VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Thursday, December 22, 2005
"KAKA NA MIMI NINUNULIE MOJA"
Kawaida huwa naandika waraka huu mapema baada ya mwaka mpya kuanza.Mwaka huu,kwa sababu ni "mwaka wa uchaguzi" basi nimeamua kuandika huu kwanza nikitumaini kuandika mwingine pindi mola atakapofanya kweli.Yaani baada ya ule usiku wenye mbalamwezi(sio sehemu zote za dunia zenye bahati hiyo) ambapo familia,majirani,vijukuu na vitukuu hukusanyika na kuungoja kwa hamu mwaka mpya. Hapa nilipo bado nasikia sauti ya bunduki ambayo babu yangu alikuwa akifyatua pale kanisani pindi saa sita kamili usiku inapogonga.Sijawahi kumuuliza babu kwamba nani alikuwa anamwalika kanisani kufanya "makeke" yale, wala nani alikuwa anampa kibali cha kufanya baadhi ya watu wazima wafanye "msaada kwenye tuta" bila kupenda. Ninachojua mimi ni kwamba alikuwa anaashiria mwaka mpya.Enzi zile kulikuwa hakuna "sumu" ya ari mpya,kasi mpya.Zile zilikuwa ni enzi za "zidumu fikra" za fulani huku wazee wetu wakitulia kama kondoo!!!Walioshtuka wakapinga yaliyowakuta sote tunayajua ingawa ni mara chache kuyasikia yakiandikwa. Rafiki yetu Mark Msaki kutoka kule kwenye shujaa wa karne huwa anaandika sana kuhusu "dhambi" ile.Amini usiamini mpaka hivi leo kuna watu huwa wanairuka ile mistari yake.Aibu kubwa.Mark endelea na mwendo huo huo.
Usiku ule huwa umetawaliwa na mambo mengi sana.Kuna wale wanaokuwa kwenye vilabu vya pombe,wakinywa na kushangilia kwamba mwaka mpya umewasili. Hawa huwa wanakuwa wale wasioogopa ule uvumi kwamba mwaka mpya ukikukuta kwenye pombe basi mwaka mzima unaofuatia wewe utakuwa "bwana chapombe",ukikutwa safarini basi wewe "msafiri" mwaka mzima nk.Ukikutwa kwenye ngono basi cha mtema kuni utakiona. Tena nimekumbuka,hivi kilichompata mtema kuni ni nini? Tafadhali anayejua nisaidie. Nakumbuka rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa hana "gavana" na masuala ya ngono alijitahidi sana ili awe "juu ya kiuno" mwaka mpya unapoingia ili mwaka mzima uwe upande wake alivyolaani tabiri hizo baada ya kukimbiwa na kila kimwana katika mwaka mzima uliofuatia! Mimi nadhani waliokuwa wanavumisha uvumi huo ni wale wapiga upatu kwamba mwaka mpya lazima kila mmoja awe nyumbani na familia yake.Hilo ni la muhimu sana ila kama huwezi usije paramia milango ya treni ilimradi tu uwe na familia.
Kwa upande mwingine huwa kunakuwa na wale wakeshaji wanamaombi,wale watakatifu walio hai.Makanisa hupata "makuhani" wa muda. Mapambio,maigizo,ngonjera huwa ndio mwendo wa usiku kucha.Kahawa na kashata huwa ndio msaidizi wa kumfukuza "shetani" asilete usingizi mtu akalala akakosa "neno".Ukiachilia mbali wengi wa makuhani wa usiku mmoja ambao naambiwa wengi wao huwa wameenda kanisani kwa hofu na mashaka juu ya mwaka ujao, wapo wale mabitozi ambao wao huenda pale kutafuta "ngono" Najua utajidai kutoa ulimi kwa mshangao.Huo ndio ukweli ngono huwa zinafanyika kwenye viwanja vya makanisa kwa kisingizio cha "utakaso".Wao watakuwa wanatoa "mahubiri" tofauti.Majeruhi wa "wahubiri" hawa huwa ni wale mabinti wa geti kali. Kanisa moja kule Tabata lilipata mshangao baada ya kukuta maganda kibao ya "ninajali" asubuhi yake. Makasisi walishangaa sana kugundua kwamba "shetani" alifika mpaka kwenye mlango wa nyuma wa kanisani. Kasheshe ilikuja pale kasisi alipoteleza baada ya kukanyaga moja ya "ninajali" hali iliyofanya na zake mbili zianguke kutoka mfukoni mwake. Unajua majina ya watoto ambao mimba zao zilitungwa katika usiku wa mkesha wa mwaka mpya? Yanayotokea usiku ule ni mengi ndugu yangu,siwezi kuyamaliza nikiyaandika hapa.

Ninapopenda mimi ni ile siku yenyewe ya mwaka mpya.Yaani tarehe moja,mwaka mwingine(2006)Kwa walio wengi mwaka mpya humaanisha mambo mapya na kwa wengi vilevile mwaka mpya huashiria matumaini mapya baada ya kuachana na mabalaa,majaribu,mitikasi bubu na kila aina ya laana za mwaka unaokuwa unapewa kisogo(upende usipende).Kwa bahati mbaya mazuri ya mwaka huwa hayakumbukwi sana katika siku hii.
Takribani kila mtu ambaye anakuwa amejaliwa kuuona mwaka mpya bila kuwa kitandani kwa ugonjwa wowote huwa ni mwenye furaha ambayo inatokana na "matumaini" niliyosema hapo juu. Harufu za pilau na maandazi ya tangawizi, kahawa,tambi, kashata na buruba huwa zinaumiza pua za watu kila kona.Ukipita mitaani utaona jinsi ambavyo watoto wanacheza na kujirusha.Huwa hawajali hata magari na wapita njia wa aina yoyote ile.Kwanini wajali bwana?Mwaka mpya umefika,nyumbani mama karekebisha maaakuli ya kueleweka,jioni ana uhakika wa kulala akiwa ameshiba? Usishangae akikuambia kwamba moyoni ana furaha kwa sababu ukiachilia mbali mwaka mpya,ahadi ya wazazi ya kumpeleka kuanza shule ndio inazidi kukaribia.Yeye hajali kama baba kichwa kinakuuma na ahadi yako mwenyewe.
Muziki mkubwa huwa bado unasikika kutoka kwenye ile "baa mpya". Magari(mengi yao madein japani) huwa yamesheheni pale asubuhi na mapema huku wenye nchi wakipata supu ya makongoro,mtori na chapati.Wengi utawaona macho yalivyowaiva,mwenye akili zako unajua kwamba hayo ni matokeo halisi ya mkesha wa mwaka mpya kwenye zile sehemu ambapo sadaka huwa ni "kaka na mimi ninunulie moja basi ya mwaka mpya".Kule ambapo kichwa hufa ganzi kila baada ya dakika kadhaa kutegemeana na kasi yako. Yaani kule ambapo urembo wa mtu huonekana dhahiri zaidi kadiri giza linavyozidi kutanda. Kama hupajui huko shauri yako.

Kwenye hii "baa mpya" ule uchangamfu wa jana usiku huwa umeanza kupotea. Sura ya majukumu huanza kujongea.Mama watoto ni mjamzito,hana kazi yoyote ya kusaidia kipato cha familia,watoto wawili ulionao tayari wanatakiwa kurudi shule mapema mwezi huu. Sare za shule,karo,vibegi nk hujanunua.Ule ushindi uliokuweka "kwa wense" jana usiku taratibu unaanza kugeuka kuwa maumivu. Tayari "mwaka mpya" umeingia.Ulilotimiza katika mwaka uliopita hulioni. Tafakari haina msaada kwa wakati huu.
Tutakiane kheri ndugu zangu.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 7:21 PM | Permalink | Maoni 3
Sunday, December 18, 2005
HIVI NYERERE YUKO WAPI?
Asubuhi na mapema,nimesimama nje ya kibanda changu cha nyasi.Usiku wa jana sikulala,kunguni hawakunipa nafasi kabisa.Isitoshe mlo wangu wa jana haukuwa mzuri.Mlo mzuri wa mwisho nilikula juzi kwenye siku ya mwisho ya kampeni kabla ya uchaguzi wa jana.Mgombea wa ubunge aliandaa pilau kwa wanakijiji wote.Mjukuu wangu anayeishi jijini Dar-es-salaam anapenda kuuita mlo huu "pilau ya rushwa".Sijui kama namuelewa au anaweza kueleweka kwa wengi.Mwenye njaa huwa na hasira,na mtu akiwa na hasira hasikii wala haelewi.
Nataka kunawa uso niende zangu shambani.Na njaa hii pamoja na usingizi, sijui kama nitaweza fanya chochote huko shambani. Nagundua sina hata tone la maji nyumbani kwangu ingawa pembeni ya kibanda changu kuna bomba la maji.Nasikia ulikuwa ni mradi wa enzi zile za vijiji vya ujamaa na kujitegemea.Miradi ambayo haikutimia na hivyo maji ya bomba yakabakia kuwa ndoto za senene.Namkumbuka mke wangu. Maisha ya hapa kijijini yalimshinda hivyo akaamua kukimbilia jijini Dar-es-salaam.Nasikia huko anafanya biashara ya kuuza mwili.Sijui mwili anauuza vipi,kwa jumla au kwa dakika chache tu? Masuala haya ya mjini huwa yananiogopesha sana.
Kwa mbali namuona balozi wetu wa nyumba kumi na moja anakuja. Uso umempauka,suruali ina matundu kibao ila alhamdululahi juu kavaa tisheti mpya. Ni hizi tisheti alizotugawia mgombea wetu,zimeandikwa "Chagua CCM,Ari mpya,Kasi mpya....nk".Nimesahau hayo maneno ya mwisho maana kusoma na kuandika sijui.Vijana wa shule ya hapa kijijini ndio waliotuambia maneno hayo. Sijui mwakani watasomea wapi na wao maana tetemeko la juzi liliangusha madarasa yote mawili ya shule.Mwalimu mmoja waliyekuwa naye nasikia na yeye ameamua kuondoka kijijini kwenda kutafuta maisha huko mjini.
Balozi ananiambia kwa sababu mgombea alitupa tisheti na pilau tukala basi tunatakiwa kwenda bomani kusikiliza matokeo ya uchaguzi mchana huu.Sina jinsi,lazima nihudhurie na ikibidi nishangilie kwa nguvu endapo atashinda.Eti najiuliza endapo "atashinda".Kwanini asishinde wakati mgombea mwenzake wa chama gani sijui kile hakuweza hata kuwapa wanakijiji maji ya chupa? Na isitoshe tukasikia kwenye radio kwamba ni mchawi? Nasikia mwenyewe analalamika kwamba hizo ni njama tu za kuhakikisha anashindwa.Namuonea sana huruma lakini sijui nifanye nini kumsaidia.Labda mjukuu wangu akija tena nitamueleza.
Jua linawaka kweli.Tumeketi chini kwenye mavumbi.Tunasubiri watu wa uchaguzi watangaze matokeo.Kama nilivyotabiri, huyu mwenye shati la kijani na suruali nyeusi anatangazwa mshindi.Anaruka juu na kushangilia(kama alikuwa hajui atashinda vile) Kwa sababu tumbo lake ni kubwa basi shati aliyovaa inachomoka kutoka kwenye suruali.Watoto wachache waliokuwa pale wanacheka kuona tumbo la mtu mzima halafu lenye ukubwa kama ule mtungi wa pombe kwa "mama muuza".
Balozi anatuamsha tushangilie! Mawazo yamenitinga,lakini najishtukia nasema ...oyeeee.Walinzi wake wameshamzunguka,hata balozi wetu anakatazwa kumpa mkono.Walinzi wanasema "mheshimiwa" anataka kwenda kupumzika,kesho asubuhi anarudi Dar-es-salaam.
Kwa madaha anaingia kwenye gari lake la kifahari.Anatutimulia vumbi.Anaondoka zake.Kichwani najua hiyo ndio imetoka. Kama tutakuwa hai tutamuona tena baada ya miaka mitano. Pembeni namuona yule mgombea mwingine.Amekusanya watu anawaelezea madhara ya tisheti na pilau.Anaeleza jinsi ambavyo tumenunuliwa na hivyo hatuna haki ya kuuliza kuhusu hospitali,maji,elimu,barabara wala chochote.
Namuona balozi kwa pembeni.Macho yamemtoka,pembeni yake mjukuu wake kasimama.Balozi ananifuata ananiambia mjukuu kaleta habari mbaya.Bibi yake kazidiwa huko nyumbani.Anaomba tukamsaidie kumpeleka kwenye zahanati huko wilayani.Ni mwendo wa masaa saba kutembea.Naona kasahau kwamba ile zahanati ilishafungwa kwa kukosa daktari na vifaa vya kutendea kazi.Naona mtu mzima analia.
Njaa imenishika bado,sijatia kitu tumboni zaidi ya mhogo niliodoea kwa jirani yangu.Nifanye nini?Tufanye nini kubadili hali hii? Namfuata mzee wetu wa kijiji nipate busara zake. Namkuta kajikunja kwenye mkeka wake.Baada ya salamu naanza kumueleza fikra zangu.Ananiuliza, hivi yule "Kambarage Nyerere yuko wapi siku hizi?".Nahisi kizunguzungu.Mjukuu wangu,nitakueleza baadaye.Bado swali la Nyerere linaniletea maruweruwe.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:28 AM | Permalink | Maoni 11
Wednesday, December 14, 2005
TATIZO LA KIUFUNDI
Kama wewe ni mtembeleaji wa huu uwanja wangu mara kwa mara utakuwa umeshagundua kwamba ina mabadiliko.Kwa bahati nzuri au mbaya mabadiliko hayo hayakufanyika kwa mapenzi yangu.Kuna tatizo la kiufundi ambalo lilitokea na ambalo kwa kweli lilikuwa nje ya uwezo wangu kurekebishika.Nikaona isiwe tabu.Kwa maana hiyo napenda kusema samahani kwa usumbufu wowote.Tunaendelea kubonga bongo kama kawaida!
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:45 PM | Permalink | Maoni 2
Tuesday, December 13, 2005
BLOGU:TUTAFUTE NENO LETU!
Kama sikosei,mojawapo ya umuhimu wa huu uwanja ni pamoja na kuelezea kero,mafanikio,kukosoa,kurekebisha,kufundisha,kugundua,kuhoji,kutoa changamoto(duh kiswahili kina maneno mengi sana,ngoja niishie na haya kwanza)
Nakumbuka kipindi cha nyuma kidogo tu,mjadala mkali sana ulirindima ndani ya ukumbi huu kuhusu matumizi ya lugha yetu ya kiswahili.Hoja zilitolewa,waliokashifiana wakafanya hivyo lakini ujumbe ukawa umewasili kwamba lazima tuanze taratibu kukitoa kiswahili "utumwani" Kwenye utumwa huu wa physics kuwa fizikia,biology kuwa biolojia nk. Katika matembezi yangu ndani ya uwanja huu nimegundua kwamba kuna neno moja ambalo tunalitumia sana.Neno hili ni BLOGU.Kama sikosei tumelitoa kwenye blog/weblog nk.
Nimejaribu sana kutafuta neno mbadala ili tuanze kwa kujivunia na majina yetu,asili yetu,lugha yetu.Usinicheke nikisema kwamba mpaka hivi leo ninapoandika nimetoka kapa.Kiswahili kimepinda.
Hivyo basi naomba nitoe changamoto.Naamini wataalamu wa kiswahili wamejaa tele kwenye uwanja huu.Tutafute neno la kiswahili tuache kuuita huu uwanja blogu.Watu watoe mapendekezo yao wakieleza kwamba kwanini huku akikumbuka mtiririko kama huu; blogu,bloguni.....nk. Kama itabidi tuingize lugha zetu za makabila ili tupate neno letu wenyewe basi tufanye hivyo.Kwa mfano kule upareni mazungumzo ni "mgayo".Maneno kama hayo.Vyovyote vile tafadhali tutafute neno letu.Ukombozi wa kiswahili chetu unaweza kuanzia hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 2:22 PM | Permalink | Maoni 6
Monday, December 12, 2005
DUH! BARIDI IMEWASILI
Ni majira ya baridi kali.Yale majira yasiyopendwa na wengi.Wakuja kama mimi hatutaki hata kuyasikia.Wazawa kidogo wanaweza kuyavumilia.Wana kila aina ya shughuli hawa jamaa.Wengine eti wanaenda kuvua samaki kutoka kwenye mito na maziwa kulimojaa barafu.Wanakenua kama watoto wa chekechea.Wakimaliza hapo wanaenda kujirusha kwenye vichuguu vilivyojaa theluji. Lakini pamoja na yote hayo wengi wao huomba majira ya joto yarejee mapema.

Huu ndio wakati wao wa kupeana zawadi za kila aina.Sehemu za maduka zimejaa bidhaa hivi sasa.Televisheni hazitangazi kitu kingine zaidi ya nini umnunulie mwenzako kama zawadi ya mwisho wa mwaka na kwa wale wakristo sikukuu ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu.Uongo! Yesu hakuzaliwa mwishoni mwa mwaka.Alipozaliwa wachungaji walikuwa makondeni.Watu hawachungi wakati wa baridi kali namna hii.Nahisi ubepari na misingi yake ya kibiashara ndio vilipendekeza masuala haya.Imani haina uhusiano na ubepari nadhani.

Nimesimama kwenye kituo cha treni tayari kuelekea katikati ya jiji la Toronto ambapo mwendo ni ule wa hakuna kulala mpaka kieleweke.Pembeni yangu wamesimama wapenzi wawili wakifanya karibuni kila kitu kuhusu mapenzi.Walichobakiza nadhani ni kanyusi kumuingila sinyuka tu! Mwanamke analalama kwamba anasikia baridi, jamaa ndio joto la asili. Nataka niwashauri wakatafute "gesti" wamalize haja zao.Looh nakumbuka sipo mitaa ya kati ya jijini Dar,kule ningechukua bakora na kuwatandika.Maadili yetu hayaendi hivyo wajameni.Hapa siwezi kuthubutu. La sivyo nitakuwa gumzo na jela nitaenda.Nitaambiwa siheshimu haki za watu.Hivi hawa jamaa wanajua kuhusu "mfadhaiko"? Shauri yao.

Naelekea mtaa mmoja unaoitwa Yonge(inatamkwa yang) yaani kama vile Yanga bila hiyo a. Inasemekana huu ndio mtaa mrefu kupita yote duniani. Mimi sina uhakika na hilo bwana.Kwanza sijatembelea dunia nzima na pili hawa wenzetu bwana kila jambo lao ni la dunia nzima. Si ushawahi kusikia wale mabingwa wao wa ligi ya mpira wa kikapu wakiitwa mabingwa wa dunia bila hata kucheza na timu za nchi zingine zozote? Hujawahi kusikia zile tunu za muziki wakasema mwanamuziki fulani ndio bora dunia nzima?Kwa wengi wao dunia huanzia hapa na kuishia hapa. Sisi tunaotoka mbali ndio tunajua zaidi yao.Kule kwetu kwenye warembo wa kila aina.Kwenye huduma nzito kama za mama ntilie na mama sukari.Kule kwenye....simalizii.

Naenda kuhudhuria mkutano wa
masuala ya Afrika. Tumeendelea kugundua kwamba picha ya Afrika sio mbaya kama wenzetu wanavyotaka tuamini.Tumeamua kupambana nao kwa kutumia nyenzo za kisasa kama huu mtandao. Pembeni yangu wamekaa vijana wanapiga hadithi ya jinsi majira ya joto yalivyokuwa. Yaani wanakumbushia ule wakati wanajamii wa hapa wanapotembea huku asilimia tisini na tano ya miili yao ikiwa wazi/uchi. Hata sijui uchi unatafsiriwa vipi hapa.

Ndani ya chumba cha mkutano mimi ndio wa kwanza kuwasili.Nilihisi nimechelewa lakini kumbe ule utaratibu wa "Hakuna matata wala haraka Afrika " Huwa hauishii Afrika tu bali huwa tunakuja nao hata huku ughaibuni. Nachelea kumlaumu mtu kwa kuchelewa kufika.Huenda wenzangu waliamua kuendesha magari yao hivyo wako kwenye foleni mbaya za majira haya ya baridi. Huwa napenda sana heshima wanayokuwa nayo madereva wakati huu wa barafu barabarani.Kila mmoja anakuwa makini kuliko kawaida! Nadhani wakati huu polisi wa hapa hawaupendi kabisa. Polisi wa hapa bwana ni kama wakusanya kodi vile.Wanapenda sana kutoa tiketi kwa binadamu wenzao. Halafu kama ulidhani utaratibu wa kujificha vichakani ni wa trafiki wa bongo tu umenoa.Muulize
Ndesanjo kama unadhani natania. Yaani wanapojificha hata huwezi dhania. Utakachoona ni vimulimuli tu nyuma yako. Siku moja nilitaka nisimamishe gari nimuulize polisi mmoja "hivi ukigongwa na nyoka huko vichakani utasema nini"? Halafu unaambiwa eti wanalinda maisha ya mwananchi.Uongo.Nishapita taa nyekundu,nimeshapigwa dafrao la nguvu,wewe ndio unajitokeza huko vichakani kwako.Ungekuwa unaonekana barabarani vizuri ningepita kweli taa nyekundu? Ni mfano tu wandugu,msipite taa nyekundu aisee,hatari sana.Naona jamaa zangu wameanza kuwasili hapa mkutanoni. Baadaye
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:07 PM | Permalink | Maoni 4
Thursday, December 08, 2005
HEKA HEKA ZA PASIPOTI MPYA!

Mambo mawili muhimu sana yanatokea nchini Tanzania mwaka huu.Jambo la kwanza ni hili la uchaguzi mkuu ambao unafanyika wiki ijayo baada ya kuahirishwa kwa muda kufuatia kifo cha mgombea mwenza wa nafasi ya uraisi katika Chadema. Macho na masikio yetu bado yameelekezwa katika uchaguzi huo.Leo sina mengi kuhusu uchaguzi.
Jambo la pili ambalo ndio msingi wa habari hii ni hili zoezi adimu la kubadilisha pasipoti.Kisingizio kinajulikana.Ni amri kutoka kwa wenzetu wa magharibi katika juhudi zao za kupambana na ugaidi duniani.Tunaambiwa kwamba pasipoti zetu za zamani zilikuwa hazisomeki kwa machine kama za nchi nyingine duniani kwa hiyo ilitubidi tuzibadilishe,tupende tusipende.Nathubutu kuiita amri kwa sababu kama isingekuwa amri basi utaratibu mrahisi sana ungetumika kwamba kama una pasipoti ya zamani basi ikiisha muda wake, ukienda kubadilisha unapewa mpya. Na kama hujawahi kuwa na pasipoti kabla ya hapo basi moja kwa moja unapewa mpya. Katika kipindi cha miaka mitano watanzania wote wangekuwa na pasipoti mpya na fedha chungu mbovu zingeokolewa na kupelekwa kwenye miradi ya kimaendeleo. Lakini kwa sababu za kiusalama,sababu za kijasusi dhidi ya ugaidi duniani wafadhili wangekataa.Wangetuelewa endapo tu tungekuwa na viongozi wenye uwezo wa kutetea maslahi ya nchi bila woga.Kwa hivyo basi zoezi hili la kubadilisha pasipoti lingekuwa limetazamwa kwa undani,kitaalamu ili kujua jinsi gani lifanyike.
Badala yake zoezi hili limegeuka kuwa kero ambayo inawafanya wengi(hususani waliopo nje ya nchi na wasio na moyo) kuamua kuukana moja kwa moja uraia wao halali wa Tanzania.Siwalaumu kwa kweli. Hili lina madhara yake.Wachumi na wanajamii wanajua zaidi kuhusu masuala kama hayo.Kero kubwa ni katika utaratibu mzima wa kubadilisha pasi hizo za kusafiria. Mengi yameandikwa kuhusu uzembe, ukiritimba kuhusiana na suala zima la kubadilisha pasipoti.
Nilipokuwa nikisoma habari mbalimbali katika vyombo vya habari kuhusiana na utaratibu mzima wa kubadilisha pasipoti nilidhani ni mapungufu yetu ya kawaida ambayo yanaongeleka.Kimbembe kimekuja nilipojaribu kuyavulia nguo maji ili kubadilisha pasipoti yangu kupitia ubalozi wetu hapa Canada. Labda niseme wazi kwamba ndio kwanza nimeanza zoezi hili la kubadilisha pasipoti. Na mpaka hapa nilipo nimeshakwama.Poleni wenzangu ambao mpo kwenye hali kama yangu.Najua mpo wengi.
Nimeagiza fomu kutoka ubalozini.Nikaambiwa kwamba ni lazima niilipie hiyo fomu $ 20. Kwanza nilishtuka kwa sababu nimeshaanza kuzoea utaratibu wa hapa Canada kwamba hamna hata fomu moja utakayopewa kwa mauzo.Iwe ni ya kuomba uraia,makazi ya kudumu n.k.Unaweza kuletewa hata fomu kumi kwa mkupuo ukitaka.Kwanini uuziwe fomu??Kodi wanazokatwa wananchi zinafanya nini? Nikaona isiwe tabu nikaagiza washirika wangu waliopo huko ulipo ubalozi wetu(Ottawa- mwendo wa kama masaa sita kutoka hapa Toronto kwa gari).

Kichefuchefu kilianza kunipata baada ya kufungua hiyo fomu yenyewe na kugundua kwamba ni fomu sawa sawa kabisa na zile tulizojaza miaka ile wakati tukiomba pasipoti zinazobadilishwa.Sana sana nimeona vifungu vichache sana ambavyo vimebadilishwa.
Wakati naanza kusamehe hayo yote nikagundua kwamba hii fomu imetengenezwa zaidi na inafaa zaidi kwa mtu ambaye bado yupo nyumbani Tanzania.Haijatengenezwa kukidhi haja ya mtanzania aliyeko nje ya nchi. Sababu ni nyingi ila ngoja nijaribu kueleza chache hapa chini.
Fomu imeandikwa kwa kiswahili kitupu bila hata tafsiri ya neno moja la kiingereza. Lazima tukubali kwamba kiswahili chetu bado sio cha kimataifa kiasi cha kutumika ulimwengu mzima. Maelekezo ya jinsi ya kujaza fomu hiyo kwenye tovuti ya ubalozi yote yameandikwa kwa kiingereza! Nadhani hata wao wanakubaliana nami kwamba kiswahili hakina nafasi hapa. Lakini pia nashindwa kuelewa kwamba kwanini tovuti kama hii ya ubalozi haina uhuru wa kuchagua lugha ya kiswahili au kiingereza? Mapungufu mengine haya.Fomu inanitaka nijaze sehemu zinazouliza mtaa/kijiji.Sijui naishi kijiji gani hapa Toronto! Hamna vijiji hapa ninapoishi.
Tayari nipo hapa,fomu inanitaka nijaze madhumuni ya safari na nchi ninazokwenda.Safari gani? Siendi popote kwa hivi sasa
Fomu inanitaka nijaze kazi ninayofanya,kiswahili chake sikijui
Fomu ina kipengele cha shuhuda kwa mwombaji
ambaye anaweza akawa jaji.kabidhi wasii,hakimu.wakili/kamishna wa viapo akiwa yeye mwenyewe ni raia wa Tanzania.Nimtoe wapi mtu kama huyo hapa Canada ndugu zangu? Hata kama nitampata hakimu,jaji nk wa hapa, nani atafanya kazi ya kutafsiri fomu hiyo?
Shuhuda anatakiwa aandike nyuma ya picha kwamba hiyo ni sura yangu.
Pili zimetolewa sampuli za picha pale,sijui wazungu wa wapi wale.Yaani tumeshindwa kabisa kuweka picha za watanzania wenzetu kama sampuli za jinsi gani picha hizo zipigwe?

Maswali magumu yenye majibu haba yananijia.Hivi sisi watanzania tuna nini jamani? Hawa tunaowaita viongozi wa nchi,mawaziri,mabalozi,wabunge ni kina hasa?Wizara za mambo ya ndani na nje wanafanya kazi gani?Kuna jamaa aliwahi kuniambia kwamba Tanzania hatuna mameneja wazuri. Sijui nikubaliane naye au nikatae?
Najua serikali yetu ni bingwa wa kupuuzia mambo.Hili nadhani lisipuuziwe.Ni aibu kwa taifa letu. Lazima serikali ikiri kwamba zoezi hili halikuangaliwa kwa makini.Walioboronga wasihamishiwe wizara zingine bali wajiuzulu au waachishwe kazi kwa nguvu.
Majuzi nimesoma mahali kwamba bidhaa za kutengenezea pasipoti mpya hamna/zimekwisha! Muda wa kusubiri pasipoti mpya ni kama miezi sita hivi. Kwa nchi yenye watu milioni 37 na ambao kati yao asilimia ndogo sana wanatumia pasipoti zao ambayo ni haki yao ya kikatiba. Kwanini utake kujua mtu anakwenda wapi,kufanya nini? Kwanini hilo lisiachiwe balozi husika?Lina uhusiano gani na pasipoti?
Kero ni nyingi sana juu ya suala hili.Wakati umefika,tuseme ukweli.Tuishauri serikali yetu,tuikosoe na isione aibu kukubali kama imekosea. Tuanzie hapa kwenye ulimwengu wa blogu.


 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:00 PM | Permalink | Maoni 6
Tuesday, December 06, 2005
MSOME FIDEL CASTRO!

Katika viongozi ambao wananivutia duniani sidhani kama kuna ambaye ananivutia kuliko Fidel Castro.Huyu ndio yule jamaa ambaye hujaza watu na wakamsikiliza kuanza mashariki mpaka magharibi.Anachokiongelea Fidel Castro hapa ni kama majumuisho ya masuala mengi sana ambayo wanablogu wa kiswahili tunayazungumzia hapa kila siku.Naamini tunaeleweka vilivyo kwa sababu habari za uhakika za kijasusi nilizonazo ni kwamba "tunaogopwa".Tunasema ukweli bila woga,tunatimiza haki zetu za msingi na zilizoandikwa kwenye katiba za nchi zetu.Kama ziliandikwa bila nia ya kutekelezwa basi bahati mbaya.Tafuta muda muafaka,kama unakunywa maji ya baraka basi yatayarishe,msome Fidel Castro hapa kwa makini,kwa vituo.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:56 PM | Permalink | Maoni 2
DAWA YA MALARIA?
Ugonjwa wa malaria unaua watu wengi barani Afrika kila mwaka zaidi ya ugonjwa wa ukimwi. Hili halina nafasi sana kwenye vyombo vya habari vya dunia kwa sababu wanaotawala mikataba ya habari ugonjwa wa malaria hauwasumbui sana.Sasa kuna mpambano unaendelea juu ya tiba ya malaria.Soma hapa uone jinsi wanasayansi wetu wanavyojitahidi.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:49 PM | Permalink | Maoni 0
Sunday, December 04, 2005
TANZANIA NA UHURU WA HABARI!
Sina hili wa lile,nimejipumzisha nikijaribu kuwa baba bora.Maisha ya ughaibuni yanataka moyo jamani.Waliopo huku watanisaidia kwa hoja hii.Simu inaita,ni Boniface Makene kutoka Texas,Marekani. Ananipa habari ambazo kwa kweli sio njema na hazipendezi kabisa katika karne hii ya ahadi ya usawa na uwazi,uhuru wa habari,uhuru wa kujisomea na kuchambua masuala mbalimbali.Gazeti ambalo naliandikia makala kila jumapili la Tanzania Daima limefungiwa kwa siku tatu.Kisa na mkasa kisome hapa.
Sheria iliyotumika ni sheria ya magazeti namba 3 ya mwaka 1976!Hili kwanza linanitia simanzi.Hivi kweli leo hii ukizingatia jinsi dunia ilivyobadilika ni halali kutumia sheria ya mwaka 1976?
Nadhani wakati umefika wa nchi yetu kukubali kubadilika na pia kuangalia masuala ya msingi zaidi. Huku ughaibuni kila siku jioni watu hukaa mbele ya luninga zao na kuangalia jinsi ambavyo viongozi wao hufanyiwa kebehi na watangazaji na wachekeshaji wa tv.Mfano mzuri ni bwana huyu anayeitwa Jon Stewart.Wapo wengine wengi tu. Ukitembelea tovuti yake unaweza pia kutazama baadhi ya dhihaka ninazozizungumzia. Sasa najaribu kujenga picha,raisi Bush angekuwa anapambana na watu kama hawa ingekuwaje?Je hii ina maanisha kwamba hatuna mengine ya msingi ya kuyafanyia kazi?
Ni kweli kwamba tamaduni zetu sio sawa na za Marekani,Canada au kwingineko.Lakini je leo hii tunaweza kusimama pembeni tukasema tuna tamaduni zetu?Tukasema kwamba raisi wetu hawezi kutaniwa? Je,habari hii kama ililengwa kwenye kumdhalilisha raisi wetu, ilisomwa na watu wengi zaidi hiyo Novemba 6 au sasa ambapo dunia nzima inatuangalia? Busara imetumika kweli hapa? Ngoja niishie hapa kwa leo!Sidhani kama kwa hali hii nitaeleweka hata nikiandika mpaka asubuhi.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 6:38 PM | Permalink | Maoni 1
Friday, December 02, 2005
MAREKANI NA HUKUMU YA KIFO!
Hukumu ya kifo nchini Marekani imechukua mtu wa 1000 tangu ianzishwe mwaka 1976. Suala la hukumu ya kifo ambayo serikali yetu ya Tanzania bado inalikumbatia( sina takwimu za watu walionyongwa kutokana na hukumu ya kifo) bado linazua mijadala mikali miongoni mwa wanasheria,wanaharakati wa haki za binadamu duniani.Canada haina hukumu ya kifo. Marekani pamoja na kuwa mtekelezaji mkubwa wa hukumu hiyo(sio katika majimbo yake yote) bado inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza duniani kwa vifo vinavyotokana na kuuawa iwe kwa mtutu wa bunduki ama vinginevyo. Suala gumu katika masuala haya ya hukumu ya kifo ni je kwa mfano huyo tunayemhukumu kifo hakuua,nini hatma yetu? Tunaweza kujadili.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:07 PM | Permalink | Maoni 1
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker