Saturday, March 31, 2007
MTAANI
Ukitembelea jiji la Toronto utakuwa hujakamilisha matembezi yako kama hutotembelea mtaa maarufu wa Yonge ambao unasemekana ndio mtaa mrefu kupita yote duniani.Halikadhalika ukitembelea jiji la Chicago (kule Michael Jordan alipojipatia umaarufu mkubwa wakati akichezea timu ya mpira wa kikapu ya Chicago Bulls) utakuwa hujakamilisha ratiba usipotembelea Michigan Avenue kama unavyoonekana pichani.Na ukiwa jijini Dar-es-salaam halafu usikatize Samora Avenue (zamani Independence) utakuwa umekamilisha ratiba?
Wakati huo huo hebu soma habari ya askari aliyekutwa uchi baada ya kumbaka mahabusu binti wa miaka 15 ambaye alikuwa mahabusu kwa madai ya kumuibia mwajiri wake.Tafakari,binti wa miaka 15 tayari alishakuwa na "mwajiri".Hivi huyo aliyekuwa mwajiri wake naye hana kosa la kuajiri mtoto?
NB:Picha haina mchanganuo (resolution) wa kutosha kwa sababu ilipigwa tokea ndani ya gari kupitia kioo cha upepo.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:17 AM


|
Permalink |
Wednesday, March 28, 2007
MUGABE NI DIKTETA?
Natizama nje kupitia dirisha langu ili kupata mandhari ya nje katika asubuhi hii inayoelekea kuwa na kila aina ya wema. Jua la asubuhi linaangaza kuashiria hali bora ya hewa katika kipindi hiki cha mvua hapa Canada. Mkononi nimeshikilia kikombe cha chai ili kuchangamsha kinywa kabla ya kuingia katikati ya jiji kutafuta. Nimefungulia luninga kwa sauti kubwa ili niweze kusikia taarifa za habari za asubuhi. Huwa napenda kusikiliza taarifa za habari ingawa najua mara nyingi huwa zimejaa ghadhabu na chumvi nyingi zenye kuvunja moyo. Leo sina bahati,nasikia wakimuongelea Robert Mugabe, hawasiti kabisa kumwita "Dikteta Robert Mugabe".Hivi kumbe...alah!
Ghafla najishtukia nikijiuliza swali lililopo kwenye kichwa cha habari hapo juu.Swali hili linazidi kuniwia gumu kulipatia jibu/majibu siku baada ya siku.Ugumu ninaoupata ninapojaribu kujibu swali hili nashindwa kuutofautisha na ule nilioupata nilipowahi kujiuliza kuhusu tofauti kati ya mpigania haki na uhuru na gaidi (terrorist). Eti Mandela alikuwa gaidi au mpigania uhuru alipokuwa na vijana wake wa Umkotho we Sizwe? Maswali kama haya yapo mengi sana,yote yanachosha na kuhemesha akili vibaya mno. Hivi Mugabe ni dikteta? Mbona kachaguliwa kwa kupitia sanduku la kura?
Mambo yanayoendelea nchini Zimbabwe hayapendezi hata kidogo.Lakini swali kubwa ni je yanatendeka Zimbabwe peke yake?Chaguzi zinazosemekana kutokuwa huru zinatokea Zimbabwe peke yake? Kwani hatukumbuki jinsi George Bush alivyoingia madarakani? Makamu wa raisi wa Bill Clinton, Al Gore siku hizi akijitambulisha anasema "I am Al Gore,I used to be the next president of the United States", unadhani anatania? Kama jibu ni hapana (naamini) tunao madikteta wangapi barani Afrika au duniani kote? Unadhani orodha hii ni timilifu? Ni nchi ngapi duniani zinazokandamiza upinzani kwa kutumia nguvu za dola za kila aina? Hivi ni nchi ngapi duniani zinazokandamiza uhuru wa kujielezea? Viongozi wangapi duniani wanaburuza tu wananchi na maamuzi yanayoumiza na hata kuua wananchi wao chungu tele?
Tunapochambua suala la udikteta viongozi kama George Bush tutawatofautishaje na kina Robert Mugabe? Kinachofanyika nchini Iraq ni ulimbwende? Wangapi tunakumbuka uongozi wa watu kama Marget Thatcher ulivyokuwa umetanda lawama? Jambo moja lililo wazi ni kwamba jamaa wa magharibi hususani Uingereza hawampendi kabisa Robert Mugabe. Ukiisoma vizuri historia ya Zimbabwe unaweza kutambua ni kwanini mambo yapo hivyo yalivyo. Usishangae basi kuona kwamba viongozi/madikteta wengi waliopo kwenye orodha kama hii hawatokei katika nchi za magharibi. Tafadhali naomba maoni yako. Unadhani haki inatendeka kwa ndugu zetu wa Zimbabwe kupitia propaganda za vyombo vya habari?Labels: Zimbabwe
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:31 AM


|
Permalink |
Wednesday, March 21, 2007
UMASIKINI HUU
Nilipoiona picha hii nilidhani ndani ya jeneza hakuna kitu mpaka nilipopata maelezo ya kina kwamba ndani ya jeneza hilo kuna mwili wa marehemu ambaye ni rafiki ya hao jamaa waliolibeba. Walipoulizwa kulikoni maelezo waliyoyatoa yanasikitisha;walisema rafiki yao amefariki na hawana hela ya kuusafirisha mwili wake kwenda kijijini kwao! Hayo yalitokea huko Democratic Republic of Congo (DRC)Haya ni matokeo halisi ya hali duni barani Afrika jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linasababishwa na uongozi mbovu unaombatana na sera mbovu na wizi wa mali ya umma.Picha kwa hisani ya Cedric Kalonji anayoblog kwa kifaransa.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:08 AM


|
Permalink |
Monday, March 19, 2007
NINI?
Hapa ni Toronto.Unaweza kuotea nini kilikuwa kinaendelea hapo?Jibu langu Ijumaa.Picha kwa hisani ya WVS Photostream.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 7:25 PM


|
Permalink |
Thursday, March 15, 2007
HIVI KWANINI?
Ukiniuliza kuhusu jambo moja ambalo linanikera sana kuhusu "ughaibuni" naweza nikawa na majibu kibao. Kutegemea na wakati naweza kukuambia kinachonikera hapa ughaibuni ni hadithi ya mtu kukuambia kwamba mambo yake safi sana kwa sababu amefanikiwa "kununua" nyumba bila kukupa ufafanuzi ambao utakupa jibu amefanikiwa "kukopeshwa" nyumba na wala sio kununua kama anavyojinadi.Deni hilo la nyumba atalilipa taratibu kwa zaidi ya miaka hata 20 au zaidi!Uwezekano ni mkubwa kwamba atastaafu (inategemea amekopeshwa nyumba hiyo akiwa na umri gani) na pengine hata kufariki akiwa bado anajikakamua kumaliza deni la nyumba. Deni la hapa halifutiki kirahisi, usipokuwa makini utarithisha watoto madeni.Hii ni tofauti kabisa na mahali kama Tanzania ambapo ukisikia mtu amejenga nyumba uwezekano ni mkubwa sana kwamba amejenga na hana tena deni na mtu. Nasikia siku hizi mikopo ya maisha kama hii huku inaanza kukua kwa kasi nchini Tanzania kutokana na utandawazi ambao umeleta mfumuko wa huduma za kibenki na mashirika mengine ya fedha.Kaa chonjo mwanakwetu.Lakini kama kuna jambo linanikera kupita yote ni jinsi ambavyo vyombo vya habari ya hapa visivyojua au kutaka kujua kuhusu lolote zuri kutoka nchi kama Tanzania,Zimbabwe,Zambia au kwa kifupi bara zima la Afrika.Nimewahi kuandika kuhusu jambo hili mara kadhaa,linanikera na litaendelea kunikera.Wazungu wengi bado wanadhani Afrika ni nchi moja.Nchi moja ndogo yenye kila aina ya matatizo kama njaa,vita,ukimwi nk.Mara nyingi wanaiongelea Afrika utadhani wanaongelea kijiji cha Ungekuwawewe. Ukisikia jambo lolote kuhusu nchi yoyote ya kiafrika basi ni kitu kibaya. Majuzi kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe alipokamatwa na kupigwa na polisi wa Mugabe sio tu ilikuwa ni habari kubwa hapa magharibi lakini ilikuwa ikirushwa kana kwamba bara zima la Afrika limewaka moto na ndivyo tulivyo. Najua ushaanza kujiuliza;Je naunga mkono mambo kama hayo yatokee na yasilaaniwe na wapenda haki,uhuru na amani duniani kote?Hapana, na tena binafsi nalaani ubabe wa namna ya serikali ya Mugabe ambao bado unaendelea kuwa adui wetu barani Afrika na hata magharibi chini ya utawala wa viongozi kama G.Bush wa Marekani. Pamoja na hayo ninachotamani mimi ni balanced news. Mwaka jana nilimuuliza news anchor mmoja maarufu sana hapa Canada kwamba kwanini wao wanapenda kuonyesha mambo mabaya tu kuhusu Afrika na wala wasionyeshe lolote jema?Jibu alilonipa ni kwamba "ndicho watu wanachopenda kuangalia/kuona".Nakumbuka kumwambia kitu kimoja,kama nyie weupe mnapenda sisi hatupendi na wala haitufurahishi na lazima waheshimu hilo. Bado ningali kwenye vita hiyo na bado sina uhakika kwamba kama ni kweli ndicho tunachopenda kuona.Mimi sipendi!Yapo mabaya chungu mbovu barani Afrika lakini pia yapo mema na mazuri. Tunaweza tusiyaone kwa sababu za kisaikolojia.Barani Afrika kuna upendo,watu bado wanasalimiana wakitaka kwa dhati kukujulia hali,wanatakiana kheri,wanatabasamu sio kwa sababu ndio masharti ya kazi zao.Watu bado wanasaidiana sio kwa minajili ya kupata unafuu wa kodi bali kwa sababu za kiubinadamu. Ukifiwa mahali kama Tanzania utaona ninachokiongelea,ukiwa na harusi au shughuli yoyote unachotakiwa ni kusema tu.Utasaidiwa.Hapa Canada nimeshahudhuria msiba uliokuwa na watu kumi na mbili tu. Nikimjua jirani yangu ni kwa sababu anataka kitu fulani kutoka kwangu au kinyume chake. Hali duni bado ni tatizo katika nchi nyingi za Afrika lakini hilo halijawazuia watu kuwa wakarimu. Ule usemi It Takes Village to Raise a Child bado una maana fulani katika nchi za Afrika(ingawa kuna ujuha umeingia wa kudhani kufanya hivyo siku hizi ni ushamba na kutokwenda na wakati). Hili huninyima raha kabisa kwa sababu wakati wenzetu wameshagundua kwamba waliwa wanakosea na washaanza kubadili muelekeo kwa kasi,sisi ndio kwanza tunaiga utamaduni ambao wenyewe wameshauona hauna mantiki.!Ndio sisi watanzania,ndio sisi waafrika.Jamaa mmoja ameandika kitabu na kuuliza ndio tulivyo?Ingawa miradi mingi inaliwa na wanaojidai wajanja(dawa yao ishachemka,bado kuwanywesha) ipo miradi ambayo inaendelea.Nadhani kilio cha wananchi wengi ni kwamba viongozi wapunguze uroho na ukibaka ili maendeleo yawe ya kasi zaidi ili serikali isiwe "tatizo letu" kama ilivyo hivi sasa.Wako vijana wenye muamko,walio na bongo zinazochemka,wavumbuzi.Wapo watu wenye utu,wanaojali jamii zao. Wapo watu ambao naamini uongozi ungewapa mazingira yanayoeleweka wangefanya miujiza.Zipo rasilimali ambazo ni vigumu kuzipata sehemu yoyote ile duniani zaidi ya ndani ya nchi za kiafrika. Tunayo mengi ya kujivunia na kwa maana hiyo vyombo vya habari vya magharibi vinayo mengi mazuri ya kuripoti. Vinapochagua mabaya tu tusikae kimya na wala tusijikombe.Hatujisaidii kwa kujidai hamnazo.Nani tumlaumu? Je, ni sisi wenyewe ambao tumekubali kuendelea kushikiliwa na minyororo ya utumwa wa kiakili? Je sisi ndio chanzo cha habari zote mbovu kuhusu nchi zetu?Ukiulizwa kuhusu nchi yako unasemaje? Unaanza kwa kuelezea mazuri (hata kama unadhani ni machache) au unaanza kwa kulia njaa? Wakati mwingine huwa najiuliza hivi raisi wetu akikutana na viongozi wenzake wa nchi zingine anaanza vipi mazungumzo yake? Nini inakuwa salamu yake? Akiulizwa "How is Tanzania doing Mr.President?" anajibu nini?Najua wakati mwingine inakuwa ngumu kukubali au hata kuona lolote jema linalofanyika ndani ya nchi zetu.Nyingi zimejaa rushwa,mipango mibovu ya kimaendeleo,viongozi wanaotamani wasingezaliwa Afrika maana hata kukaa nchini hawataki,kutwa wapo safarini.Kila mtu serikalini anatafuta fursa ya kwenda nje eti kubadilishana uzoefu na kujifunza wenzetu walivyofanya.Uzushi mtupu. Lakini je ni kweli kwamba hakuna lolote jema kabisa? Je ni kweli kwamba nchi zetu zote za kiafrika ni uwanja wa fujo, mshikemshike,mbinde kila kukicha, kila kukicha heri ya jana? Vyombo vyetu vya habari, sisi wanablog,wewe msomaji,wewe mwananchi unasemaje?Mtazamo wangu umeshausoma hapo juu.Ndesanjo aliwahi kuuliza siku moja,now that we have got blogs,what are we gonna do with them? Ndesanjo alikuwa akiongelea muungano na muelekeo mpya wa blogs kama nyenzo mpya ya mabadiliko ya jamii. Mabadiliko hayo yalijumuishwa vizuri na BBC wiki chache zilizopita walipouliza can we rebrand Afrika? (samahani sijapata kiungo cha habari hii) Napenda kuamini kwamba inawezekana hata kama wengine mnadhani tumeshachelewa sana.Lazima sisi watanzania/waafrika tuanze kuonyesha picha tofauti ya kuhusu nchi zetu/bara letu.Kama tunakubaliana kwamba blogs ni nguvu mpya ya umma basi hatuna budi kuitumia.Kumbuka kwamba sisemi kwamba tusionyeshe mabaya yetu ila ninachosema ni kwamba tuonyeshe mazuri pia(ikiwezekana mengi zaidi) na pia wakati huo huo tuonyeshe mabaya ya wenzetu na ikiwezekana mazuri pia ambayo yanafaa kuigwa. Huo ndio uundwaji mpya wa jamii katika dunia ambayo inazidi kuwa kama kijiji.Ombi: Kama unayo picha au unazo picha zinazoonyesha shughuli za kimaendeleo nchini Tanzania, shughuli chanya za utalii,sanaa,michezo, maisha au lolote lile jema,lolote lile unalodhani vyombo vya magharibi visingependa kulionyesha tafadhali nitumie kwenye e-mail jeffmsangi@sympatico.ca na mimi sitosita kuziweka kwenye blog zangu hususani ile ya kiingereza ya proudafrican.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 1:39 PM


|
Permalink |
Tuesday, March 13, 2007
BARIDI INAPOANZA KUPUNGUA.......
Hali ya hewa ni habari kubwa sana katika hizi nchi za magharibi.Kuna watu ambao hutazama luninga ili tu kupata utabiri wa hali ya hewa!Siku hizi hata mimi hujishtukia nikizingatia kwa makini utabiri wa hali ya hewa tofauti na nilivyokuwa kwetu.Sina uhakika kama huu ndio ule utaratibu wa "ukikuta wenzio ni chongo na wewe fumba jicho moja" au la!Usishangae sana basi kuona kwamba mara kwa mara nimekuwa nikikuhabarisha au kukuletea picha za hali ya hewa kutoka hapa.Nilipokuwa Tanzania jamaa wa hali ya hewa walikuwa wakishaanza utabiri wao baada ya taarifa ya habari ungetarajia mambo mawili yatokee;nizime televisheni au nibadili channel.Inawezekana kwa sababu hadithi yao kila siku ilikuwa ni ile ile..."kanda za juu kusini mvua za hapa na pale, mikoa ya Dar-es-salaam,Pwani,Morogoro itapata mawingu na mvua za rasha rasha".Tofauti na kwetu ambapo masuala ya hali ya hewa huwekwa mwishoni hapa wakati mwingine(kama sio mwingi) hali ya hewa huwa ndio "breaking news".Huwa inatokea jamaa wakautisha umma mzima na wala hali ya hewa isiwe mbaya kama walivyosema.Bahati nzuri au mbaya ni kwamba utabiri wa hali ya hewa ni mojawapo ya taaluma chache sana duniani ambapo mtu anaweza kukosea na wala asiwajibike kwa yeyote.Hivi sasa baridi imeanza kupungua.Majira ya baridi kali ndio yanayoyoma ili kupisha masika za huku kabla ya kuyakaribisha majira ya joto (summer). Jambo moja la aina yake huku ughaibuni ni jinsi maduka yanavyobadili bidhaa kuendana na majira yaliyopo. Hivi sasa ukienda madukani karibuni kila kitu cha kusaidia kupambana na baridi kama masweta,makoti nk vishaondolewa kwenye shelves. Msimu mpya vitu vipya.Hii ni tofauti kabisa na kwetu ambapo bidhaa nyingi hudunda dukani miaka nenda,miaka rudi mpaka atokee atakayezinunua. Hapa nakumbuka jinsi lile duka la "mangi" pale mtaani kwetu lilivyosheheni bidhaa hususani alipoacha kutukopesha! Pichani juu ni mall kubwa ijulikanayo kama Eaton Centre iliyopo jijini Toronto ambayo huhesabika kama mojawapo ya vivutio vikubwa vya utalii.Huko ndipo wengi wanapoelekea ili kujiandaa kwa majira yanayokuja.Kazi kweli kweli.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:42 AM


|
Permalink |
Tuesday, March 06, 2007
UMESIKIA KUHUSU "YESU" HUYU?
"You can become whoever or whatever you want to be,just put your mind into it".Nausikia msemo huu kila mara katika matamasha ya kuhamasisha vijana ninayohudhuria mara kwa mara hapa Marekani ya Kaskazini.Endapo unahisi kukata tamaa ya maisha ni dhahiri kwamba msemo kama huo hapo juu unaweza kubadilisha japo theluthi ya mawazo yako.Pamoja na hayo sijawahi kufikiri au kudhani kwamba kumbe "kuwa chochote au yeyote" ni pamoja na kuweza kuwa kitu kama "Yesu" kama ambavyo jamaa mmoja anayeishi huko Houston,Texas,nchini Marekani anavyodai. Waumini wake wanazidi kuongezeka siku baada ya siku.Ile hadithi ya kufa,kufufuka na kisha kupaa mbinguni ya yule Mnazareti ni kama ngonjera kwa waumini hawa.Yesu wao yupo hai na anaishi,anadunda na kunywa mvinyo kwa raha zake.Some habari hii kwa undani hapa.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 6:29 PM


|
Permalink |
Thursday, March 01, 2007
NINI TAFAKURI YA KAULI HII?
RAIS Jakaya Kikwete, amesema matatizo yanayojitokeza katika mikataba mbalimbali ambayo serikali imeingia na wawekezaji, pamoja na mambo mengine, yanasababishwa na uwezo mdogo walionao baadhi ya wataalamu wa Kitanzania wanaoshiriki katika majadiliano ya mikataba hiyo
Huo hapo juu ni utangulizi wa habari iliyoandikwa leo katika gazeti la Tanzania Daima chini ya kichwa cha habari "JK aiangukia Norway".Kama mwandishi wa habari hiyo (mwandishi wa raisi?) amemnukuu vizuri raisi wa jamhuri,basi ni wazi kwamba amekiri na kuanisha mambo mengi sana.Je ina maana Tanzania imekuwa kila siku inatuma "vihiyo" wakajadili mikataba yenye maslahi mazito ya kitaifa?Je ni kweli kwamba Tanzania haina wataalamu wa kuweza kuuangalia mkataba fulani na kuona mapungufu yake kabla haujasainiwa? Kwanini basi tumvike mtu majukumu mazito kama ya kuamua kuupitisha au kuukataa mkataba fulani kama hatuna imani na uwezo wake?Mtu kama huyu aliajiriwa vipi,alipata vipi cheo alichonacho.Unaweza kuisoma habari nzima kwa kubonyeza hapa.
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 7:30 PM


|
Permalink |