kwa maneno mengine,leo ni Tanzania Blog Day.
Naikumbuka vyema siku ile kwani sio tu nilidamka asubuhi na mapema(ili niwahe mkutano uliokuwa umetegwa kwa masaa ya Tanzania ingali nipo Canada) bali pia sote tuliohudhuria mkutano ule tulikuwa tuna shauku ya kuunda jumuia ambayo italeta mabadiliko ya kijamii hususani kuhusu jinsi tunavyopashana habari na pia kuchangia katika uundwaji au ubomoaji wa sera za nchi.Huo ndio muelekeo wetu ambao nina uhakika bado tunalo jukumu la kuuendeleza kwa hali na mali.Siku ile sote tulikuwa na mioyo ya kimapinduzi na upendo wa aina yake kwa taifa letu,jamii zetu na dunia yetu kwa ujumla.
Usingeweza kututofautisha na kina Fidel Castro,Che na wenzao walipokuwa wakipanga mikakati ya kimapinduzi enzi zile.Tofauti kati yetu na wao ni kwamba wao walikuwa na silaha za wazi wazi kama bunduki na mijeledi.Sisi tulichokuwa nacho na ambacho naamini bado tunacho ni uhuru wa kupashana habari na kuwasiliana kwa minajili ya kuleta mabadiliko ya kijamii.Hii ndio jamaa wa Global Voices wanaiita Blogging For Social Change!Ingekuwa zamani tungesema tulikuwa tunachukua ule msimamo kwamba A Pen is Mightier Than A Sword.Tatizo ni kwamba zama hizi zinatumia zaidi “keyboard”kuliko kalamu ya kawaida au Bic kama wengi wetu tulivyozoea enzi zile.Kwani mmesahau kwamba kuna wakati tulikuwa tunahitimu kutumia penseli na kisha tunahamia kwenye kutumia bic?Hivi ilikuwa darasa la ngapi vile?
Tungekuwa tunaenda kwa ule mwendo wa kichama chama, leo ingekuwa ndio siku ya gwaride,mapambio,mashati au t-shirts za rangi za vyama,hotuba,vipeperushi, ahadi na mambo kama hayo. Tungekutana pale bwalo la maofisa na kutumia fataki za ule mvinyo wa kizungu(champagne) utadhani tumeshafanikiwa kuitokomeza vita ya njaa,maradhi na umasikini.Ungetuona usingedhani kama tunaishi kwenye nchi yenye raia kibao wanaolala njaa,wanaolala nje,mitaani,chini ya magari,yenye raia wengi wanaopoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma za afya na kero zingine chungu mbovu.Hapo sijataja wanaopasua kichwa badala ya mguu.Hebu tuachane na hayo,ngoja niendelee na ajenda ya leo ili nisije nikakukwaza ndugu msomaji bure.
Baada ya mkutano ule wa kihistoria tulichagua viongozi.Palikuwa na kampeni,japo za chini chini,tukapata fursa ya kukagua wasifu wa baadhi ya wagombea nk.Demokrasia ikachukua mkondo wake,tukapata viongozi.Hapakuwa na shampeni wala ulanzi lakini sote tulifurahi na bado tunafurahi kwamba tunao viongozi.Lakini nisingependa tusahau kwamba hata kabla ya kukutana rasmi na baadaye kupata viongozi,kuna wakati tulishapata “Azimio la Dodoma”.Si unakumbuka tulivyowekeana maadili ya maana?Tatizo wale jamaa waliokutana Dodoma na baadaye sisi kuamua kulikubali azimio lao,wote wamepotea kwenye ulimwengu wa blog hivi leo.Blog zao zimeanza kuwa kama zile ofisi za masijara za ile wizara pale karibu na wanaposhinda kutwa nzima vijana wanaoojiita “misheni tauni”.Najiuliza hapa,hivi nikiwatajia yale majina ya wana-Dodoma mtanisaidia kuwauliza nini kimewasibu?Au na wao kuna mlungula umetembea ili kuwazima?Sijui.
Pamoja na kupata viongozi na matumaini mapya,leo naomba nisiwe mnafiki bali niseme wazi kwamba,kuanzia pale mambo kwa kiasi fulani yakaanza kwenda taratibu mno.Sababu zaweza kuwa nyingi na tofauti.Lakini ukweli utabakia(kwa mtizamo wangu) kwamba kuna kasi imepotea ambayo hatuna budi kuirudisha kwa kasi pia.Mfano mzuri ni jinsi ambavyo siku hii ya leo tunaikumbuka.Si unakumbuka kwenye mkutano kuna jamaa aliniahidi kwamba leo atanipa mvinyo tani yangu?Au wewe umesahau?
Yote tisa,kumi ni swali ambalo leo limegubika moyo wangu.Swali hilo ni je wangapi kati ya wanablogu waliohudhuria mkutano ule na hata wale ambao hawakuhudhuria lakini baadaye wakatambua yaliyojiri mkutanoni siku ile wanaikumbuka siku hii muhimu?Na je mbona viongozi wetu hata hawakuchukua jukumu la kuikumbusha jamii kuhusiana na siku hii?Nini kimetokea?Kama na wewe msomaji wangu umesema,ah hivi kweli eenh,todei wi wea sapozidi tu rimemba endi selebreiti bulogu dei,basi jua tuna tatizo.Mimi na wewe.Wala usipande darini ukadhani utakuwa salama.Kunguni wako kila sehemu,shauri yako.
Kwa mfuatiliaji wa maendeleo ya blogu za kitanzania,atakubaliana na mimi kwenye jambo moja muhimu.Msisimko uliokuwepo hapo mwanzo mwanzo,haupo tena.Unazikumbuka enzi zile za kumkaribisha kila mwanablogu mpya kwa maneno matamu na ya kutiana moyo?Kila mtu mpya “alipokata shauri” na kuamua kufungua blogu sote tulifahamishana.Tukachukua dakika chache za kukaribishana na kutakiana heri.Tulikuwa na ujamaa wa aina fulani ambao binafsi niliupenda sana.Mpaka leo hii napata faraja nikitembelea “post” yangu ya kwanza kabisa na kuona jinsi wanablogu walioanza kabla yangu walivyonikaribisha na kunitakia kheri.Whati hapenedi?
Ni wazi kwamba tunafanya makosa.Tunafanya makosa ya kuzipuuza zama hizi mpya za mawasiliano ya umma(mtazamo wangu).Kwanza sitaki kuamini kwamba tunazipuuza au tumeanza kuzipuuza. Sitaki kabisa kuwaza namna hiyo kwani nikifanya hivyo siku si siku itabidi mnipeleke Dodoma.Wenzetu,kwa mfano wakenya na waganda wanaendelea kuzikumbatia zama hizi kwa marefu na mapana.Sisi bado tunaenda kwa mwendo wa kinyonga.Tuna haja ya kuanza tena kukimbia.Tuna kila sababu ya kuzidi kuungana,kuzidi kuwaalika watanzania wengine wenye maarifa tofauti tofauti kufungua blogs zao,tena za Kiswahili ili sio tu tukuze lugha yetu bali tuongee tuelewane.Tusipofanya hivyo tunazidi kuwaachia wenzetu fulani fulani,wa ndani na nje ya nchi,waamue mustakabali wa maisha yetu.Nasema hivi kwa sababu moja,usiposema kupitia kwenye mawasiliano ya umma kama blogs,utasema kupitia wapi?Kwenye pishi la pilau na kanga kutoka barahindi?
Ubaya au uzuri wa zama mpya mara nyingi huwa zinahitaji kuoteshwa ili baadaye ziweze kuota mizizi na kutupa matokeo tunayoyahitaji.Raisi Museveni wa Uganda ana kitabu chake kizuri sana kinachoitwa Sowing The Mustard Seed(ukikipata kisome).Jukumu hilo la kuotesha ni letu sote.Viongozi kazi yao ni kutuongoza tu,watendaji ni sisi sote.Tusikubali kutupa mti na jongoo wake. Kama umekaa pembeni ukisubiri wenzio wakuoteshee mbegu kwanza unafanya lisilo jema.Fikiria upya.
Mwisho naomba niwatakieni wote Happy Tanzania Blog Day.Najua hata kama hakuna shangwe na vigelegele mwaka huu,basi mwakani huenda tukawa nao.Tutazichagua blog bora na kuwapa waongozaji wake japo bilauri ya mpingo ili wakanywee ndani yake wakikumbuka kesho yake wanatakiwa kuendeleza libeneke kama rafiki yangu Issa Michuzi anavyopenda kusema.Tuko pamoja ndugu zangu katika blogu.Nalia lakini..usinione hivi.