VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Sunday, December 17, 2006
MWANABLOG,UNAWEZA KUSHITAKIWA?
Tulipokutana tarehe 18 mwezi uliopita na kuweka historia mpya katika ulimwengu wa blog za kitanzania, mojawapo ya yaliyokubaliwa na kupitishwa na wajumbe karibuni wote kama sio wote kabisa ilikuwa ni suala la nidhamu katika lugha na maandishi tunayoyatumia,utafiti makini wa kile tunachoandika , kutunza heshima na utu wa binadamu wenzetu (wale tunaoandika habari juu yao) na matumizi muafaka wa kazi za watu wengine yakiwemo maandishi,video, picha nk.

Masuala hayo hapo juu na mengineyo mengi yamekuwa yakiongelewa mara kwa mara kuhusiana na tekinolojia hizi za kisasa zinazoruhusu uandishi wa raia ambao unasemekana kuwa wenye uhuru kuliko ambavyo imeshawahi kutokea.Masuala ya sheria, haki za binadamu, muelekeo wa tekinolojia hizi, matumizi yake kama vimulika vya jamii,faida na hasara za blogs huwa ni ajenda zisizoonekana kuwa na mpaka.Mijadala mbalimbali bado inaendelea.

Hivi karibuni nimejaribu kufanya uchunguzi kidogo tu kuona nini kimeshatokea baina ya kile ninachoweza kukiita mapambano baina ya mkono wa sheria na blogs. Kesi moja ambayo imeanza kuvutia wengi huku Marekani ya Kaskazini ni
hii hapa inayohusu matumizi ya picha zilizopigwa na watu wengine bila kutaja wazi chanzo(source) chake. Zaidi ya kesi hiyo maswali kama haya hapa chini ni muhimu kuyazingatia kama wewe ni mwanablog na mkereketwa wa uhuru huu wa upashanaji habari nk.

Je unaweza shitakiwa kwa maoni ambayo wasomaji wako wameacha kwenye blog yako?
Soma kesi hii.

Je ukiweka kiungo cha; kwa mfano video ya matusi unaweza shitakiwa? Soma hapa pia

Je nini kinaweza kutokea endapo wanafunzi wataacha maoni ya aina fulani kwenye blog na wakuu wao wa shule wakayapitia? Unadhani jambo kama
hili hapa ni sawa?

Tuwe makini.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 7:17 PM | Permalink | Maoni 6
Wednesday, December 06, 2006
KUULIZA SWALI NI KOSA?
Leo katika gazeti la Tanzania Daima nimesoma habari hii ambayo imeniacha kinywa wazi, sio kwa usingizi mzito, bali kwa mshangao. Eti ni kosa kumuuliza mbunge wako swali na kwamba jamaa mmoja ambaye amefanya hivyo amejikuta akipewa adhabu. Bonyeza hapa usome habari nzima.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:20 AM | Permalink | Maoni 6
Sunday, December 03, 2006
SAIDIA WATOTO WA AMANI

Wiki iliyopita,kupitia kitabu changu cha wageni, nilipata ujumbe kutoka kwa mwanadada Valerie Johnson(30) ambaye ni mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojulikana kama Amani Children's Home (Nyumba ya Watoto ya Amani) lenye makao yake kule Moshi,Tanzania.

Ujumbe wa Valerie kimsingi ulikuwa umeelekezwa kwa jumuia nzima ya wanablog wa kitanzania popote tulipo duniani.Nia ni kuomba kuungwa mkono kwa kile anachokifanya nchini Tanzania kujaribu kunusuru maisha ya watoto wa mitaani na wale ambao wamejikuta ni yatima baada ya wazazi wao kuchukuliwa na ugonjwa hatari wa ukimwi.Misaada mbalimbali ya hali na mali ndio vitakavyofanikisha maendeleo ya taasisi kama hii ya Amani.

Ni wazi kwamba tatizo la watoto wa mitaani na yatima linazidi kushamiri siku baada ya siku.Huu ni ukweli ambao hatuwezi wala hatupaswi kujaribu kuupa kisogo.Kwa bahati mbaya sera za kiserikali juu ya tatizo hili zimegeuka kuwa "bubu".Haishangazi kuona kwamba matatizo kama haya yameachiwa taasisi zisizo za kiserikali pekee jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa jamii ya leo,kesho na keshokutwa.

Wakati tukiendelea kushiriki katika kuiamsha serikali kuhusiana na sera zake kuhusu jamii ya watoto yatima na wa mitaani, tunaweza kuanza kujitolea kusaidia taasisi kama hii ya Amani.Kwa habari zaidi juu ya kituo hiki cha Amani tembelea tovuti yao kwa kubonyeza hapa. Pale utaweza kujisomea mengi kuhusiana na kituo hiki ambacho kina umri wa miaka takribani mitano sasa.Unaweza pia kupata mawasiliano na kituo hicho.Kumbuka kutoa ni moyo na sio utajiri.

NB:Pichani ni baadhi ya watoto wa nyumba ya Amani na ni kwa idhini ya Valerie Johnson
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:54 AM | Permalink | Maoni 5
Friday, November 24, 2006
UNAWEZA KUOA WAKE WAWILI KATIKA SIKU MOJA?

Maajabu ya dunia yetu hii hayaweza kuisha hata siku moja. Labda huo ndio ukweli mzito kuhusu dunia yetu. Hivi karibuni huko katika kitongoji kijulikanacho kama Ibrahim Koodnur, karibu na mji wa Hargeysa jamaa mmoja ajulikanaye kwa jina la Ismail Osman Abdullahi alioa wanawake wawili katika siku moja kama anavyoonekana katika picha hiyo hapo juu. Majina ya wake zake hao wawili ni Gasira Mohamed Hussein na Shukri Osman Mohamed.

Habari hii ambayo nimeletewa na rafiki yangu mmoja anayetokea katika nchi hiyo anayeishi hapa Canada hivi sasa, imeniacha kinywa wazi kidogo. Hivi inawezekana kweli?


Chanzo cha habari hii kinapatikana hapa kwa wale wanaojua kisomali.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 2:29 PM | Permalink | Maoni 5
Thursday, November 23, 2006
MPAKA WAKATI MWINGINE....MATOKEO YAMETOKA!
Matokeo ya raundi ya kwanza kuelekea mwisho wa tuzo za Blog bora nchini Canada yametoka. Kama mnavyojua blog yangu ya kimombo African Perspective kwa mara ya kwanza ilikuwa imeteuliwa kuwania tuzo hizo katika kundi la blog bora za kitamaduni.

Kwa bahati mbaya blog hiyo haikuweza kuchaguliwa kwenda raundi ya pili ya mchuano huo. Unaweza kutizama matokeo kwa kubonyeza hapa.Je,hilo linakushangaza? Mimi binafsi limenishangaza lakini sina budi kukubali kushindwa ili niwe mshindani (wakati mwingine labda). Asiyekubali kushindwa........

Ninachojua hivi sasa ni kwamba wengi wenu mlinipigia kura. Idadi ya barua pepe,simu,ujumbe mfupi wa simu za mkononi nk zilitosha kabisa kunionyesha jinsi gani mlinipa kura zenu.Kwa hilo sina budi kuwapeni shukrani zangu za dhati.Ahsanteni sana sana.Kilichotokea upande wa pili,baada ya kura zenu kuhesabiwa sikijui na wala huenda nisije kijua milele.Tekinolojia bwana,zina mambo yake!

Kwa wale ambao,kwa sababu moja au nyingine,hamkuweza kupiga kura wakati huu,tutajaribu tena wakati mwingine,inshallah.Nitaendelea kuandika kwa kutumia hizi lugha mbili,kiswahili na kule African Perspective,kwa kiingereza.

Sasa kwa sababu siku zote huwa inaudhi kushindwa, kumpigia kura mtu wako kisha asishinde, nimeona nikupe burudani kidogo na wimbo huu hapa chini wa hayati Bob Marley unaoitwa Three Little Birds(Ndege watatu wadogo).Ahsanteni sana.






 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:20 PM | Permalink | Maoni 6
Friday, November 17, 2006
NDANI YA TUZO ZA BLOG BORA CANADA

Kwa heshima na taadhima, ninayo furaha kuwatangazieni nyote kwamba blogu yangu ya kimombo inayojulikana kama African Perspective, imeteuliwa katika kinyang’anyiro cha tuzo za blogu bora nchini Kanada (2006 Canadian Blog Award). Imeteuliwa katika kundi la blogu bora za Kitamaduni (Best Cultural Blog).

Kura yako ni muhimu sana ili niweze kushinda.
Bonyeza hapa ili uweze kunipigia kura yako. Ukifika kwenye huo ukurasa mkuu wa 2006 Canadian Blog Award shuka chini mpaka ufike kwenye orodha ya Best Cultural Blog). Bonyeza hapa usome blogu yangu ya African Perpective. Ahsante sana kwa kura yako.

NB: Mkutano wetu ni kesho. Ndesanjo ameweka maelekezo mazuri na muhimu sana juu ya mkutano huo.
Bonyeza hapa usome alichokiandika.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:28 AM | Permalink | Maoni 4
Tuesday, November 14, 2006
MKUTANO NI JUMAMOSI,SAA NANE
Baada ya zoezi la kupiga kura ili kuchagua muda muafaka wa mkutano wetu, imeonekana kwamba waliopendekeza saa nane mchana kwa saa za Tanzania wameshinda.Kwa maana hiyo mkutano wetu wa kwanza wa wanablog, wasomaji,wachangiaji,watanzania,mimi na wewe utafanyika Jumamosi ya Tarehe 18 Novemba,2006 kuanzia saa nane mchana kwa saa za Tanzania.

Ukurasa wa wiki wa mapendekezo ya ajenda za mkutano huu bado upo wazi. Unaweza kuupata ukura huo kwa kubonyeza hapa.Unazo haki zote za kimsingi za kuchangia na kutoa mapendekezo yako pale pale.

Shukrani nyingi kwa wote ambao wameshiriki zoezi la kupiga kura ya kuchagua muda.Tunaweza.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 2:04 PM | Permalink | Maoni 4
Sunday, November 12, 2006
SIKU YA MWISHO YA KURA
Kama ilivyotangazwa ijumaa iliyopita, leo ndio siku ya mwisho ya kupiga kura ili kuchagua muda muafaka wa mkutano wetu wa Jumamosi ijayo Tarehe 18 Novemba,2006. Kura zilikuwa zikipigwa hapa. Hivyo kama bado hujapiga kura yako na ungependa kufanya hivyo kabla ya siku hii kumalizika unaweza fanya hivyo kwa kubonyeza hapa na kufuata maelekezo katika ukurasa utakaofunguka.

Halikadhalika, ukurasa wa kuandaa ajenda (zoezi pekee lililobaki) za mkutano wetu upo wazi kwa kila mtu na mapendekezo yanaendelea kutolewa. Fungua hapa uone mapendekezo yaliyokwisha tolewa na pia utoe ya kwako nk.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:34 AM | Permalink | Maoni 2
Friday, November 10, 2006
KAKA YAKE AWILO?


Kama wewe ni mtu wa "viwanja" si ajabu umeshaisikia "Chacarron".Ninachojiuliza mimi ni kwamba huyu sio kaka yake Awilo Longomba kweli? Bonyeza hapo juu ya picha uone mwenyewe.Have fun!
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 2:13 PM | Permalink | Maoni 1
Thursday, November 09, 2006
TUJENGE AJENDA SASA
Siku ya mkutano inazidi kukaribia.Swali ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara ni kwamba ajenda ya mkutano wetu ni nini? Pendekezo la mwanzoni lilikuwa kwamba tutakutana bila ajenda maalumu ili kutoa nafasi kwa wote kushiriki katika kutengeneza ajenda ya mkutano mwingineo. Kwamba tuachane na ukiritimba wa wachache kujifanya machinoo.Ambacho hatukukijua wakati ule ni kwamba inawezekana kabisa tukakutana huku tukiwa tayari na ajenda kibindoni. Tekinolojia bwana....we acha tu!

Kama kawaida,mwenzetu Ndesanjo Macha, ametupatia ufumbuzi wa suala hili. Bonyeza hapa usome ufumbuzi wenyewe na uanze moja kwa moja kushiriki katika uundwaji wa ajenda. Shukrani sana Ndesanjo.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:41 AM | Permalink | Maoni 14
Tuesday, November 07, 2006
KURA YAKO BADO INAHITAJIKA!
Natambua wazi kwamba wengi wetu vichwa bado vichwa vinauma kufuatia tukio la kifo cha mtanzania mwenzetu Hassan Mbonde. Mbonde ameiaga dunia kufuatia mkono wa mtanzania mwenzetu mwingine, mtu tuliyeamini kwamba ni kiongozi na wala sio mtoa roho! Pole nyingi kwa wote walioguswa na msiba huu na ambao wanaamini kwamba kila mtu ana haki ya kuishi hata kama hana kitu,hajulikani kwa yeyote,hana jina linalovuma kama upepo wa nyika.

Matukio kama haya ya kinyama na uonevu ni mengi,yanatokea kila mara. Hili limevuma labda kwa sababu limetokea jijini Dar ambapo angalau kuna vyombo vya habari, kuna wapiga vipyenga (whistle blowers) ambao wasingeweza kukaa kimya.Hawastahili kukaa kimya. Je, ni mangapi yanatokea huko mikoani na wala yasisikike? Ni wananchi wangapi wanaonewa,wanavuliwa utu wao,wanadhalilishwa,wanauawa na wale ambao wanajificha kwenye kivuli cha "ukubwa"?

Ni sababu na tafakuri kama hizi ambazo zinafanya iwe muhimu sana kwa taasisi za umma kuundwa na kuwa imara ili kuhakikisha thamani ya maisha ya kila mtu inaheshimiwa. Haki za kila raia zinaandikwa katika kila paji la uso.Ndio maana mkutano wetu wa Jumamosi Tarehe 18, Novemba,2006 unazidi kuwa muhimu. Bado ukumbi wa kupiga kura ya kuchagua muda upo wazi.Ukumbi utakuwa wazi mpaka Jumapili Tarehe 12, Novemba,2006(wiki hii mwishoni) Baada ya hapo ukumbi wa kupiga kura utafungwa kisha kura zitahesabiwa ili tuafikiane rasmi muda muafaka wa kukutana. Mpaka hivi sasa wanaosema tukutane kuanzia saa nane mchana kwa saa za Tanzania wanaongoza.Kama bado hujapiga kura yako tafadhali bonyeza hapa ufanye hivyo.

Kama hukusoma tangazo la kwanza juu ya mkutano huu bonyeza hapa. Ukitaka kujua jinsi gani mkutano huu utafanyika bonyeza hapa. Kumbuka tu kwamba hata kama huna blog bado unakaribishwa kushiriki mkutano huu.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 6:34 PM | Permalink | Maoni 7
Sunday, November 05, 2006
HII NDIYO TANZANIA YA SASA!
Mkuu wa mkoa wa Tabora,Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, ameua kwa kutumia silaha! Hiki ni kisa cha kinyama cha aina yake. Sidhani kama naweza kuelezea vizuri kisa chenyewe.Bonyeza hapa ujisomee.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 1:31 PM | Permalink | Maoni 11
UNGEFANYAJE?

Maandalizi ya mkutano wetu bado yanaendelea. Umuhimu wa kupiga kura yako ili kuchagua muda bado upo na kura yako inahitajika sana. Hivyo bonyeza hapa upige kura yako.

Michezo ya kwenye tarakilishi(computer games) ni mojawapo ya nyanja za maendeleo ya kimtandao ambayo zinazidi kukua kwa kasi sana. Ingawa wanajamii wengi wameishaanza kuihusisha michezo hiyo na mporomoko wa maadili miongoni mwa wanajamii hususani vijana, baadhi ya michezo hiyo ina mafunzo mazuri na pia inaburudisha.(?)

Wiki chache zilizopita,
Shirika La Umoja Wa Mataifa Linaloshughulika na Watoto (UNICEF) lilizindua mchezo wa kwenye tarakilishi unaolenga katika kutoa elimu juu ya ukimwi katika kujikinga na pia kupima. Mchezo huo ambao unapatikana katika lugha ya kiswahili na kiingereza umepewa jina la Ungefanyaje.

Basi kama wewe ni mpenda michezo ya kwenye tarakilishi bonyeza hapa uuone mchezo wenyewe. Mwisho,nini maoni yako kuhusiana na michezo hii ya kwenye tarakilishi? Unadhani njia hii ni muafaka katika kufikisha ujumbe kwa vijana wetu ukizingatia kwamba upatikanaji wa mtandao bado ni adimu?
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:30 AM | Permalink | Maoni 2
Friday, November 03, 2006
TUKUTANE SAA NGAPI?
La mgambo limelia,kuna jambo.Jambo lenyewe ni mkutano wetu wa kwanza wa wanablogu,wachangiaji,wasomaji,wananchi, mimi na wewe.Shukrani nyingi kwa wote ambao wameitikia wito huu kwa haraka na kwa moyo wote. Hii inaonyesha kwamba inawezekana na tunaweza!

Mpaka hivi sasa nadhani wote tumekubaliana na tarehe iliyopendekezwa ya 18 November,2006. Kikubwa kinachobaki ni kuamua muda wa mkutano. Kutokana na sababu mbalimbali kama mahali, upatikanaji wa umeme(hii inatia hasira) nk imeonekana ni wazo zuri kama "demokrasia" ya kura itatumika. Hatuna budi kutenda tunachohubiri,demokrasia.

Hivyo basi, mwenzetu
Ndesanjo Macha, mwanamapinduzi ya tekinolojia, kwa kutumia tekinolojia ijulikanayo kama Doodle, ameturahisishia jinsi ya kuendesha zoezi hilo la kuchagua muda ambao wengi watakuwa wameuchagua. Tafadhali bonyeza hapa uchague muda mzuri wa mkutano.Ukifika pale kumbuka kwamba tarehe ambayo mpaka hivi sasa imeonekana kushinda zingine zote ni 18 Novemba,2006. Mida inayopigiwa kura ni saa sita au saa nane mchana kwa saa za Tanzania.

Naomba radhi kama kuna usumbufu wowote.Kumbuka tu kwamba hii ni mara yetu ya kwanza na tuna mengi ya kujifunza kwa sababu safari ndio kwanza tunaianza. Pia kama hujasoma bado alichoandika
Ndesanjo kuhusu tekinolojia tutakayotumia, mitabendi, nk basi bonyeza hapa. Usisahau kumpa habari hizi mwenzako ambaye unadhani hajazipata bado.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:25 AM | Permalink | Maoni 10
Tuesday, October 31, 2006
MKUTANO WA KWANZA WA WANABLOG WA KITANZANIA!

Kama unasoma habari hii nina uhakika kwamba wewe ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya Tanzania, ya kitanzania na watanzania nyumbani Tanzania na popote tulipo ulimwenguni.Pia nadhani sitokosea sana kama wewe ni mmojawapo wa watanzania waliotapakaa sehemu mbalimbali za dunia na ambao tayari wanaendesha au kumiliki chombo kipya cha mawasiliano ya umma yaani blog( jina mbadala la kiswahili bado lina mjadala kidogo)

Isitoshe nina uhakika kwamba umeshajionea au kuona jinsi ambavyo nchi yetu inasonga mbele au kurudi nyuma. Kutegemea na jinsi unavyoona wewe inawezekana unafurahia au unashikwa na hasira, unakata tamaa na wala usijue la kufanya(mimi ni mmojawapo).

Binafsi naiona hasira ya wananchi kutoka kila kona,hasira ambayo wakati mwingine inafanya hata uwezo wa watu kufikiri kwa nia ya kupata ufumbuzi inapotea. Huwa sishangai wananchi wakimimina matusi tu kwa mfano pale kwa
Michuzi.Hawa watu sio vichaa,ni hasira ndio inawaongoza.

Ukweli mwepesi ni kwamba nguvu ya siasa katika kuleta mabadiliko ya kijamii nchini Tanzania haitii imani tena. Kuna kitu kinamiss. Miaka zaidi ya arobaini inatosha kukupa picha halisi.

Katika kujaribu kuangalia jinsi gani tunaweza kushiriki katika maendeleo halisi ya nchi yetu ni wazi kwamba nguvu ya wananchi, nguvu ya umma, ambayo nadhani bado haijatumika ipasavyo, inahitajika kuliko wakati mwingine wowote. Katika nchi zilizoendelea taasisi za kijamii (civil societies) ndizo zimekuwa chachu muhimu ya maendeleo yao. Kwa bahati mbaya za kwetu hazina uhai.

Kufumba na kufumbua, imejitokeza nyenzo muhimu sana ya kuunda upya nguvu hii ya umma. Nguvu hii inaitwa blogu. Ziada ya nguvu hii ni kwamba sio tu inaweza kutumika kama chombo muhimu cha nguvu ya umma bali pia inatoa burudani, inaelimisha, inajenga uzalendo, inaamsha fikra na ikitumika vizuri inaweza kabisa kuandika katiba mpya! Haishangazi basi kuona kwamba wanasiasa maarufu duniani,maraisi, mawaziri,wabunge,washika dau chungu mbovu wanamiliki blog pia. Ushahidi upo wazi kwamba wanasiasa na viongozi wetu wa Tanzania ni wasomaji wazuri wa blogu za watanzania.Ujumbe muhimu unawafikia na hivyo kuathiri uundaji wa sera mbalimbali.

Lakini ni muhimu sana ieleweke kwamba blogu sio uwanja wa siasa. Blogu hivi sasa ni jamii.Jamii ina watu wa kila aina. Ndio maana hata blogu za kitanzania sio zote zinazojadili masuala ya kisiasa peke yake. Ukweli ni kwamba wanablogu wengi wa kitanzania (nikiwemo mimi) sio wanasiasa hata kidogo. Ni watu tu wenye mapenzi na nchi yao na wanaotamani kuona nchi yao ikipiga hatua. Hivyo basi watatumia njia kadhaa kama sanaa, siasa, elimu nk kuhakikisha ujumbe muhimu unawafikia walengwa.

Ingawa idadi ya blogu za kitanzania (za lugha kadhaa za kiafrika, kizungu na kwa wingi kiswahili) zimekuwa zikiongezeka kila mara na hata kuushangaza ulimwengu wa blogsphere, hatujapata nafasi ya “kukutana”. Nia imekuwepo, sababu zimekuwepo, mipango ya muda na jinsi ya kukutana ndio imekuwa migumu. Habari njema ni kwamba sasa tunaweza kukutana kwa kutumia tekinolojia hizi hizi za mitandao ambazo zimetuwezesha baadhi yetu kufahamiana bila hata kuwahi kukutana!

Kikubwa kilichobaki ni sisi wenyewe kuamua lini tunataka tukutane, saa ngapi (tukizingatia uwepo wetu katika maeneo mbalimbali ya dunia, upatikanaji wa mtandao kwa wale wanaotumia migahawa ya mtandao nk) Mwenzetu Ndesanjo Macha amejitolea kutambulisha na kuunda mitabendi rahisi ambazo zitawezesha kukutana kwetu. Atatoa maelekezo zaidi tukishakubaliana kukutana.

Nimeweza kuwafikia baadhi yenu na wengi mmependekeza kwamba tunaweza kukutana siku ya Jumamosi, Tarehe 18 Novemba, 2006 kuanzia Saa Sita Kamili Mchana kwa saa za Tanzania. Sasa ili kuwa na demokrasia kamili ni muhimu kama nyote mtatoa maoni yenu hapa na kusema kama mnadhani tarehe hiyo hapo juu, siku, muda na saa ni muafaka ili maandalizi mengine yaendelee.

Nia kuu ya mkutano huu ni kukutana. Hapatakuwa na ajenda maalumu. Ajenda ya kikao kitakachofuata baada ya hiki itaundwa na washiriki wote ili kuondoa tabia ya “wachache” kuunda ajenda wanazozitaka wenyewe.

Wasiokuwa na blogu pia wanakaribishwa sana katika mkutano huu.

Naomba kuwasilisha!




 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:42 PM | Permalink | Maoni 28
Monday, October 30, 2006
TUJENGE UTAMADUNI WA KUWAJIBIKA TUNAPOKOSEA
Nadhani wengi wenu mnajua kwamba mimi ni mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima siku ya jumapili. Kwa wale ambao hamkupata nafasi ya kusoma nilichoandika jumapili ya jana, unaweza kupata waraka huo kwa kubonyeza hapa. Waraka umebebwa na kichwa cha habari kilichopo hapo juu. Nakutakia wiki njema.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:18 AM | Permalink | Maoni 2
Saturday, October 28, 2006
UTALII WA MJINI

Utalii ni nyanja ambayo inaziingizia serikali za miji,majiji,vijiji,kata,wilaya nk kipato kikubwa kutokana na mapato yatokanayo na shughuli nzima ya utalii. Kama unavyoweza kuona katika picha hiyo hapo juu, gari hilo la manjano ni moja ya magari mengi jijini Toronto yanayofanya kazi ya kutembeza watalii. Jina maarufu la magari hayo ni "sight seeing vehicles".Toronto ni makao makuu ya serikali ya jimbo la Ontario na ndio jiji maarufu zaidi kushinda yote nchini Canada na inawezekana ndio linaongoza kwa shughuli za kibiashara na hivyo kuwa "commercial city headquarters"

Wakati utalii ukizifaidisha nchi chungu mbovu duniani, Tanzania bado inazembea sana kuhusu utalii. Wananchi wanaoishi kwenye "visima" vya utalii nchini Tanzania bado hali za maisha yao ni duni sana. Utalii wa ndani bado ni wa kusadikika huku nchi za jirani kama Kenya zikiendelea kufaidi "visima" vya utalii vilivyopo Tanzania kwa mfano mlima Kilimanjaro,mbuga za wanyama za Serengeti,Ngorongoro,Manyara nk kwa sababu watalii wengi hutua kwanza nchini Kenya na kisha kuingia mikataba na makampuni ya utalii ya Kenya kwa minajili ya kuwapeleka vilipo "visima" hivyo. Kampuni hizi za Kenya hazifanyi kosa lolote, zinatumia nafasi zinazojitokeza ambazo zingeweza kutokuwepo endapo wizara yetu ya utalii kwa kushirikiana na bodi ya utalii zingekuwa na mikakati endelevu kuhakikisha watalii wanatua Tanzania kwanza. Njia pekee ni matangazo na sio vipeperushi vinavyopigwa vumbi katika balozi zetu mbalimbali duniani.

Lingine ni ukweli kwamba serikali ya Tanzania kupitia wizara ya utalii imeshindwa kabisa kuyahifadhi,kuyatengeneza maeneo ya kihistoria ambayo ni maarufu duniani kwa kuleta wataliii. Mfano mzuri ni kama vile Bagamoyo. Kama uliwahi kutembelea Bagamoyo utakuwa uliona sehemu ambayo bado ina minyororo waliyofungwa mababu zetu enzi hizo za biashara ya utumwa. Nasikia alama kama zile za kihistoria ambazo zingekuwa chanzo kizuri sana cha utalii zinatokomea taratibu kama bado hazijauzwa kwa "wawekezaji" ambao hawana uchungu na historia yetu hata kidogo.Hawana sababu ya kuwa nayo.


Kuna tofauti gani kati ya Bagamoyo na Gore Island nchini Senegal sehemu ambayo kwa mwaka hushuhudia maelfu ya watalii? Watalii wangapi wanaenda mkoani Iringa kutembelea ngome ya Mkwawa? Wangapi wangemiminika huko kama ingekuwa ni sehemu iliyotengenezwa vizuri kwa minajili ya utalii? Utalii sio kutembelea mbuga za wanyama tu. Watu wengi hupenda kutembelea maeneo ya kihistoria(nikiwemo mimi). Tuamke sasa!
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 4:44 PM | Permalink | Maoni 3
Thursday, October 26, 2006
TATIZO LA KIUFUNDI
Kwa takriban siku moja na nusu blog yangu ilikuwa na matatizo ya kufunguka. Pole na samahani kwenu nyote mliopata usumbufu,shida na karaha mlipokuwa mkijaribu kunitembelea. Naamini kwamba hivi sasa imetengemaa na moto ni ule ule.

Simon Kitururu, asante kwa kunikumbusha kuhusu tatizo la kutofunguka kwa kutumia ile blog yangu ya kizungu. Ahsante sana.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 6:23 PM | Permalink | Maoni 2
Tuesday, October 24, 2006
NATAKA CHEZA DOGORI

Nawaona wananipungia. Unaweza dhani wamekuwa punguani. Hawataki kukutana nami uso kwa uso. Wamejaa soni. Wamekunywa yohana mtembezi kupita kiwango. Hawanipendi eti kwa sababu napenda msondo na siishi kutumia Kiswahili. Wanasema maisha yatanipiga chenga siku zote kwa sababu sitaki kujifunza lugha ya wenyewe yaani kizungu. Wananiita msimbo ili wazungu wawaone wao wa maana zaidi.

Wanacheka mavazi yangu eti yana makunyanzi na sio kama yao ya kizungu. Ithibati juu ya hili haionekani. Kwikwi zangu ni juu yao.Wamekubali kuwa watumwa. Natami niwavishe kafani, roho zao zimeshatutoka.

Wanakuwa kama watoto wanaochezea mapulizo. Wanatamani wanilishe punju. Wanashindwa kwa sababu mimi sichezi pungwa kama wao.Wanashindwa wanione wapi. Sina jinsi ya kuweza fikia itifaki nao.

Nalia mimi.

Pichani ni usafiri maarufu jijini Toronto ama subway kwa jina maarufu. Nasikia Dar-es-salaam nayo itakuwa na subway siku si nyingi.Ni kweli?
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:52 AM | Permalink | Maoni 4
Monday, October 16, 2006
UNATAKA KUSIMAMA NAMI?
Afrika inateketea, Tanzania inazidi kuyoyoma kutoka kwenye ramani ya ulimwengu. Hivi karibuni itakuwa tena koloni. Koloni lisilo na mtawala. Watazame. Wanarudi kimya kimya. Wananchi wamekata tamaa. Wameamini maneno ya wageni, nyie ni masikini. Hamna mnaloweza kufanya bila msaada wetu. Akili zimetekwa nyara. Tunauana wenyewe kupitia rushwa,ufujaji wa mali, ubadhirifu. Tunapigana kuliko wanyama. Tumechoka,hayo ni maneno ya baadhi yetu. Mwenye nguvu ndio ataishi, hii ndio njia ya maisha yetu.

Kiongozi hajali tena wananchi wake. Anajali zaidi tumbo lake, la familia yake. Anapayuka majukwaani kwa sauti ya radi. Anaongopa bila aibu. Kijasho chembamba kinamtoka pindi tunapouliza maswali magumu, ziko wapi kodi zetu? Anachekacheka huku anashika tumbo lake,akichoka kushika tumbo anashika sharubu zake. Amejaa unafiki, ananuka uroho wa madaraka. Kavalia suti ya marumaru, anamkenulia mtoto aliye tumbo wazi, mtoto mwenye njaa kali.Kinywani kwake kajiwekesha kijiti cha kutoholea vijinyama kutoka kwenye meno. Yeye kashiba.

Huyu tuliyenae ndio mkoloni mpya. Ameshika fimbo,ameshika kisu kikali. Anatukata bila huruma. Anasema maneno yale yale ya mkoloni. Aibu machoni kwake haionekani, achilia mbali moyoni mwake. Anaitwa mtumishi wa umma wakati umma ndio unaomtumikia yeye. Hawezi hata kufunga mkanda kwenye gari lake. Mikoba yake hatuna budi kumbebea. Akitembelea jimbo lake tunatamani tupige deki barabara zote. Kazi yake ni kuweka sahihi mikataba asiyoisoma. Anapata ten percent. Anaua jamii yake. Midomo yake miekundu kama damu, imejaa damu. Maisha ya watu keyachezea. Utumishi huu utumishi gani?

Tafadhali nipatie kikombe cha maji, kiu kimenibana kupita kiasi. Moyo wangu umejaa hasira na huzuni. Najua ninachotakiwa kufanya, bahati mbaya ni kwamba siwezi kukifanya peke yangu. Naomba msaada wako. Simama na mimi nisimame, sote tumzonge adui. Tumpe heshima kama anastahili. Kama anastahili adhabu basi tusisite. Nimechoka.

Nimechoka kuona ndugu zangu wanaishi kizani. Eti wanaishi mijini. Ama kweli dunia hadaa na ulimwengu shujaa.Amani inamsaidia nani eti? Nimechoka kuona mbwa wa Ulaya ana maisha mazuri kuliko binadamu. Nimechoka kusikia mapambio ya kinafiki. Ahadi hizi mpaka lini? Nataka kusimama,naomba tusimame pamoja. Nchi yetu inayoyoma.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:01 PM | Permalink | Maoni 10
Saturday, October 14, 2006
TUNAPOMKUMBUKA NYERERE!
(Picha kwa niaba ya Issa Michuzi)

Kama mtanzania, leo sina budi kuungana na watanzania wenzangu duniani kote kuadhimisha miaka 7 tangu Mwalimu J.K.Nyerere aage dunia kule Uingereza. Nafanya hivi kwa heshima niliyonayo juu ya kiongozi huyu aliyeongoza mapambano dhidi ya ukoloni na ukombozi wa bara zima la Afrika. Kinachomtofautisha Nyerere na viongozi wengine ni nia safi, imani halisi katika ukombozi wa muafrika.

Kinachotakiwa kufanyika hivi leo ni tafakuri za dhati juu ya uongozi wa Mwalimu,nini alikisimamia,nini alikiamini na kwa namna gani alifanikiwa au alishindwa. Tafakuri za namna hii sio tu zitatusaidia kujua historia bali kupanga vizuri mikakati ya taifa letu. Hatuwezi kuepuka kirahisi (pengine hatuna hata sababu) misingi waliyotuwekea Mwalimu na viongozi wenzake wa wakati ule. Mwalimu alijaribu. Kama binadamu yoyote yapo aliyokosea.Mimi nimemsamehe kwa sababu aliposhindwa alikiri, japo inawezekana kwamba alichelewa kukiri au kukubali kwamba amechemsha.

Kwa bahati mbaya siku hii ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imetekwa nyara ya wakora wa siasa. Leo hii utasikia hotuba chungu mbovu,utasikia neno "tumuenzi" kuliko neno lingine lolote. Hili hutia hasira kupita kiasi.Ukitaka kujua kiwango cha unafiki miongoni mwa viongozi wetu basi nenda tu viwanjani,majukwaani nk ukasikilize hotuba za viongozi katika maadhimisho haya. Naamini kabisa kwamba endapo viongozi wetu wangeitumia siku hii kujifanyia personal analysis ya uongozi wao basi "nchi ya ahadi" haingekuwa mbali kama ilivyo sasa.

Katika maadhimisho haya mwaka jana
niliandika namna hii (usisahau kusoma maoni ya wachangiaji). Ningeweza kabisa kuiweka makala ile kama ilivyo kwa sababu hakijabadilika kitu. Pengine swali ambalo sote tunabidi tujiulize ni unafiki umepungua au umeongezeka? Jibu sahihi unalo wewe msomaji. Hivi unadhani Nyerere angekuwa hai na kiongozi wa nchi angeweza kutokea Cuba kwenye mkutano wa nchi zisizofungamana na upande wowote na kisha kukimbilia Washington kupiga stori na "mkuu wa mabepari"? Unapoongelea kumuenzi Mwalimu unakuwa unamaanisha moja au mbili?

Tupende, tusipende jina la Nyerere limebakia kuwa nembo ya kisiasa tu.Viongozi wetu wa sasa wameamua,kwa makusudi, kulizika jina lake kwa "kutomuenzi" kama ahadi zao za kisiasa zinavyosema kila siku. Wanaolia na kumkumbuka kwa dhati ni wananchi wa kawaida ambao nao wanafanya hivyo kwa imani tu kwamba huenda angekuwa hai hili na lile lisingekuwa kama lilivyo hivi sasa. Huenda angeshazidiwa nguvu na majangili. Dalili za kuzidiwa nguvu zilianza kuonekana tangu akiwa hai. Unakumbuka msururu wa watu waliotaka kwenda ikulu mwaka 1995? Unajua wako wapi aliowakemea? Unajua mali wasizoweza kuzitolea hesabu zimeongezeka au zimepungua? Sasa nani anakudanganya kwamba kuna falsafa ya Mwalimu iliyobakia?


Yana mwisho haya.Tafakari.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:03 AM | Permalink | Maoni 4
Wednesday, October 11, 2006
MUZIKI WA KIZAZI KIPYA, UZALENDO, UTUMWA MPYA

Hapa chini ni makala niliyowahi kuandika siku za nyuma juu ya muziki wa kizazi kipya.Mmojawapo wa wasomaji wangu aliniomba nijadili suala hili. Kwa sababu suala hili lilishawahi kujadiliwa na mimi kuliandika nimeona ni bora kuiweka hapa makala nzima.

Siku chache za nyuma niliandika juu ya kuchipuka kwa umaarufu wa muziki wa kizazi kipya. Pia niliandika kuhusu umuhimu wa kuunga mkono muziki huu unaoitwa wa kizazi kipya ama Bongo Flava. Kilio changu kilikuwa tuwaunge mkono wanamuziki hawa wa kizazi kipya kwa sababu sio tu kwamba wanatuburudisha bali pia wanatupa utamaduni mpya kupitia muziki. Kiufupi tunakuwa na chetu wenyewe ingawa kimsingi tumeiga kutoka kwenye utamaduni wa muziki wa hip hop ambao ni maarufu sana Marekani miongoni mwa jamii ya watu weusi(black Americans au African-Americans).

Nilitoa ombi kwa watu kununua cds au kaseti halali na kuachana na ule mchezo wa kurekodi ovyo ovyo bila kuzingatia jasho la msanii.Hapa ningeweza kuwaunganisha na wale wezi wa kazi za wanablogu bila idhini yao.Hoja yangu ilikuwa kama tunataka muziki huu uendelee na pengine baadaye kuwa kitambulisho cha vijana wetu duniani kote basi lazima tuunge mkono ili ukue.Njia pekee ya kuweza kufanikisha hilo ni kununua kazi halali za wasanii hao. Sina uhakika kama ombi langu lilisikika au la.

Baada ya hapo nikabakia kuwa mpenzi na mnunuzi mkubwa wa muziki huo. Ingawa mpaka hivi sasa nabakia kuwa mnazi wa muziki huu nakatishwa tamaa na jinsi wasanii wenyewe wanavyotaka kuutangaza muziki huu. Ninashindwa kabisa kuelewa kwamba kwanini muziki huo unazidi kuonekana wa kimarekani siku baada ya siku? Matumaini ya kwamba siku moja muziki huu utakuwa kitambulisho chetu kipya cha vijana wetu,sanaa zetu, tamaduni zetu nk yanakuwa finyu siku baada ya siku.

Majuzi nimeletewa baadhi ya dvd za muziki huo.Jambo moja ambalo lilikuwa wazi kabisa ni kwamba kila mmoja anajaribu kuiga utamaduni wa mtu mweusi wa marekani kwa udi na uvumba.Nimeona katika hizi video watu wamevaa vilemba( tena vya bendera ya Marekani!) hereni ,wamesuka,wakavaa masuruali makubwa makubwa,wakaghani kama vile kina 50 Cent,kina Jay Z nk. Kitambulisho kwa muziki huu unatokea Tanzania hakipo kabisa! Nimejaribu kuwaonyesha watu mbalimbali video hizi na kila mmoja anaponirudishia kaseti zangu ananiambia suala moja.Ingependeza zaidi kama wasingekuwa wanajaribu kuiga utamaduni wa kimarekani. Ni dhahiri kwamba kila mtu analiona hilo na halitii mvuto wowote kwa kweli.

Natambua kwamba zimekuwepo hoja kama upi basi ni utamaduni wa mtanzania? Swali hili linapoulizwa mimi huwa na masuala mawili kichwani kwangu.Moja kama una umri zaidi ya miaka 20 kwa mfano na bado hujui utamaduni wako kama mtanzania basi pana tatizo kubwa. Pili huwa nasikitika, nakumbuka hoja aliyowahi kuitoa Mwalimu Nyerere juu ya dhambi kubwa kupita zote walizofanya wakoloni, ya kutuambia tamaduni zetu hazifai, tusitupe jalalani. Kumbe basi tamaduni zetu zipo,zilikuwepo na tunaweza kuziendeleza kama tukitaka huku tukiziboresha.

Nimejaribu kutafuta kama kuna mwanamuziki wa kizazi kipya anayeendana na utamaduni wa kiafrika bila mafanikio.Nia ilikuwa ni kualika mwanamuziki kutoka Tanzania kwa ajili ya Tamasha la kila mwaka hapa Toronto linaloitwa AfroFest. Sasa nitaanzia wapi kama kila nimuonaye anajifanya mmarekani kuliko hata wamarekani wenyewe? Hivi kweli kuna maana yoyote kumleta mpaka hapa mwanamuziki kutoka Afrika ya Mashariki kisha akuonyeshe jinsi gani alivyo mahiri wa kumuiga Jay Z,50 Cent,Lil’ John nk? Ungekuwa wewe ungefanyaje? Najua wapo wanamuziki wanaondamana na utamaduni wa kitanzania au kiafrika,sijapata mawasiliano nao.Kama unayo tafadhali nipatie.

Ukweli ni kwamba kama wanamuziki wetu wanataka kuuza kimataifa basi ni lazima wajifunze utamaduni mpya.Tuliiga mtiririko wenyewe wa hip hop,sio lazima tuige mavazi na video zao.Kwa mtaji huu hamna mzungu au mmarekani atakayetaka kununua muziki wetu.Kwanini anunue wakati anapata kitu hicho hicho,kwa lugha yake na kwa bei nafuu zaidi kama anataka muziki wa aina hiyo? Lazima wanamuziki wetu wawe wabunifu.Kuiga kidogo sio mbaya lakini hili mnalofanya hivi sasa halitowafikisha mahali popote.Ila kama nia yako ni kuendelea kupata jina kubwa wakati huna senti mfukoni basi endelea na utaratibu wako wa kuwa mtumwa wa kiakili na kimtazamo.

Najua kuna huu utamaduni wa watu weupe siku zote kupenda kutuona sisi waafrika tumevaa majani,ngozi za wanyama tukikata viuno na kuona huo ndio utamu wenyewe.Sina hakika kama sisi wenyewe tunapenda kuonekana hivyo. Lakini kama hatupendi basi hatuna budi kuboresha muziki wetu kwa kubuni na kujivunia mavazi yetu,(sio ngozi na majani) miondoko yetu nk. Hapo ndio muziki wetu na wanamuziki wenyewe wataingia kwenye ulimwengu wa muziki kimataifa.

Nimewahi kusoma kwenye magazeti na mitandao mbalimbali inayowapa sifa hewa watanzania kwamba hivi sasa mwanamuziki fulani anakuwa wa kimataifa kwa sababu amealikwa kufanya maonyesho Marekani,Canada,Uingereza nk. Kwangu mimi kama unakuja hapa kutumbuiza watanzania waishio hapa basi wewe bado sio wa kimataifa. Utakuwa wa kimataifa pale muziki wako utakapouzika kwa watu wa jamii na tamaduni zingine,pale utakapopanda jukwaani kutumbuiza mashabiki wa tamaduni mchanganyiko. Kuna umataifa gani kuja kunitumbuiza mimi na rafiki zangu tuishio hapa Toronto? Kupanda ndege ndio umataifa ndugu zangu?

Hivi kuna ugumu gani wa mwanamuziki fulani wa bongo flava kuamua kuvaa mavazi ya kiafrika tu?Mbona yanapendeza na kukubalika dunia nzima? Hapa Canada mavazi ya kiafrika ni ghali kuliko nguo za aina zote. Unaona sifa gani kuvaa nguo iliyoandikwa Toronto,New York,Washington nk wakati hujawahi hata kufika sehemu hizo? Hivi ukionekana na nguo iliyoandikwa Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa,Arusha nk ni ushamba?

Utumwa wa akili huanzia hapo.Unapoona kwamba chako sio bora bali cha mwenzio.Unapoona kila kizuri ni cha mzungu. Jogoo lililonona ni la mzungu,kuku mweupe ni wa kizungu,nyumba nzuri ni ya kizungu nk. Kama huthamini mavazi yaliyotengenezwa nyumbani kwetu Tanzania kwa kuyanunua na kuyavaa,kama huthamini bidhaa za kwetu,kama huthamini mazao ya kwetu unalalamika nini kuona hali ya uchumi inazidi kuwa mbaya? Kwanini unaenda kununua machungwa yaliyotoka Afrika ya Kusini wakati yale ya Lushoto ni bora zaidi? Unadhani nani anastahili lawama katika hili; raisi, serikali au mwananchi?

Wenzetu wa Afrika ya magharibi wanaheshimika kwa kushikilia tamaduni zao ingawa sio wote wafanyao hivyo. Mavazi yao yanathaminiwa dunia nzima. Upuuzi huu wa kutothamini mavazi fulani ndio hupelekea siku nyingine ukialikwa kwenye tafrija fulani unaambiwa kwamba vazi rasmi ni suti nyeusi.Kataa! Shati la kitenge au wax sio nguo?Usikubali kuwa mtumwa wa kiakili ndugu yangu.Jivunie chako.

Picha nadhani zinajieleza zenyewe.Hao vijana mbele ya bendera ni watanzania?
NB.Naendelea kujifunza masuala ya photoshop. Mwalimu wangu ni Scout wa http://harper-valley.blogspot.com/
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:55 AM | Permalink | Maoni 3
Wednesday, October 04, 2006
KAZI NI KAZI?

Waafrika au niseme watanzania tunao msemo unaosema kazi ni kazi, ili mradi mkono uende kinywani. Nadhani wazee wetu walipoutunga msemo huu walimaanisha tusichague kazi,tufanye kazi yeyote iliyopo mbele yetu. Nadhani nitakuwa sijakosea nikisema msemo huu ni mzuri na kama wengi wetu tungeuzingatia basi pengine yale makundi ya vijiweni kila kukicha yangepungua.

Unadhani msemo huu unazingatiwa? Nipe maoni yako. Pichani ni jamaa akiwa kazini jijini Toronto. Anatangaza bidhaa kwa ajili ya watoto huku akiwasaidia kupuliza maputo yao.Kazi ni kazi? Hebu malizia kwa kusoma
makala hii hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:09 PM | Permalink | Maoni 4
Friday, September 29, 2006
NANI MTOTO KATI YA HAWA?

Maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga. Msemo huu wa kiswahili nadhani una maana nyingi kuliko nilivyokuwa nikifikiria. Nguo ni nini katika msemo huu,maji je? Maswali haya yanakuwa mengi pindi "habari za aibu" za aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi la polisi Tanzania zilipotinga kwenye vyombo vya habari. Hapo ndipo ninaposema, ukishayavulia chupi..huna budi... Kwa habari zaidi juu ya mkasa huu bonyeza hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:32 AM | Permalink | Maoni 8
Monday, September 25, 2006
NINI KINAUZWA HAPA?

Ulimwengu wa biashara siku hizi unaenda sambamba na ubunifu mkubwa wa jinsi ya kutangaza bidhaa au huduma kwa jamii. Haishangazi basi kusikia kwamba mabilioni ya fedha hutumika katika nyanja hiyo muhimu ya kujitangaza.

Ukweli ni kwamba yapo matangazo ambayo yanavutia kiasi kwamba unaweza kununua usichokihitaji (commercials makes you buy what you do not need).Kuna umuhimu sana wa kujiuliza je hiki kitu ninachotaka kukinunua nakihitaji au nakitaka tu?


Majuzi katika pita pita yangu jijini Toronto,nimekuta hiki kigari kilichozungukwa na asasi za jikoni kimeanikwa juani.Unadhani nini kinauzwa hapa? Hicho kigari au hivyo vyombo?
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:14 PM | Permalink | Maoni 2
Friday, September 22, 2006
ZANZIBAR NDANI YA TORONTO!

Siku za nyuma niliwahi kuibandika hii picha hapa ubaoni. Niliahidi kwamba ningali namsaka mmiliki wa sehemu hii ili aeleze kwa kifupi uhusiano wa visiwa vya Zanzibar na hii sehemu ambayo shughuli zake haziendani na maadili ya visiwa vya Zanzibar ambavyo ni sehemu muhimu sana ya nchi yetu ya Tanzania.Ukitoa Zanzibar hakuna tena Tanzania bali Tanganyika. Ukibonyeza juu ya hiyo picha ukasoma maandishi yaliyopo nje utagundua nini naongelea kuhusu shughuli zinazofanyika humo ndani.

Kwa bahati mbaya mpaka hivi leo sijafanikiwa kuonana na mmiliki wa kibanda hii. Nilimuachia simu yangu anipigie lakini naona mpaka leo kimya. Nimeamua kuibandika tena picha hii ili kama kuna ambaye anajua uhusiano wa Zanzibar hii ya Toronto na ile ya Pemba na Unguja atusaidie.Unadhani hii inapotosha watalii wanaotaka kuvitembelea visiwa vya zanzibar au ndio inachangia watalii wengi kumiminikia Zanzibar wakiwa na yao kichwani? Unaweza oanisha habari hii na ile ya majuzi kumhusu Mercury? Isome
hapa.

Uchunguzi kidogo nilioufanya unaonyesha kwamba hizi Zanzibar ziko nyingi sana huku ughaibuni. Zote zina shughuli zinazoendana.Mfano angalia hapa au hapa Kwanini?Kulikoni?
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:06 AM | Permalink | Maoni 6
Wednesday, September 20, 2006
ANOTHER NIGHTMARE!

Wakati viongozi wa dunia wanakutana New York,Marekani yapo machache ambayo yananivutia. Kubwa ni hotuba ya raisi wa Iran Mahmoud Ahmadinejad kuhusu anachokiamini,kinachofanyika nchini mwake kuhusiana na tekinolojia ya nyuklia na jinsi ambavyo anaelezea ubabe wa nchi za magharibi. Unaweza isoma hutuba yake kamili kwa kubonyeza hapa.

Bado nasubiri kusikia atakachokisema(pengine ninavyoandika ashasema) raisi wa Tanzania-JK. Mpaka leo sijaweza kupata hasa msimamo wa raisi wangu. Nadhani hili linatokana na wingi wa siasa katika maneno yake. JK hapendi kuudhi mtu,anapenda kupendwa na kusifiwa tu. Ukimuuliza swali atakujibu unachotaka kusikia.Alichokisema huko Havana-Cuba siku chache zilizopita kilionekana kuwa cha maana. Lakini umaana huo unapotoshwa kabisa unapoona kutoka Havana alikimbilia Washington kuonana,kusabahiana,kunywa kahawa na kujikomba kwa raisi George Bush wa Marekani ambaye kimsingi nchi yake ndio adui mkubwa wa nchi zinazosema hazifungamani na upande wowote. Sishabikii viongozi wa dunia kuonyeshana ubabe kila mara ila nadhani kuna wakati maneno ya majukwaani lazima yaendane na vitendo. Msimamo wetu,wa raisi,au nchi yetu ni upi hasa? Nadhani lazima tufikie mahali tueleweke. Tutaheshimika zaidi namna hiyo. Political prostitution sio sifa nzuri hata kidogo.

Yote hayo tisa. Miezi michache iliyopita sinema ya Darwin's Nightmare ilizua janga huko Tanzania. Wimbo wetu wa taifa ukawa "mapanki". Wanasiasa kupitia bunge wakatuonyesha rangi zao halisi juu ya nini wanakijua,nini wanakizingatia nk. Wapiga kelele kama mimi tukaandika. Ukitaka kusoma nilichoandika
bonyeza hapa.

Sasa majuzi nimetumiwa sinema nyingine. Hii ni kuhusu child labour. Imepigwa kule Mererani,kule kule yanakochimbwa madini adimu ambayo serikali yetu imeshindwa kabisa kuyaona kama urithi wa kipekee wa nchi yetu. Najaribu kujiuliza,je safari hii raisi wetu atasema nini? Wabunge wetu watasema nini? Unaweza kuitazama sinema yenyewe kwa
kubonyeza hapa. Pia unaweza kusoma ripoti ya jamaa wa IRINnews kwa kubonyeza hapa.

Picha ya juu kwa niaba ya Michuzi wa www.issamichuzi.blogspot.com. Pichani ni vijana wa Mererani wakisaka Tanzanite. Huko ndiko child labor inapozidi kuota mizizi.


 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:56 AM | Permalink | Maoni 6
Friday, September 15, 2006
WANAUME HAWA BWANA

Wakati wa mkutano wa kimataifa wa masuala ya ukimwi hapa Toronto mwezi uliopita, yalikuwepo mambo mengi sana ya kujifunza, kutathmini na kisha kujiuliza wapi tunakwenda. Mojawapo ya mambo ambayo yalikuwa yakiwashangaza wengi na kwa maoni yangu kupoteza kabisa muelekeo wa mkutano wenyewe ni masuala ya haki za wasenge na watu wanaohama kutoka kwenye jinsia moja kwenda nyingine (transgenders).

Kimsingi katika nyakati nyingi mkutano ulikuwa unageuka kutoka kwenye majadiliano ya ugonjwa wa ukimwi,tafiti za tiba nk na kuwa jukwaa la haki za binadamu. Inavyoelekea siku hizi ni vigumu sana kutenganisha siasa,haki za binadamu na ukimwi. Kilichokuwa kinanipa tabu zaidi ni kujaribu kuingia vichwani mwa waalikwa kutoka Afrika ambako masuala haya ya ndoa za jinsia moja,usenge na hata transgenders bado ni ndoto za usiku wa manane. Hivi walikuwa wanajifunza nini? Au ndio mbinu ya kuwaanda "kuiga" sera hizi za kimagharibi au la waitwe "wasioheshimu haki za binadamu"?

Pichani hao ni transgenders. Hao ni wanaume ambao wako njiani kujigeuza kuwa wanawake. Wao husema muumba alifanya kosa.Unasemaje?

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 1:40 PM | Permalink | Maoni 16
Friday, September 08, 2006
WANAUME WA BLUU

Wiki chache zilizopita niliwaona hawa jamaa wanaoitwa wanaume wa bluu .Ukisoma historia yao utagundua kwamba walianza jamaa watatu kimchezomchezo tu. Historia yao siwezi kuitofautisha na ile ya jamaa fulani pale jijini Dar ambao hupita baa baada ya baa,mtaa baada ya mtaa,wakiwachekesha watu huku wamejipaka masizi na kuweka vitambi vya matambara,tai za ajabu ajabu nk. Pengine wale tunaweza kuwaita Dark Men, kwa sababu wao wanatumia rangi ya masizi ambayo ni nyeusi.

Tanzania kuna vipaji vingi kupita kiasi. Hili hunipa maswali na aibu ndani ya kichwa changu. Hivi kwanini tunashindwa kuviendeleza vipaji? Hapa naongelea sisi wananchi,wenye nchi, kwa sababu kimsingi serikali imeshashindwa.Miaka zaidi ya arubaini bila muelekeo wa maana katika kuendeleza vipaji vya kisanii hakuna maana nyingine zaidi ya kushindwa. Na je,sisi tuliopo ughaibuni,sisi ambao tunaona jinsi gani vikundi kama hawa wanaume wa bluu wanavyofanya kazi tunashindwa nini kuibua vipaji kama hivyo kutoka nyumbani na kuvitangaza kimataifa?
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:07 PM | Permalink | Maoni 4
Wednesday, September 06, 2006
USISAHAU



Mama nieleke. (KITANDA) Mother! Carry me on your back. (BEDSTEAD)

Parr! Hata Makka. (UTELEZI) Prr! straight to Mecca. (SLIPPERINESS

Nende huko na nikirudi nimshike Ngombe wa mama mkia. (KATA YA MAJI) Let me go far away and when I come back let me catch hold of the tail of my mother’s cow. (LADLE for DRINKING WATER)

Nyumba yangu haina milango.(YAI) My house has no door. (EGG)

Kitendawili changu cha ajabu kina matone ya dhahabu. (QURANI TAKATIFU) My wonderful riddle is adorned with spots of gold. (THE HOLY QURAN )

Ubwabwa wa mwana mtamu. (USINGIZI) A child's porridge is delicious. (SLEEP)

Kipo lakini hukioni(KISOGO) It is here but you cannot see it(THE NAPE OF THE NECK)

Nilikuwa nikienda njiani nilipomsikia mtu akinita Wifi! Wifi!” lakini nilipogeuka sikumwona mtu. (MBAAZI KAVU) I was going along the road when I heard a person calling me, Sister -in-law!’but when l turned round there was no one in sight. (DRY PIGEON-PEAS in THEIR PODS)
Nzi hatui juu ya damu ya simba. (MOTO)The fly cannot settle on the lion’s blood. (FIRE)

Bibi mweupe ametupwa mibani. (MACHICHA YA NAZI)The white lady has been thrown upon the thorns. (THE SHREDS OF THE MEAT OF THE COCONUT AFTER THE MiLK HAS BEEN SQUEEZED OUT OF IT)

Pana visu vingi lakini mpini mmoja tu. (CHANA YA NDIZI)There are many knives but only one handle.(A BUNCH OF BANANAS)

Ukiona Njigi’ utadhani ‘Njege’; na unapoona Njege’ utafikiri ‘Njigi’. (MAZIWA NA TUI LA NAZI)If you see ‘Njigi’ you will take it be Njege’;and should you see Njege’ you will ihink it Njigi (COW-MILK AND COCONUT-MILK)

Popoo mbili zavuka mto. (MACHO)Two areca-nuts cross a river. (EYES)

Nyumba yangu ndogo ina madirisha mengi.(DEMA)My house is small but it has many windows. (A FISH- TRAP)
Kombe Ia Mungu Ii wazi (KISIMA)God’s cup is open. (A WELL)

Nimewafungia milango wanangu huku wakipigana(BISI ZIKIKAANGWA) I have shut the door on my children and theyare now fighting. (MAIZE-SEEDS BEINGROASTED)

Nyumba yang kuu ina mlango mdogo.(CHUPA) My house is large but its door is small. (BOTTLE)

Wanangu wote wamevaa vizibao, wasiovaa siWanangu. (KUNGURU WENYE MABAKA MEUPE) My sons wear Waistcoats: those who do not arenot my Sons. (WHITE-BREASTED CR0WS)

Nimeanika mpunga wangu juani lakin, kulipopambazuka sikuuona. (NYOTA) I have put my paddy rice in the sun to dry butwhen day dawned I couldn’t see it. (STARS)

Watoto wangu wote wamevaa kofia, wasiovaa siwanangu. (FUU) All my children have caps on. those withoutare not my children. (FRUIT OF VITEX CUNEATA )

Nina watoto wanne, lakini akiondoka mmojawaliosalia hawafanyi kazi. (MATENDEGU YAKITANDA) My children are four in number but, when onegoes away, the rest cannot work. (THE LEGS OF A BED)

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:08 PM | Permalink | Maoni 5
Saturday, September 02, 2006
INA MAANA GANI?

Hiki ni kisa cha kweli.Mchana wa leo,saa za hapa Toronto,nikiwa katika mihangaiko yangu ya kawaida mwishoni mwa wiki nimekutana na dada huyu pichani.Yeye anatokea visiwa vya St.Vincent(mojawapo ya visiwa vya Carribean).Dada huyu aliponiona nimening'iniza kamera begani akanisihi nimpige picha.Kichwani nilitegemea angetoa ushungi wake ili picha iwe maridhawa zaidi au sura yake ionekane.La hasha,alijitega vizuri kabisa na kuniambia "haya piga".Nikampiga picha na kumuahidi kumtumia baadaye kwenye barua pepe yake.Nishafanya hivyo.
Baada ya hapo nikajishtukia nimejawa na maswali kadha wa kadha.Hivi ina maana gani kupiga picha na hata sura yako isionekane? Hivi huyu naweza kumfananisha na wale watu wanaopenda kutoa maoni kwa kutumia kivuli cha anyonymous? Hivi ina maana gani kutoa maoni kwa kutumia kivuli cha anyonymous huku ukiandika kama vile mwenye blog atakutambua? Rafiki yangu
Michuzi ni victim wa watu wa kivuli hiki.Kwa bahati mbaya wengi huvuka hata mipaka na kufurumusha matusi.Hivi ina maana gani? Hivi ni kweli Tanzania ina watu waoga kiasi hicho au ni kweli kwamba Tanzania haiheshimu uhuru wa kujielezea mpaka watu waogope kuweka maoni yao kwa uhuru,bila kujificha?Si 9/12 huwa ni sikukuu ya uhuru?
Kwa namna moja au nyingine,huwa naelewa,kwa mbali lakini,utoaji wa maoni kwa kivuli cha anyonymous.Naelewa suala la uoga,kutokujiamini au kuwa kwenye witness protectionism acts.Lakini wakati huo huo huwa nashangaa,hivi kama tutashindwa kutumia nguvu ya umma,kama blog,kujielezea,bila kujificha,tutasukuma vipi gurudumu la maendeleo?

Bado nasaka majibu kutoka kwa huyu mwanadada kwamba ina maana gani au inasaidia nini kupiga picha yake huku akiwa ameficha uso?Niambieni wenzangu.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:57 PM | Permalink | Maoni 11
Friday, September 01, 2006
MDUNDIKO

Nani alikudanganya kwamba Toronto hakuna mdundiko? Mbona upo,tena sio wa kawaida. Dada huyu alikuwa akinengua kwenye lile tamasha maarufu la Caribana mwaka huu.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:18 AM | Permalink | Maoni 3
Thursday, August 31, 2006
FELA ANIKULAPO KUTI

Afrika ndio asili ya muziki,muziki na afrika ni mapacha.Haya ni maneno yangu lakini ukweli unabakia kwamba Afrika ni bara ambalo limeshawahi kutoa(pengine linaendelea kutoa,sina uhakika) magwiji wa muziki wa aina yake.

Unapoanza kutaja majina ya magwiji wa muziki wa Afrika huwezi kuacha kulitaja jina la Fela Anikulapo Kuti wa kule Nigeria. Ana rekodi ya kutoa santuri zaidi ya 77 na pia kuoa wake wanaofikia 27! Fela hakuwa mwanamuziki tu bali mwanasiasa,mwana-mapinduzi,mpigania haki,mwafrika wa kweli na mengineyo mengi.

Leo nimepitia mahali fulani na kukuta maandishi mazuri sana kumhusu Fela Kuti na mapicha kibao yanayoelezea historia yake vizuri sana.Bonyeza hapa usome. Ndesanjo hii ni zawadi yako na wengineo wapenda muziki na tamaduni za Afrika.Mti Mkubwa sijui kapotelea wapi.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:47 AM | Permalink | Maoni 0
Tuesday, August 29, 2006
MAZISHI YA BAADHI YA BLOGU!

Zipo siku ambazo hunipa huzuni sana,zipo siku ambazo hunipa furaha sana,zipo pia siku ambazo sizielewi.Nikihoji kuhusu siku nisizozielewa huwa naambiwa nimechanganyikiwa au naanza kuchanganyikiwa.Wanaosema hivyo wananiambia niwe na furaha au masikitiko tu kama binadamu wengi. Sijui nisikilize la nani.

Leo nipo msibani,namalizia kufukia kaburi.Mchanga wangu ni tekinolojia na bahati nzuri ninaowazika hivi leo wanaweza kufufuka,kama wakipenda. Niliwahi kuisikia
tekinolojia ya bloglines ziku nyingi sana zilizopita. Niliheshimu mantiki yake,niliheshimu pia falsafa ya kuokoa muda iliyotumika. Lakini kwa muda mrefu huo huo sikuona umuhimu wake. Huruma ilinijaa.

Leo nimefikia mwisho.Nimechoka kufungua baadhi ya blogu kwa takribani miezi sita bila kukuta lolote jipya.Ukiwauliza wamiliki wa blogu hizo wanadai wako bize.Walipozianzisha blogu zao waliomba kwa nguvu zote watangazwe,wakaahidi kutoa changamoto kubwa uwanjani,wako wapi? Uhuru usiokuwa na majukumu umerudi tena? Hapana bwana,nimechoka.

Sasa leo,baada ya tafakuri nimeamua kuanza rasmi kutumia tekinolojia ya
bloglines.Kama hujaandika kitu hutonisikia,hutoniona kijiweni kwako.Hata kama umeleta bangi ya Malawi,sitaki. Huu ndio msiba wa leo.Nazizika baadhi ya blogu,zile zisizoandika kitu,zile ambazo nguvu ya soda ilishaisha.Ni ukweli,usikasirike. Naamini kwenye nguvu ya habari,naamini bila nguvu hiyo ambayo wenzetu wazungu wanazidi kukomaa nayo,hatutafika,tutasahaulika.Mtanisamehe ndugu zangu msioweka chochote kipya kwenye blog zenu. Kwaherini kwa sasa,mkitaka kufufuka nitakuja kuondoa saruji.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 2:44 PM | Permalink | Maoni 5
Sunday, August 27, 2006
NIAGARA FALLS.


Ukisema ulikwenda kutembea,kuhudhuria mkutano/kongamano,kusoma au kuishi Canada hususani kwenye jimbo la Ontario basi si ajabu ukaulizwa kama uliwahi kupanda/kutembelea CN Tower au kama ulikwenda kuyaona maporomoko ya maji ya Niagara(Niagara Falls). Kwa wale ambao hamjawahi kuyaona au kufika hapo Niagara leo nimeona niwaletee picha ya maporomoko haya nikitumaini kwamba wikiendi yako ilikuwa njema.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:09 PM | Permalink | Maoni 3
Friday, August 25, 2006
PODCAST
Tekinolojia inakua kwa kasi sana. Huu ni msemo mpya,wa kizazi hiki ambacho wengine tunakiita cha .com. Mwanablog mwenzetu Ndesanjo Macha ni mmojawapo ya wanablog ambao wamejikita sana katika kuhakikisha kwamba habari za tekinolojia mpya,hususani kwenye ulimwengu wa habari na mawasiliano hazitupiti. Kila mara unapopitia tovuti yake utakuta ameweka habari zenye mtizamo huo wa tekinolojia.Kwa mfano habari hii na nyinginezo nyingi.

Naamini kwamba wengi hupitia tovuti kama hii ya Ndesanjo na nyinginezo nyingi kwa minajili ya kupata habari za tekinolojia. Mojawapo ni watu kutoka kule Columbus,Ohio (nakumbuka Ndesanjo aliwahi kuishi Ohio) Hawa wameikumbatia tekinolojia ya podcast kwa kasi ya aina yake. Radio Butiama inayoendeshwa na Deus Gunza aliyeko huko Columbus,Ohio ni mfano mzuri wa tekinolojia hii.Ukitaka kusikiliza baadhi ya matangazo yake yakiwemo mahojiano na watu kama mwanamuziki Cosmas Chidumule au mpiga picha maarufu,mwanablog mwenzetu Issa Michuzi bonyeza hapa. Kwa kujua zaidi jinsi gani tekinolojia hii ya podcast inavyofanya kazi bonyeza hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:34 AM | Permalink | Maoni 1
Sunday, August 20, 2006
DARWIN'S NIGHTMARE!
Kuitendea haki nafsi yangu kunakwenda sambamba na kusema bayana yale yaliyomo moyoni. Hii ndio sababu iliyosababisha wiki hii niandike maoni yangu kuhusu sakata la Jinamizi la Darwin ambalo huko nyumbani Tanzania limekuwa la muhimu kuliko sera za nchi na utekelezwaji wake. Soma hapa nilivyoandika katika ule waraka wangu wa kila jumapili katika Tanzania Daima.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:55 PM | Permalink | Maoni 3
Thursday, August 17, 2006
SANAA KAMA NJIA YA KUELIMISHA.

Mambo yanayoendelea kwenye mkutano wa 16 wa masuala ya ukimwi hapa Toronto ni mengi.Inabidi uwe makini sana katika kuchagua mihadhara na shughuli zinazoendelea. Kama unapenda longolongo za wanasiasa utazipata,nyingi tu.Ukipendelea kukutana na watu ambao wamegeuza ugonjwa hatari wa ukimwi kuwa miradi na biashara zao binafsi utawapata pia. Kama unapendelea mambo ya sanaa kama njia muhimu sana ya kuelimishana kuhusu masuala ya ukimwi kama mimi basi hutobanduka kwenye sehemu inayoitwa Global Village. Pichani hao ni vijana wa Msumbiji wakitumia sanaa kuelimisha. Soma habari zao na mchezo wanaocheza kwa kubonyeza hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:41 AM | Permalink | Maoni 0
Monday, August 14, 2006
XVI INTERNATIONAL CONFERENCE ON HIV/AIDS



Mkutano wa 16 wa Ukimwi kwa mwaka 2006 umeanza rasmi jana hapa Toronto,Canada. Zaidi ya washiriki 24,000 kutoka kila pande ya dunia,ikiwemo Tanzania wanashiriki mkutano huu. Ujumbe wa mwaka huu ni kwamba "muda umewadia",wakati wa kuonyesha uwajibikaji kwa vitendo ndio huu. Ninahudhuria baadhi tu ya kongamano nyingi zilizoko kwenye mkutano wote ambao utafanyika kwa takribani wiki moja. Pichani ni jana kwenye uzinduzi rasmi ambapo watu mashuhuri kama Bill Gates na mkewe Melinda, mwanamuziki Alicia Keys, mwigizaji wa sinema wa Hollywood Richard Gere wa Gere Foundation nk walikuwepo. Uzinduzi huu ulifanyikia ndani ya Rogers Centre hapa Toronto. Nimeandika zaidi kuhusu habari hii kwenye blog yangu ya kimombo!

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 8:29 PM | Permalink | Maoni 3
Wednesday, August 09, 2006
AFRICAN GUITAR SUMMIT
Hawa ni baadhi ya wanaojulikana kwa pamoja kama African Guitar Summit. Ni kwamba wanacharaza magitaa kuliko kawaida.Hapa walikuwa wakifanya vitu vyao kwenye tamasha la AfroFest hapa Toronto mwezi uliopita. Ukiikuta CD yao popote ulipo na kama unapenda muziki wenye nakshi za magitaa na ngoma basi usisite kuinunua.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:42 AM | Permalink | Maoni 5
Wednesday, August 02, 2006
KETI TUZUNGUMZE

Ni kipindi cha joto kali sana hapa Canada na hata hapo kwa jirani Marekani. Jana joto la hapa Toronto na maeneo ya jirani lilifikia nyuzijoto 36! Na kwa sababu ya viwanda na mioshi kama inayotoka kwenye magari basi tunaongelea nyuzijoto zaidi ya 40! Tayari watu kadhaa,hususani wazee,washakata roho kutokana na joto hilo.

Kutokana na hilo,sina budi kujikita zaidi ofisini au nyumbani.Uzururaji hauna budi kupungua. Hapo ndipo ninapopata muda wa kusoma mengi,kujiuliza maradufu,kupiga hesabu za mamilioni bila kuwa na senti mfukoni. Hapo ndipo nikakutana na
makala hii hapa, imeandikwa na Magabe Kibiti (simfahamu). Nikahisi damu inanisisimka, msimamo wangu unajulikana. Lakini nikaona huu unaweza kuwa mjadala mzuri sana ndani ya ulimwengu wetu wa blogu. Ndio maana nauweka hapa, wewe unasemaje kuhusu mtazamo huu? Je,ni kweli kwamba hatuna chetu?

NB: Nimekuwekea picha kama kiburudisho tu, picha hiyo ni kutoka tamasha linaloitwa
Caribana. Inasemekana ndio tamasha kubwa kupita yote hapa Amerika ya Kaskazini linalohusu tamaduni za watu wanaotokea visiwa vya Caribbean.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:36 AM | Permalink | Maoni 2
Thursday, July 27, 2006
HII NI NJAA,TAMAA AU UKWELI NA MUHIMU?
Nimekutana na habari hii leo asubuhi, nimeshindwa niseme nini,niongee na nani,nimlaumu nani au hata nimpige nani konde. Hivi kwanini lakini,kwanini kwa jina la Tanzania ambayo si mali ya mtu mmoja bali wananchi wote,wakuzaliwa na wakuletwa toka bara hindi na kokote duniani?

Alichokifanya huyu ni tofauti na kile alichowahi kukifanya Emil Muta? Inabidi serikali iunde sheria mpya ya matumizi ya jina la nchi kwa faida binafsi? Hivi kwanini jamani?Hebu nisaidieni kwa mawazo hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:51 AM | Permalink | Maoni 4
Thursday, July 20, 2006
AMARA KANTE

Huyu anaitwa Amara Kante. Nilimuona siku chache zilizopita akifanya tambiko na ngoma zake kwenye tamasha la AfroFest mwaka huu hapa Toronto. Ukisikia amekuja katika mji uliopo nenda kamtazame,hususani kama wewe ni mpenzi wa ngoma.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:08 PM | Permalink | Maoni 2
Sunday, July 16, 2006
DAR ZIPO MBILI?
Kijasho chembamba kinatoka,leo jua limewaka kwelikweli.Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kwamba ukiona jua limewaka namna hiyo ujue malaika aliyeko zamu ya kuwasha na kuzima jua kwa siku hiyo ana roho mbaya sana,au pengine ni mlevi na pombe ya jana bado haijamtoka kichwani hivyo kalala na kusahau kurekebisha mambo. Alah! kumbe malaika nao wako namna hiyo jamani?

Kituo cha mabasi Mwenge, leo kimejaa watu ile mbaya.Naambiwa eti wengi wanaenda downtown kutafuta riziki.Mbona naona kama wameshachelewa?Mchana wote huu jamani,kwani nyie hamuamini kwamba biashara ni asubuhi,jioni mahesabu?Aaa wapi..mbona kanuni za dunia ya leo zinasema biashara jioni,watu wakishatoka makazini?

Leo nimeamua kuchukua njia hii ya kutokea Mwenge baada ya jana kutumia ile ya Ubungo..au barabara ya Morogoro.Waswahili bwana..mpaka niseme Morogoro Road ndio nitaeleweka.Rafiki yangu Ndoga anayeishi huko Uholanzi(nchi ya aina yake hii..ukitaka kuwa bwabwa sawa tu,ukitaka kuuza mwili wako poa tu,ukitaka kula uroda kwenye bustani za jiji twende tu,ukitaka ku..twende tu..ama kweli) kaniambia jambo ambalo sina budi kulithibitisha kwa macho yangu na akili zangu chache.Kasema eti ukielekea mjini kwa kutumia Moro rd na ukitumia hii ya "mzee ruksa" eti utaona jinsi gani Dar ni jiji moja lenye tabaka mbili tofauti.

Labda nianze na nilichokiona jana.Taa ya kijani inawaka,konda anamuamuru dereva akanyage mafuta.Mpiga debe wake anakimbiza gari,hajapewa ujira wake wa kupayuka(hivi ina maana Dar watu wengi hawajui kusoma nini?Sasa kwanini mtu apasue mishipa namna ile?) Duh,karibuni jamaa akanyagwe aisee..hivi kwanini? Naona wananchi kibao pembezoni mwa barabara,naambiwa hawa ni wafanyakazi wa viwanda kama UFI na URAFIKI..ama kweli..kwanini viwanda hivi viwe karibu namna hii na makazi ya watu?Hali ya hewa je?Hapa si ndio Shekilango..pale kwa Lowassa majuzi?Hivi nani karekebishwa? Mara tunafika mahakama ya ndizi...kama huna koo jepesi unaweza rudisha chenji(yaani unaweza tapika).Kwanini ndizi ziuzwe namna ile?Hivi wachaga na wahaya wanajisikiaje wakiona chakula chao kikuu kinadhalilishwa namna hii?

Tunafika Manzese..hii ndio Kibera au Mathare ya Tanzania. Eti kuna mtu anaitwa afisa mipango jiji hapa.Naona kale kanjia ka kuelekea uwanja wa fisi(kama hupajui shauri yako). Hivi vijana wote hawa ni wachuuzi wa mitumba? Mbona basi uwiano ni kila kijana mmoja kwa mtumba mmoja? Naanza kuvuka daraja maarufu la Manzese..naliangalia naona "masela" wameweka chata...Barcelona! Hata sielewi Barcelona na Manzese ina uhusiano gani.Sishangai sana..mbona mbele kidogo ni Manzese Argentina? Maradona..okay.

Naendelea kukata mbuga...Kagera,mwembechai..hali ni zilezile..wazee nje wanacheza bao.Vijana wanajaribu kuchuuza kila wanachoweza..kila tunaposimama wauza maji,nyembe,turi nk wapo madirishani.Survival for the fittest..ushawahi kuiona hiyo senema? Naingia mitaa ya jangwani sasa...ama kweli...naziangalia kwa chabo nyumba za wananchi wenzangu. Maisha.

Leo sasa,gari inakamata Ali Hassan Mwinyi,kondakta kasimama mlangoni,mlango kafunga vizuri kabisa.Ohh kumbe gari hili lina kiyoyozi bwana! Kila abiria amekaa kwenye kiti.Naona watu wana sura tofauti huku.Wengine wanasoma magazeti ya mchana...nachungulia naona kichwa cha habari..kama kawaida..Kikwete na Lowassa kiboko.Sina sababu ya kununua gazeti nadhani,habari ni zile zile.Tofauti na jana naona upande huu watembea kwa miguu ni wachache.Kila kituo naona wakinadada warembo wanasubiri usafiri.Wakiingia kwenye gari,mashalah..manukato! Huku naona ofisi nyeti za kiserikali.Naona taasisi ya kukuzia mitaala(mitaala gani,sijui..mbona mambo ni yale yale?),naona tvt,ooh nyuma tushapita makao makuu ya habari Tanzania(aipipiii)..duh hata chuo cha posta kipo huku...alah..hata tume ya sayansi kumbe?

Mbele nakuta kituo cha mafuta chenye pampu nyingi kupita vyote afrika mashariki..hivi ni kweli? Lakini nyuma tumeshapita majengo mazuri na ya kisasa kabisa hapa Bongo.Hata wazungu(sio kwamba wao ni watu zaidi yetu) nawaona kibao huku.Ndani ya magari mazuri wakati wengi wao "vihiyo" tu. Naona kituo cha polisi..oysterbay! Duh huku watu wanauza maua rozi...huku ni nchi nyingine bwana.ati.Kule kwa jana..thubutu...nani wa kununua maua?Nipo mbuyuni..nakumbuka Kessington Market kule Toronto..jamaa anauza vitu vya anasa..vya watalii.Natamani nishuke..hapana nitashuka siku nyingine.

Nashangaa mahali pako kimya namna hii..sorry nilisahau kwamba hapa ndio Oysterbay penyewe,wanapokaa we... wa nchi hii.Kwa mbali nasikia mbwa anabweka. Fanya fujo uone..naona balozi za nchi za wenyewe zilivyojipanga. Bahari hii hapa...duh beach la Barcelona hili nini?

Las Vegas Casino..wait..hivi nipo wapi?California Dreamer..you must be kidding me! Mbele yangu nauona mtaa wa mabenki..benki zote za nje hizi..Namwambia konda anishushe hapo Delinews..nataka kumsalimia Michuzi. Ama kweli..hivi hii ni Dar moja au mbili?
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 1:21 PM | Permalink | Maoni 3
Friday, July 14, 2006
ULINZI MKALI!

Wakati wa kombe la dunia ulinzi ulikuwa mkali kupindukia. Hapo ndio utajua kwamba kitumbua kimeshaingia mchanga na mdudu ndani ya kokwa la embe keshaanza kutotoa wenzake. Tazama kwa makini picha hii.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:32 AM | Permalink | Maoni 0
Monday, July 10, 2006
MTIHANI KWA KIKWETE?

Katika ile safu yangu ya kila jumapili kule Tanzania Daima,wiki hii niliongelea suala la ushabiki mtupu wa kisiasa jambo ambalo kwa mtazamo wangu halina manufaa yoyote kwa nchi kama Tanzania.Ukitaka kuisoma nilichoandika kuhusu "ushabiki" bonyeza hapa.

Nilichokuwa nikikizungumzia ni kusihi tuachane na ushabiki ambao umejaa maneno matupu na wala sio vitendo ambavyo kisayansi ndio vinavyotakiwa kutumika ili kufanya tathmini ya utendaji wa serikali "mpya" ya Tanzania. Tuache "JK kweli kiboko"..Lowassa anatisha za kisiasa nk.Lazima tuwe na matendo ya kumfanya mtu awe anatisha au kiboko na sio maneno ya kwenye majukwaa ya siasa ambayo wote tunafahamu yana ukweli au uongo kiasi gani.

Baada ya kuwa nimeandika waraka wangu huo leo limejitokeza hili.Lisome zaidi hapa. Je hii kasi mpya na ile ahadi ya kupitia upya mikataba itafanyaje katika hili?Haya ndio mambo ambayo hatuna budi kuyaandika vizuri kwenye majarida yetu ili siku za mbeleni tuulizane kwa ufasaha bila ushabiki.

Habari za World Cup zitakuja soon,naziandaa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 12:40 PM | Permalink | Maoni 5
Sunday, July 02, 2006
TEKINOLOJIA INAPOWEZESHA!
Mara nyingi sana Ndesanjo amekuwa akielezea na kunadi jinsi ambavyo tekinolojia inazidi kuiunda upya dunia yetu. Jinsi ambavyo tekinolojia inazidi kuwa tishio kwa wale ambao ni wakoloni wa hata habari pia. Tekinolojia za habari kama hizi za blogu, tunazoandikamo masuala mbalimbali yanayohusu jamii kwa matarajio ya kujenga na wakati mwingine hata kubomoa ni nyanja inayokua kwa kasi sana na mfano mzuri wa mapinduzi haya. Habari ni haki na ni nguvu pia.

Kwa wiki kadhaa hapa Canada pamekuwepo na malumbano makali sana kuhusu imam mmoja wa huko Uingereza anayeitwa
Shaykh Riyadh Ul Haq.Baadhi ya vikundi vya kidini na hata kijamii hapa Canada viliiomba serikali kutomkubalia huyu bwana kuja Canada ambako alikuwa amealikwa aje kutoa mihadhara kadhaa kwenye mkutano wa vijana wa kiislamu ambao unaendelea hapa Canada. Mkutano huo umeandaliwa na The Islamic Foundation ya hapa maeneo ya Toronto.Hoja zao ni kwamba jamaa anatoa mihadhara inalenga katika kujenga chuki miongoni mwa wanajamii nk nk. Jamaa wa uhamiaji waliridhiana na maombi ya wanajamii hao na hivyo kumzuia jamaa asipande kabisa ndege kwa minajili ya kuja Toronto.

Sasa kilichotokea ni kwamba jamaa amehutubia mkutano huo kwa kutumia tekinolojia,akiwa huko huko ofisini kwake Uingereza huku vijana wakimsikiliza kwa utulivu wa aina yake.Leo hii anaendelea kuhutubia mkutano huu na hata pia kuwa na wakati wa maswali na majibu na vijana hao.Upo hapo?Soma zaidi
hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:38 AM | Permalink | Maoni 2
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker